Prof. Kabudi, Rais Barrick wakata mzizi wa fitina

0
1156
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu makubaliano ya uanzishwaji wa Kampuni ya pamoja ya uchimbaji madini ya Twiga inayomilikiwa na Serikali na Barrick. Katikati ni Rais wa Barrick, Mark Bristow na Ofisa Mkuu Mtendaji, Willem Jacobs.

*Wazindua kampuni ya pamoja ya Twiga, kesi zote zafutwa


FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

SERIKALI kwa kushirikiana na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation wamemaliza mzizi wa fitina kwa kutangaza ukurasa mpya ikiwamo kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya madini Twiga Minerals Company Ltd.


Kampuni hiyo itasajiliwa nchini na kuwa na Makao makuu yake jijini Mwanza baada ya kufutwa kwa kampuni ya Acacia.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya kutambulisha kampuni hiyo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi, alisema katika kampuni hiyo ya Twiga, Barrick watakuwa na umiliki wa asilimia 84 huku Serikali ikimiliki asilimia 16.


“Nikiwa Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli ya kufanya majadiliano na makampuni mbalimbali ya madini ikiwamo Kampuni ya Barrick, ninayofuraha kuwatangazia watu wote duniani kuwa sasa Barrick na Serikali ya Tanzania wameunda kampuni moja ya Twiga Minerals Company Ltd na itakuwa na makao makuu yake jijini Mwanza.


“Kampuni hii ya Twiga ndiyo itakayosimamia migodi ya Buzwagi Bulyanhulu na North Mara ambapo katika migodi hiyo katika kila mgodi Serikali itakuwa na asilimia 16 na Barrick 84 kama ilivyo kwa Twiga,” alisema Prof. Kabudi.


Prof. Kabudi alisema kuwa kuundwa kwa Kampuni hiyo kumetokana na kufutwa kwa kampuni ya Acacia ambayo Barrick Gold ilikuwa na umiliki wa asilimia 63.9 huku nyingine zikiwa kwa wanahisa wadogo hivyo Barrick kuamua kununua hisa zote na kufikisha hisa asilimia 100 za umiliki kisha kuifuta kampuni hiyo ambayo ilikuwa na makao makuu yake jijini London, Uingereza.


“Hivyo tunavyozungumza hivi sasa ofisi ya Acacia mekufa, haipo na badala yake imekuja Kampuni ya Twiga na maana yake ni kwamba Ofisi ya jijini London nchini Uingereza ambayo ilikuwa inatumia fedha nyingi imefungwa na badala yake shughuli zote zitafanyika hapa nchini Tanzania, hivyo leo (jana) ni siku kubwa, ni siku ya ushindi kwa Barrick lakini pia ni siku ya ushindi kwa Tanzania.


“Kama mtakumbuka Machi, 2017 Rais Dk. Magufuli alitutangazia wananchi wa Tanzania na dunia kwamba tuna mgogoro na Kampuni ya Acacia iliyokuwa inaendesha migodi mitatu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara kwa vitendo ambavyo vilikuwa vinatufanya sisi tupoteze mapato na ambavyo havikufaa.


“Hivyo kuunda tume mbili na baada ya hapo tukawa katika mgogoro mkubwa ndipo mwenyekiti wa Barrick, Prof. John Thornton alipoamua kuja nchini kufanya mazungungumzo na Rais Magufuli ambapo baada ya kikao hicho ndipo tukakubaliana kuanza mazungumzo.


“Tulianza mazungumzo na timu ya mwanzo ya Barrick Julai 31, mwaka 2017 ambayo yalikamilika Oktoba 19, mwaka 2017 kw akutia saini makubaliano kati ya Serikali na kampuni ya Barrick ambapo tulikubaliana, kwanza kuchangia faida za kichumi 50/50, kuunda kampuni mpya, kuhakikisha tunabadilisha muundo wote wa uendeshaji wa kampuni hiyo.


“Kufunga ofisi ya fedha iliyokuwa Johannesburg Afrika Kusini na mambo yote ya fedha kufanyika hapa nchini ambayo yanaendana na mabadiliko tuliyoyafanya na kufunga ofisi ya London,” alisema Prof. Kabudi.


Aidha, alisema kuwa mara baada kukamilika kwa mazungumzo hayo ya awali, Oktoba, mwaka 2017 serikali ilianza majadiliano ya kina ya kujadili nyaraka mbalimbali ambapo yaliendelea na kufika mahala akaanza kusuasua.


“Lakini jambo kubwa lilitokea Januari mwaka huu ambapo kampuni ya Land Gold Resources ya Afrika Kusini ambayo awali Mark Bristow (Mtendaji Mkuu wa Barrick kwa sasa alikuwa mmiliki wake) iliamua kuungana na Kampuni ya Barrick.


Katika kuungano huo, Bustow baada ya kufanikiwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Barrick alitamka kwamba wanataka kumaliza mgogoro uliopo Tanzania ili warudi Tanzania ili warudi Tanzania kwa ubia, mwelekeo na mtizamo mpya ambao utakuwa na maslahi kwa pande zote mbili.


“Ndipo Msimamizi wa shughuli ukanda wa Afrika na Mahariki ya kati, Dk. Willem Jacob alifika hapa nchini Novemba 23, mwaka jana tukaanza mazungumzo ambayo yalienda vizuri sana ambapo tumekamilisha nyaraka tisa, na sasa kwa mujibu wa sheria ya serikali nyaraka hizo zote tumezipeka kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili zipitiwe kwa mujibu wa taratibu za kiserikali.


“Hivyo tunaamini kuwa hadi kufikia Novemba 15, waka huu shughuli hiyo ya mapitio ndani ya Serikali itakuwa imekalimika na ndipo nyaraka nyingine zitatiwa sahihi chini ya kampuni hii mpya ya Twiga Minerals Corporation Ltd,” alisema Prof. Kabudi.


Awanyooshea kidole wakosoaji
Katika hatua nyingine Prof. Kabudi mbali na kuwashukuru watendaji hao wapya wa Barrick pia aliwanyooshea kidole wale waliokuwa wakiamini kuwa serikali ya Tanzania ilikurupuka kuibana Acacia na kwamba ingeshindwa mahakamani.


“Kwanza niwashukuru watendaji wapya wa Barrick kwani ni watu ambao wamekuja katikati na kununua kampuni na kuamua kununua na matatizo ya kampuni, tulipoanza mazungumzo haya Julai 31, 2017 wapo waliosema kwamba hatutaishinda Acacia, wapo waliotabiri kwamba Acacia watatushitaki na nikweli kwamba Acacia walitushtaki wakidai mamilioni ya pesa.


“Lakini leo (jana) haya ninayoyasema yamedhihirisha kabisa kwamba, Rais Dk Magufuli alikuwa na hoja na hoja hiyo imefanikiwa kwa Acacia kufa na kuundwa Twiga kulikowezeshwa na Bristow na hivyo kufanya kesi zote za London kufa na madeni kufa.


“Hivyo wale waliodhani tutalipa mamilioni ya fedha imekufa, Acacia imekufa, madeni yamekufa sasa tunaanza ubia mpya chini ya kampuni hii ikiwa na maana kwamba sasa hakuna kampuni London wala Afrika Kusini inayosimamia migodi hii badala yake hawa vitu vyote vitasimamiwa hapa ndani hiyo ndiyo tofauti ya barrick ya sasa na ya zamani kwani kampuni inayosimamia sasa ya Twiga ni ya kitanzania, imesajiliwa Tanzania na itakuwa na makao makuu hapa, hivyo leo ni mwanzo wa safari mpya ya mafanikio ya sekta ya madini nchini hivyo kampuni nyingine za madini ziige mfano huu,” alisema Prof. Kabudi.


RAIS WA BARRICK
Awali akizungumza kwenye hafla hioyo, Rais ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow alisema kuwa kufikiwa kwa makubaliano ya kuundwa kwa kampuni hiyo mpya ya Twiga utakuwa ni mwanzo mpya wa Tanzania na raia wake kuanza kunufaika na rasilimali zake za madini ikilinganishwa na huko nyuma pamoja na kufuta mzozo wa muda mrefu baina ya serikali na Acacia.


“Sote tunafuraha kuona kwamba leo tumefungua ukurasa mpya na serikali ya Tanzania kwenye sekta ya madini kupitia uundwaji wa kampuni mpya ya Twiga hivyo sisi kama Barrick tunaamini kuwa huu ni mwanzo mpya wa watanzania kuanza kunufaika na raslimali zao za madaini wanazozimiliki, pia ni ukomo wa mzozo uliodumu kwa muda mrefu baina ya serikali ya Tanzania na Acacia.


“Pia kufikiwa kwa makubaliano hayo kutatoa mwanya mpana kwa serikali kushiriki moja kwa moja kwenye sekta hii ya madini ikiwamo kufanya maamuzi, uendeshaji na shughuli nyingine ikilinganishwa na huko nyuma ambako kulikuwa na changamoto kadha wakadha.


“Lakini pia niweka wazi kwamba fursa za ajira kwa watanzania ni kubwa kwani tayari kuna Watanzania ambao wameajiriwa na kupata mafunzo kwa ajili ya kuziba pengo la wafanyakazi waliondoka ambapo kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakitekeleza majuku yao ipasavyo,” alisema Bristow.


Katika hatua nyingine alisema kuwa kampuni hiyo iko kwenye mkakati wa kuhakikisha kuwa inarejea kwenye soko la hisa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here