RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Profesa Paramagamba Kabudi, amesema Serikali itahakikisha taswira ya nchi inalindwa na kwamba walitumia kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN), kufafanua tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.
Profesa Kabudi alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2019/20, ambapo aliomba kuidhinishiwa Sh bilioni 166.9 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
“Katika kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN), tulitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu tuhuma za upotoshaji unaofanywa mara kwa mara, kuwa kuna ukiukwaji wa haki za binadamu nchini,” alisema.
Profesa Kabudi alisema Tanzania iliitaarifu jumuiya ya kimataifa namna Serikali inavyotimiza misingi ya haki za binadamu kama ilivyobainishwa katika katiba na mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania ni mwanachama.
Alieleza Serikali itaendelea kuhakikisha taswira ya nchi inalindwa kila mahali pale shutuma dhidi ya nchi zinapotolewa.
“Niendelee kuzisihi jumuiya za kimataifa, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kushauriana na Serikali pale ambapo wanahisi kuna tatizo kabla ya kutoa shutuma,” alisema Profesa Kabudi.
Alisema Tanzania inaongozwa na misingi ambayo lengo kuu ni kudumisha amani, ulinzi, usalama na mshikamano wa wananchi kama ilivyowekwa na waasisi wa taifa mara baada ya uhuru.
“Katika kutekeleza hilo, Tanzania imeendelea kulinda uhuru wetu, kujiamulia mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa, kulinda mipaka ya nchi, kulinda haki, kuimarisha ujirani mwema na kuunga mkono sera za kutofungamana na upande wowote,” alisema.
Alisema Tanzania inashirikiana na nchi wanachama wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM), hususan nchi zinazoendelea, kulinda na kutetea masilahi ya pamoja katika mijadala ya kimataifa.
Profesa Kabudi alisema katika kutekeleza azma hiyo, Tanzania ilishiriki mkutano wa mawaziri wa NAM mwaka 2018, uliofanyika Baku nchini Azerbaijan.
“Misingi hiyo ndiyo inayotufanya tujivunie kuwa taifa lenye amani, ulinzi imara na usalama duniani, kuwa mstari wa mbele kutetea wanyonge, haki na uhuru, kutafuta amani na kutatua migogoro na kuwa kimbilio kwa wananchi wa mataifa mengine,” alisema.
NAFASI YA TANZANIA KIMATAIFA
Kuhusu nafasi ya Tanzania kimataifa, Profesa Kabudi alieleza kuwa inaheshimika kutokana na mchango wake katika masuala mbalimbali duniani ikiwa pamoja na kudumisha ulinzi na usalama.
Pia alisema Tanzania inaheshimika kimataifa kutokana na juhudi zake za kupambana na rushwa, dawa za kulevya, utakatishaji fedha, kutetea masuala ya haki za binadamu na kuunga mkono misingi ya demokrasia na utawala bora.
MSIMAMO WA TANZANIA KIMATAIFA
Profesa Kabudi alisema msimamo wa Tanzania kuhusu mgogoro wa Israel na Palestina ni kuendelea kuzingatia msingi uliowekwa na waasisi wa taifa, ambayo ndiyo nguzo ya sera ya mambo ya nje kupigania haki ya kujitawala, kuheshimu mipaka na kuunga mkono maazimio ya jumuiya ya kimataifa.
Alisema Tanzania inaunga mkono maazimio ya UN na Umoja wa Afrika (AU) kuhusu mgogoro huo na itaendelea kushauri pande husika kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa.
“Tanzania inaamini kwamba suluhisho la kudumu katika mgogoro huu ni kuwa na nchi mbili ambazo zitaishi kwa pamoja ikiwa ni Palestina huru na Israel salama,” alisisitiza.
Kwenye mgogoro kati ya Morocco na Sahrawi katika eneo la Sahara Magharibi, alisema Tanzania inaunga mkono juhudi za UN na AU kwa pande zote kushiriki mazungumzo ya namna bora ya kutatua mgogoro huo.
Alisema katika mijadala hiyo, Tanzania imeendelea kuzisihi pande zote kukaa meza moja kupata suluhu ya kudumu.
“Tunapongeza mazungumzo yaliyofanyika Desemba mwaka jana, Geneva nchini Uswisi kati ya pande mbili, ni matumaini yetu kuwa suluhu ya mgogoro huo itapatikana mapema,” alisema.
Pia, alisema urejeshaji wakimbizi wa Burundi nchini mwao kwa hiari unafanyika kwa uweledi kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za nchi.
Hata hivyo, alisema kuna watu wachache wenye nia ovu, hususan wanaodai kuwa ni Warundi waishio kweye baadhi ya nchi za Ulaya, walianzisha kampeni chafu dhidi ya Tanzania kuwa inawalazimisha wakimbizi hao kurejea kwa nguvu.
MAONI YA KAMATI
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, mjumbe wa kamati hiyo, Cosato Chumi, alisema kuna umuhimu Serikali kuharakisha mchakato wa kupatikana sera ya taifa ya Diaspora.
“Sera hiyo itawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa, hususan kiuchumi, jambo ambalo kwa sasa halifanyiki kutokana na kukosekana mwongozo wa namna ya kuwashirikisha,” alisema.
Aidha, alisema kamati inashauri fedha zinazotengwa kwa ajili ya safari za kikazi za viongozi wa kitaifa nje ya nchi, zitolewe moja kwa moja na hazina bila kupitishwa katika fungu la wizara.
UPINZANI
Kwa upande wa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, msemaji kwenye wizara hiyo, Salome Makamba, alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kuipa kipaumbele wizara hiyo.
“Ndiyo maana mataifa yaliyoendelea huwa na mpango mkakati katika wizara zao za nje,” alisema.