PROF. TIBAIJUKA: BAJETI HAIJAWASAIDIA WA TETEMEKO

0
709

 

 

Na KULWA MZEE-DODOMA

MBUNGE wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), amesema bajeti ya mwaka 2017/18, haijatenga fedha kuwasaidia wananchi wa Bukoba walioathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka jana.

Profesa Tibaijuka aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akichangia bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Waathirika wa tetemeko hatuoni ni kwa jinsi gani bajeti hii itakavyotusaidia,” alisema Profesa Tibaijuka.

Pamoja na hayo, aliomba viwanda vya vifaa vya ujenzi, vifunguliwe ili kuwasaidia watu kujenga makazi yao, kwani wengi wao wanapata ugumu wa kununua vifaa vya ujenzi kwa kuwa vinauzwa kwa gharama kubwa.

Katika maelezo yake, alitolea mfano mfuko wa saruji ambao Dar es Salaam alisema unauzwa kwa Sh 9,000 na Bukoba unauzwa kwa Sh 15,000.

Naye Mbunge wa Nkenge, Balozi Deodorus Kamala (CCM), akizungumzia biashara ya mazao, alisema vibali vya kuvusha mazao eneo la Mtukula vinatolewa kwa upendeleo.

“Nilipopata taarifa hizo, nilizifuatilia na kubaini ndani ya Bunge kuna wabunge wanapewa vibali kuvusha bidhaa Mtukula… uchafu gani huu.

“Nawaomba waache tabia hiyo kwani wakulima nao wanataka kuvusha mazao,” alisema Dk. Kamala.

Kwa pande wake, Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF), alisema bajeti hiyo ni ya kusadikika kwa kuwa makusanyo ya fedha yako kwa ajili ya kulipa deni la taifa.

“Deni la taifa ni zaidi ya Sh trilioni 50 na kila mwezi tunatakiwa kulipa Sh trilioni 1.3 wakati makusanyo ya kila mwezi ni Sh trilioni 1.4.

“Hatuhitaji madeni chechefu, yaani madeni yasiyolipika kwa sababu Rais Kikwete aliacha deni la taifa likiwa ni Sh trilioni 39.1 na baada ya Magufuli kuingia madarakani, mpaka sasa deni hilo limepanda na kufikia Sh trilioni 50,” alisema Salim.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here