27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Prof. Mbarawa kupambana na madereva wazembe

mbarawanewNa ESTHER MNYIKA -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ametoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wote wa malori ya mchanga na kokoto watakaobainika kutofuata sheria za ubebaji wa bidhaa na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo juzi mkoani Kigoma katika ziara yake ya kukagua Barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa kilomita 50, ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla, hivyo haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombinu hiyo kwa makusudi.

“Kuanzia sasa Serikali haitavumilia madereva wasiozingatia kanuni na sheria za usafirishaji wa mizigo katika barabara nchini, hivyo nawaagiza mameneja wa Tanroads katika mikoa yote nchini kusimamia sheria ili kudhibiti miundombinu ya barabara,” alisema Prof. Mbarawa.

Profesa Mbarawa ameliomba Jeshi la Polisi kushirikiana vema na makandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wanaiba vifaa vya makandarasi jambo linalochangia kukwamisha shughuli za ujenzi wa barabara.

Kutokana na hali hiyo amewataka wananchi wa Wilaya ya Kasulu kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara hiyo ili kuwezesha ujenzi huo kukamilika haraka.

Naye Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, alibainisha changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni wizi wa mafuta na vifaa vya ujenzi hali inayosababisha mradi kusuasua.

“Wananchi tambueni kuwa fedha hizi ni za kwenu mnapohujumu vifaa vya ujenzi ni dhahiri mnajicheleweshea maendeleo na kukwamisha fursa za kiuchumi katika wilaya yenu,” alisema Choma.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi, Mekbib Tesfaye anayesimamia mradi huo kutoka Kampuni ya DOCH Limited, amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24 ambapo kwa sasa kazi inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili na makalvati katika barabara hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles