24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Lodhi: Kusweka rumande watu kulimsononesha Mwalimu Nyerere

160377-004-ecb7bcbd

NA SARAH MOSSI,

WIKI iliyopita katika sehemu ya pili ya simulizi ya Profesa Maalim Abdul-aziz Lodhi alizungumzia namna uasi uliofanywa na waliokuwa wanafunzi wa Mlimani (sasa UDSM), mwaka 1966 ulivyochangia kuharakisha kuanzishwa kwa Azimio la Arusha.

Profesa Lodhi ambaye naye aliswekwa rumande akidaiwa kushiriki maandamano hayo. Katika sehemu hii anazungumzia uhusiano wake na Mwalimu Nyerere ikiwa ni maalumu tukiadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere Oktoba 14. Endelea…

MTANZANIA: Miaka 50 tangu kufanyika kwa maandamano yale itatimia Oktoba 20, mwaka huu, Je, mmepanga kufanya nini mkikumbuka kadhia ile?

PROF. LODHI: Hakuna sherehe yoyote iliyopangwa na mtu yeyote, jambo hili halifai kusherehekewa lakini linastahili kuadhimishwa kwa sababu ni mualama (milestone) muhimu katika historia ya nchi yetu.

Wasomi na wanahistoria wanapaswa wayachambue masimulizi ya matokeo hayo ili habari kamili na sahihi zipatikane, ziandikwe vyema na kuhifadhiwa. Mansoor Ladha wa Canada ameyaeleza kwa upande wake mambo haya katika kitabu kitakachotolewa mwezi ujao.

Tanzania ilikuwa imefika njia panda na watawala iliwabidi waendeleze mweleko wa elimu uliohitajika. Ninavyoona, Tanzania ilikuwa haina budi Azimio la Arusha litungwe na siasa rasmi ya elimu ya kujitegemea ifuatwe kuleta haki, usawa na maendeleo kwa walio wengi; tena ilitubidi tuuondoe miongoni mwa sehemu kubwa ya wale waliokuwa wameelimika ule ujeuri wa kiusomi waliojipatia baada ya kugharimiwa elimu na majasho ya makabwela.

Halafu tena, “majaribio” ya kiujamaa yakashindwa ni masimulizi mengine, maendeleo ya ujamaa yalihujumiwa hasa na viongozi wa viwango vya kati na chini na wengi wa viongozi wa kiwango cha juu walijigeuza kuwa miungu midogo. Mwalimu Nyerere alikuja kubaini hayo lakini baadaye sana. Ndiyo maana aliniambia siku moja kwamba “Mapinduzi ya Tanzania Bara na Zanzibar yamesalitiwa na viongozi wetu! Watanzania wamesalitiwa na viongozi wao!

Nataka kuongezea kidogo kuhusu yale mabango yaliyobebwa na wanafunzi kwenye maandamano ya Oktoba 1966, niliambiwa na baadhi ya wanafunzi (marehemu Wilson Tibaijuka akiwa mmojawapo) kwamba mabango machache yenye maneno ya kibaraka na ya kihaini kama vile “Remember Indonesia!” na “It was better before!” yalitengenezwa na wanafunzi waliokuwa wanachama wa Tanzania Youth League (TYL) na walioshawishiwa na Profesa Chagula na viongozi wa tawi la TYL la Chuo Kikuu kuyahujumu maandamano.

Profesa Chagula pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Huduma Ya Taifa na alikuwa anazozana na  viongozi wa Dar es Salaam University Students’ Union (DUSU).

Siku chache kabla ya maandamano, kamati ya DUSU ilipinduliwa na kamati mpya kabisa ilichaguliwa. Kamati hiyo ndiyo iliyoyapanga mandamano. National Union of Tanzania Students (NAUTS) ilikuwa haijahusika na hayo. Vile vile, maandamano yalikuwa yenye amani kabisa; hakukutokea kelele wala fujo yoyote na wanafunzi wote waliandanama kwa ukimya. Na walipokamatwa na polisi na wanajeshi kule Ikulu, wanafunzi hawakuleta upinzani wowote. Polisi walibeba silaha nzito nzito.

MTANZANIA: Katika mazungumzo yako inaonekana mlikuja kuelewana na Mwalimu Nyerere nini kilitokea?

PROF. LODHI: Ndio baadaye tulikuja kuelewana na nilikuwa nazungumza na Mwalimu mara nyingi, wakati mwingine ananiita nyumbani kwake na wakati fulani tulisafiri pamoja kwenda Swaziland na kurudi.  Mwalimu alikuwa akifikiri sana kwa Kiingereza na wakati mwingine anatafua maana ya maneno hayo kwa Kiswahili hapati jibu na hivyo alikuwa akiniuliza sana mimi.

Wakati mwingine neno analipata kwa Kiswahili anatafsiri mwenyewe kwa Kiingereza. Siku moja aliniambia kama angepata nafasi ya kuandika au kutafsiri upya mabepari asingetumia neno hilo

MTANZANIA: Kwanini unadhani Mwalimu Nyerere alifikiria hivyo?

 PROF. LODHI: Aliniuliza siku moja kwa Kiingereza lakini kwa sababu wakati anapokuwa anapata hisia anaongea Kiingereza, akaniuliza ” What went wrong… tell me what went wrong” Sikuwa na jawabu la haraka, lakini nikamjibu “May be our definition was too narrow, in return even a Store owner or owner of a  Kioski was a dirty capitalist. Anyone dealing with money was a dirty capitalist according to our definition, and those who were deciding were the worst people na bureaucracy”.

Ndio maana wao walikuwa wanapinga kama Rais Mwinyi alivyosema safari moja kwa “Socialism is good for everybody not for us”

MTANZANIA: Inaonekana mlikuwa karibu sana na Mwalimu?

PROF. LODHI: Ndio, kwa hakika mwaka 1963 mwanzoni tulitayarisha mchezo wa Julius Caesar kwenye Radio Zanzibar, tulitayarisha sisi All Zanzibar Students Union akina Mzee li Baramia.

Mimi nilimwandikia barua Mwalimu ya kutumia hiyo na alitujibu haraka na alifurahi na ukaanza kuchezwa katika Sauti ya Unguja wakati ule. Halafu mwaka 1966, nikakutana na Mwalimu kwa mara ya kwanza.

Baada ya hapo tukaendelea kukutana mara kwa mara na siku moja alinialika katika Birthday ya mtoto wa kaka yake aitwaye Sophia alikuwa akikaa naye na ndipo nikakutana na mama yake. Nimo katika kuandika habari hizi.

MTANZANIA: Una jambo gani la kukumbuka katika uhusiano wako na Mwalimu?

PROF. LODHI: Ninakumbuka mkutano wangu na Mwalimu wa dakika 50 uliofanyika katika chumba chake alichokuwa akikitumia pale ukiingia tu nyumbani kwake.

Aliniambia siku hiyo nisiende na Tape recorder. Hiyo ilikuwa ni Julai, 1994, baada ya kurudi naye Swaziland na kwa kupitia Katibu Muhtasi wake alimwambia anipatie wakati wa kukutana naye.

Wakati huo nilikuwa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Taasisi ya Kiswahili akaleta gari ya CCM aina ya Landrover inifuate. Nakumbuka tukiwa katika hicho chumba ambacho kuta zake zilikuwa zikiipa mgongo bahari pale Msasani na siku hiyo bahari ilikuwa imechafuka na mawimbi kweli kweli (anacheka).

Tulikuwa tunazungumza habari za watu kutiwa ndani na Mwalimu kuweka saini kila mwezi kurefusha watu waendelee kukaa rumande wasiletwe mahakamani.

Nikamwuliza imekuwaje, kuna watu wamekaa ndani miaka kumi, akaniuliza watu gani hao unawajua? Nikamjibu ndio nawajua, nikamtajia na nikamwambia na hawa wamefanya kazi na wewe. Basi kila nikisema hivyo akawa akigeua uso wake upande mwingine.

Nikamwuliza swali, Mwalimu wewe si ulikuwa ukiletewa makaratasi yenye orodha ya watu wanaotakiwa kuendelea kukaa rumande na ulikuwa ukisaini, hivyo ndivyo katiba ya nchi inavyotaka akasema naam, naletewa makaratasi nasaini nilikuwa siangalii na sipati nafasi ya kusoma kila kitu ati.

Nikamwuliza Mwalimu wewe ulikuwa unachukua dhamana ya nchi nzima, unaletewa waraka husomi? Akajibu mimi nilikuwa nawaamini wenzangu. Nikamwambia Mwalimu hapa hatuna tape recorder hutoweza kunishitaki kwamba nimekuvunjia heshima, lakini nakuuliza swali, hukuwa na udadisi wowote kujua watu gani hawa waliotiwa ndani? Akageuza uso tena.

Nikamwambia ninavyofikiri mimi bila shaka mwanzoni hii orodha ilikuwa kurasa moja au mbili lakini baadaye ilikuwa ukurasa 50 au 60 akageuza uso wake tena. Ghafla akanijibu hii ndio kazi yenu nyie wasomi tafuteni ukweli. Nikamwambia hatuwezi kutafuta ukweli kama hatuna hizo karatasi pengine zimeshachomwa moto.

Baada ya hapo ghafla wimbo moja kubwa likaja na kwenda moja kwa moja kwa Mwalimu na kulowesha suruwali yake, Mwalimu akaruka na kusema “ Hee hata bahari inanichukia”

Simulizi hii ya Profesa Lodhi inayohusu maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu waliomuasi Mwalimu na uhusiano wake na Mwalimu itaendele wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles