Eliud Ngondo – Mbeya
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda, ameishauri Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kutoa mikopo kwa raba kwa watoto wanaotoka familia zinazojiweza kiuchumi na kusomesha bure wale wanaotoka familia masikini.
Profesa Bisanda alisema mfumo wa sasa wa kutoa mikopo kwa wanafunzi kutoka familia masikini, unaongeza mzigo kwa bodi na wanaopewa mikopo hiyo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa Serikali ya Wanafunzi ya chuo hicho kutoka kwenye matawi yake nchi nzima, alisema kitendo cha kuwakopesha wasiokuwa na uwezo ni kuwaongezea mzigo wa maisha haswa ikizingatiwa sasa mfumo wa ajira ni mgumu.
Alisema endapo wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kifedha wataendelea kukopeshwa, itakuwa ni kazi kurejesha mikopo hiyo kwani hawatapata ajira na riba ya mikopo itaendelea kuongezeka kila mwaka.
Prof. Bisanda alisema endapo watasomeshwa bure na bodi, watakuwa wamepunguziwa mzigo wa deni na hivyo hata wasipopata ajira na wakaamua kujiajiri, itakuwa rahisi kwao kuendesha maisha yao na kuwasomesha wengine.
Alisema watoto wa matajiri wakikopeshwa ni rahisi kurejesha mikopo hiyo hata kama hawataajiriwa baada ya kumaliza masomo yao ya elimu ya juu na wakisharejesha fedha hizo zinarudi tena kwenye mzunguko wa mkopo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuanzisha mfumo huu wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi, ni kweli wanasaidia hata watoto wa masikini kupata elimu ya vyuo vikuu, lakini mtazamo wangu ni kwamba utaratibu huo hausaidii sana.
“Mtazamo wangu ni kwamba Serikali ingetenga fungu la fedha kwa ajili ya kuwakopesha watoto wa matajiri ambao watakuwa na uwezo wa kurejesha pamoja na riba na hiyo riba irudi kusaidia watoto wa maskini kwa kusoma bure,” alisema Prof. Bisanda.
Alisema utaratibu huo wa kuwasaidia watoto wa masikini unatakiwa uendane na viwango vya ufaulu kwa maelezo kuwa kinatakiwa kiwekwe kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi anayestahili kusomeshwa bure.
Hata hivyo aliwataka wanafunzi wa OUT ambao wengi ni watumishi kutopenda kusoma kwa kutegemea mkopo kwa maelezo kuwa mkopo ni utumwa wa maisha ya baadaye.
“Unapokopa ujue unakula maisha yako ya baadaye leo maana utalazimika kulipa mkopo huo na riba juu, lakini ukipambana ukajisomesha mwenyewe utakuwa huru sana,” alisema Prof. Bisanda.
Vilevile alisema utaratibu wa bodi ya mikopo kutaka vyuo vikuu kuwasilisha sahihi za wanafunzi waliopokea mikopo yao ndani ya siku 30, ni mwiba kwa chuo hicho kwa maelezo kuwa wanafunzi wa chuo hicho wamesambaa nchi nzima na hivyo ni vigumu kuwapata wote kwa muda huo.
Alisema baadhi ya wanafunzi wanaishi vijijini na hivyo akaomba bodi hiyo iwape siku 90 za kuwasilisha sahihi hizo kwa maelezo kuwa muda huo ndio utatosha kuwafikia wanafunzi wa matawi yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Awali Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Felix Lugeiyamu, alisema chuo hicho kina mfumo mzuri wa uongozi ambao unawashirikisha pia wanafunzi kwenye majukumu ya utawala.
Alisema Serikali ya menejimenti ya uongozi wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho umeandaa mradi maalumu wa kufundisha Watanzania uzalendo kwa taifa lao na kwamba mradi huo utawafikia wananchi wote.
“Mradi huu utagharimu Sh milioni 300 na tunaamini zitapatikana, pia sisi kama menejimenti tumesaidia mambo kwenye chuo ikiwa ni pamoja na kununua jenereta kwa ajili ya kituo cha Lindi na viti kwa kituo cha Morogoro,” alisema Lugeiyamu.
Alisema wao wanaamini uzalendo ni imani kama ilivyo kwa imani zingine na hivyo watahakikisha wanasambaza imani hiyo mpaka ngazi ya familia ili kuchochea maendeleo ya taifa.