NA MWANDISHI WETU
-MKURANGA
WAZIRIÂ wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Â amewataka wanafunzi wa shule za sekondari Mwinyi na Nasibugani kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa kuacha kujiingiza kwenye vikundi au mambo ambayo hayana tija kwa maendeleo ya Taifa.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo jana wakati alipofanya ziara wilayani Mkuranga mkoani Pwani, kwa lengo la kukagua ujenzi unaoendelea wa vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule hizo ambao unatekelezwa na programu ya Lipa kulingana na matokeo.
Profesa Ndalichako alisema jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli za kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa wanafunzi zinapaswa kuungwa mkono kwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kufaulu vizuri.
Waziri Ndalichako amesisitiza kuwa Serikali haihitaji kuona wanafunzi wanafeli bali inataka kuona wanafunzi wanafaulu ambapo amewasihi walimu kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia weledi.
Naye Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), alimshukuru Waziri Ndalichako kwa kutatua kwa wakati changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu.