25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Prof. Tibaijuka atangaza kutogombea tena ubunge

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), amesema hatagombea tena nafasi ya ubunge Uchaguzi Mkuu ujao.

Profesa Tibaijuka aliyepata kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa Serikali ya awamu ya nne, alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na mtandao wa Millard Ayo.

Pamoja na mambo mengine, alisema anastaafu kwa sababu yeye ni kizazi cha Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliwafundisha kung’atuka.

“Mimi 2020 ninastaafu, ninang’atuka kwa sababu sisi ni kizazi cha Mwalimu Nyerere na katika vitu alivyotufundisha ni kung’atuka.

“Katika uchaguzi wa 2015, Muleba Kusini pamoja na kampeni ya Escrow bado nilipita kidedea, kwa kweli nawashukuru wananchi wa Muleba, ni watu wanaotafuta maendeleo, wana kiu ya maendeleo.

“Na ninaposema nastaafu ubunge, haimaanishi kwamba nastaafu Muleba, hivi ni vitu viwili tofauti, mimi ninastaafu uwakilishi, Bunge letu hili lingekuwa Seneti ningesema nitaendelea.

“Lakini sasa ni Bunge la Uwakilishi, hatuna Bunge la Seneti, yaani Bunge ambalo sasa hoja zinalinda masilahi mapana ya umma, hapa tunawakilisha wananchi na mimi naamini tunaweza kupata mwakilishi mzuri wa Muleba,” alisema.

Alisema anaamua kung’atuka si kwa sababu ya kuhofia kushindwa, kwani ingekuwa hivyo angeshindwa katika uchaguzi uliopita kutokana na kampeni chafu juu yake.

“Mimi kama kupigwa chini, ningepigwa chini mwaka 2015 au sio. Asiyekubali kushindwa si mshindani, kwa hiyo mimi sistaafu kwa ajili ya hofu, kwanza Muleba anayenishinda ni nani? Ni Mwenyezi Mungu peke yake.

“Kwa kipindi cha miaka 10 nimejifunza, nimeelewa matatizo ya wananchi na wakati ule nilipotoka Umoja wa Mataifa, nilikuja na nia moja ya kujifunza kwamba taifa letu lina tatizo gani.

“Tufanye nini ili tuweze kusogea mbele, kwa hiyo hata bungeni ninaposimama, nikiona kitu hakijakaa sawa huwa sisimami kiitikadi, pia sitaki ushabiki ambao hauna mantiki,” alisema.  

Mwanasiasa huyo ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), alisema sasa anarudi kwenye jamii akiwa kama mwanaharakati.

Akizungumzia kuhusu jambo lililomuumiza akiwa waziri, alisema mgogoro wa ardhi ulimpa wakati mgumu sana.  

“Nakumbuka wakati ule nilikwenda Loliondo kukumbana na mgogoro wa ardhi, nilitembea siku hiyo na Wamasai kijiji kimoja nikiweka mipaka kuzuia watu na hapo nilikuwa nimeitwa na Mkuu wa Mkoa na baadaye nikaenda na Waziri Mkuu wa wakati ule, Mizengo Pinda.

“Kwakweli katika vitu vyote ambavyo vilikuwa vigumu kwangu ni mgogoro wa ardhi, lakini kazi ya ardhi haikunishinda, nilipambana,” alisema Profesa Tibaijuka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,211FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles