24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Lipumba akumbuka mapambano ya zamani CUF

Leonard Mang’oha -Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameelezea jinsi chama hicho kilivyopambana kutafuta haki, akiwataka wanachama kutokata tamaa katika kutafuta haki.

Profesa Lipumba alisema hayo jana Dar es Salaam katika kongamano la miaka 19 ya vurugu zilizotokea Januari 26 na 27 mwaka 2001 baada ya wananchi visiwani Zanzibar kuandamana wakitaka kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi na kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba kutokana na karoso zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Alisema kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 watu wengi walihamasika na kukifanya chama hicho kuwa na nguvu kubwa jambo ambalo liliifanya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kukataa kusimamia vema uchaguzi na hatimaye ikatangaza kurudiwa uchaguzi huo.

Profesa Lipumba alisema kuwa kutokana na uamuzi huo, wananchi visiwani humo waliamua kufanya maandamano Januari 2001 wakishinikiza kupatikana Katiba yenye msingi wa demokrasia kwa Tanzania Bara na Zanzibar, Tume Huru ya Uchaguzi ya Zanzibar na Tanzania, pamoja na kuwapo kwa utawala bora unaozingatia utawala wa sheria.

Alisema kutokana na maandamano hayo, Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kubwa kuwatawanya waandamanaji ambapo watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa, huku baadhi wakikimbilia nchi jirani ya Kenya na kusababisha Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia kuwa na wakimbizi.

“Mkapa (Rais mstaafu Benjamin Mkapa) ameandika kitabu akieleza kuwa hili ni moja ya mambo ambayo yalitia doa uongozi wake na anasema wahanga walilipwa, ukweli ni kwamba tulihojiwa na Tume ya Hashim Mbita, wakati huo Maalim Seif alikuwa Uingereza.

“Tanaikumbuka siku hii kwa sababu watu walipoteza maisha kwa kudai haki ambayo mpaka sasa haijapatikana na lazima tuendelee kuidai kwa sababu mikwara na makucha ya CCM  ni mabaya kuliko ya mkoloni. Tulikuwa tunafanya mikutano ya siasa, sasa hivi mikutano ya siasa hairuhusiwi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kwa kuwa hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli,  aliwaahidi Watanzania kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu utakuwa huru na haki, ni vema sasa atamke mara moja kuwa mikutano ya hadhara imeruhusiwa ili kuthibitisha kauli yake hiyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya aliwataka wanachama na Watanzania kutorudi nyuma katika kudai haki na usawa kwa wote.
Sakaya alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1992, hakijawahi kurudi nyuma katika kudai haki.

Alisema pamoja na shuruba mbalimbali wanazozipata hawatarudi nyuma katika kudai haki kwa wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles