Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ameanza kazi rasmi kwa kumtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuanza mabadiliko wizarani hapo.
Profesa Kabudi ambaye hata hivyo hakusema ni mabadiliko ya aina gani yanahitajika wizarani hapo, amesema hayo leo Jumatatu Februari 4, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuapa kuwa waziri wa wizara hiyo baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, juzi.
“Lazima tubadilike na tutambue mabadiliko haya ni sisi wenyewe ndani ya wizara mabadiliko ya haraka, huo ndiyo ujumbe wangu na ahadi yangu kwa watu wote,” amesema.
Pamoja na Profesa Kabudi, pia Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Augustine Mahiga aliapishwa na baadhi ya Makamishna wa Jeshi la Polisi.