28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Kabudi aanza kwa kutoa onyo, Mahiga aeleza msoto Mambo ya Ndani

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amewatahadharisha watu wanaoisema vibaya nchi na kuwataka wakae kimya.

Akizungumza jana baada ya kuapishwa kutumikia wizara hiyo, alisema huu si wakati wa kuisema vibaya au kuibeza nchi.

“Nchi yetu si ya kuchezewa, kudharauliwa, kudhihakiwa, kama umeshindwa kusema yanayofaa kwa nchi yako kaa kimya.

“Tunahitaji kuwaambia watu wengine nchi hii ni ya kidemokrasia ili isonge mbele na wananchi wapate maendeleo,” alisema Profesa Kabudi.

Aliahidi mabadiliko makubwa katika wizara hiyo na akasema yataanza na viongozi hivyo wasisubiri kubadilishwa.

“Jana (juzi) haikuwa siku ya amani kwangu, kwanza hukuniarifu (akiamaanisha Rais Magufuli), lakini nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii tena. Nakuhakikishia utumishi, utii, uaminifu katika kutumikia nafasi hii.

“Tuna kazi moja tu ya kufanya mabadiliko ndani ya wizara, tena haraka sana. Mabadiliko haya yaanze na sisi wenyewe na tusipobadilika tutabadilishwa…tusisubiri tubadilishwe,” alisema.

Naye Dk. Augustine Mahiga, aliyeapishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, alisema lazima nchi iwe tayari kupambana na wapotoshaji kwa kuwafanya marafiki wake wawaelewe na kuielewa awamu ya tano inataka nini.

“Hivi karibuni kumekuwa na malumbano ya wazi kabisa lakini kwa jitihada za wizara yangu (akimaanisha alipokuwa Mambo ya Nje) tumeeleza na kuainisha sera na mwelekeo wetu.

“Watu wengi wanajua Tanzania kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita lakini tunawaambia Tanzania imebadilika ina utawala mpya unaosisitiza uwajibikaji, ndio maana kuna sera ya kupambana na rushwa na ufisadi, kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kuwafikia wananchi kwa kuwapa haki zao,” alisema.

Alisema Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa na changamoto ya kujirekebisha ndio maana wamekuwa wakiwahamisha hamisha baadhi ya watumishi.

“Nimejitahidi niwezavyo kujaribu kuweka wizara katika misingi ambayo watumishi wake ndani na nje wanakuwa tayari kutekeleza siasa, nchi yoyote lazima iweke misingi ya kisiasa katika jumuiya za kimataifa.

“Leo tunaweza kusimama na kusema Tanzania ina marafiki wengi, hatuna adui duniani na siasa yetu ya kutofungamana na upande wowote imetusaidia kutupa heshima,” alisema.

Alisema pia amesimamia kuandika upya sera ya mambo ya nchi za nje ili kuweka mwelekeo wa diplomasia ya uchumi.

Kuhusu majukumu mapya katika Wizara ya Katiba na Sheria, alisema yatamuwezesha kuwa karibu na Bunge, watu na Serikali.

“Nimeshiriki kutengeneza katiba za nchi tano, katiba yangu naifahamu na nitafanya kazi na vyombo vingine, hii pia ni imani kubwa sana, wizara ambayo ndiyo kitovu cha Serikali na amani yetu,” alisema Dk. Mahiga.

Alisema pia sasa atakuwa karibu na familia yake tofauti na awali ambapo majukumu yalimfanya apate muda mchache kukaa na familia.

“Nimesafiri usiku na mchana, kuna wakati nalala saa mbili wakati mwingine mwezi mzima familia yangu naweza kuwaona siku mbili au tatu, lakini sasa nitakuwa karibu na familia yangu,” alisema.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema; “Watanzania wanapokuwa nje waisemee vizuri nchi yetu, mmetuona tukiwa wakali sana, si tabia yangu lakini wakati mwingine inakera. Kuiweka nchi mahali pazuri ni jambo linalofurahisha,” alisema.

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwataka mawaziri hao wakajifunze kwa haraka na kutambua vipaumbele vilivyopo katika wizara zao.

“Tuna mwaka mmoja tu wa kukamilisha ahadi zote za CCM, hivyo mkajifunze kwa haraka mtambue vipaumbele vilivyopo kwenye wizara zenu kulingana na namna Rais alivyowaahidi Watanzania,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles