25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

PROF BAREGU: NI VIGUMU PROFESA KUFANYA KAZI NA RAIS MAGUFULI

                Profesa Mwesiga Baregu

Na EVANS MAGEGE

PROFESA Mwesiga Baregu amekuwa na umaarufu wa aina yake katika medani za siasa za upinzani kwa muda mrefu sasa. Ingawa aina ya siasa ambayo amekuwa akiiendesha si ya mikikimikiki ya majukwaani, lakini kauli zake zimekuwa na tafsiri pana katika jamii.

Profesa Baregu licha ya kuwa mhadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali nchini pia anatumikia nafasi ya mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema na mlezi wa vijana wa chama hicho.

MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano naye yaliyolenga maswala mbalimbali ya kitaifa, ukiwamo mwenendo wa siasa za nchi pamoja na afya ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

MTANZANIA Jumapili: Wiki iliyopita Serikali iliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, ukiwa ni mtaalamu wa siasa unayazungumziaje mapendekezo hayo?

Profesa Baregu: Sijui nizungumze nini…. Kwa kifupi ninaweza kusema kwamba sioni la maana kujadili Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini unasema hivyo?

Profes Baregu: Huu ni mtazamo wangu,  nasema hakuna la maana kwa sababu naamini fedha zitakazotengwa na kupitishwa na Bunge, matumizi yake yatabadilishwa kinyemela na mtawala.

Kwa msingi huu naomba nikwambie kuwa ni bora nifuatilie matangazo ya mpira wa miguu kuliko kujadili mapendekezo hayo kwa sababu historia ya bajeti inayokwisha muda wake ilichezewa sana na mtawala ambaye ni dhahiri  anadhani anayo mamlaka ya kutumia fedha kinyume na malengo ya wapitishaji wa bajeti hiyo.

Bunge ndilo linaloikabidhi Selikali kusimamia fedha kwa maana ya kiasi gani kitozwe na kitumikeje, hivyo kwa ujumla Bunge ndio mamlaka yenye nguvu ya kifedha na si mtawala lakini tumeona kwa bajeti iliyopita mambo yamevurugwa, yanakwenda kinyume na taratibu sasa sijaona mantiki ya kufuatilia bajeti ya mwaka huu kwa kuwa yanaweza kujirudia yaleyale yaliyojitokeza katika bajeti ya mwaka 2016/17.

MTANZANIA Jumapili: Chadema bila Dk. Wilbrod Slaa unaionaje?

Profesa Baregu: (Kicheko), Chadema bila Dk. Slaa naiona inakwenda vizuri sana. Lakini lazima nikiri kwamba mwanzoni wote tulishtuka kwa sababu tulikuwa tumemzoea sana na kwa sehemu kubwa alikuwa amechangia katika kukijenga chama, kukitangaza na kukiendesha.

Dk. Slaa alikuwa amejitambulisha kama mwana-Chadema wa ukweli na ujue Katibu Mkuu ni mtu mkubwa ndani ya chama kwa sababu yeye ndiye anayendesha chama kama taasisi.

Kwa maana kama angeondoka tofauti na alivyoondoka au kwa lugha nyepesi angeondoka kwa maridhiano tungemmiss sana.

MTANZANIA Jumapili: Kwa maelezo yako unamaanisha hamjammiss Dk. Slaa?

Profesa Baregu: Kwa sababu  alivyoondoka kisaliti saliti na katika kipindi kigumu cha kampeni za uchaguzi, hilo lilitusaidia kwa kiasi kikubwa kuvumilia hali ngumu na hali hiyo ikatulazimu tujihami kwanza kuelekea kwenye uchaguzi mkuu na pili kuelekea kumpata Katibu Mkuu mpya.

Najua tulijihami vizuri na mafanikio tuliyapata makubwa na si tu ya kuongeza idadi ya wabunge.

Kwa mantiki hiyo pamoja na Dk.Slaa kuondoka tulivuka salama kwenye uchaguzi na msingi wa hali hii unatufanya tusimmiss kabisa kwa sababu ilionekana ushindi unawezekana bila yeye. Wanachama wamejiamini kwa mtazamo wa kwamba hakuna kurudi nyuma.

Kwa msingi huu kwa sasa tunaye katibu mkuu mpya ambaye anaendelea kujengeka na kujiamini, unajua huyu kijana ni daktari wa binadamu kwa sasa amejikuta mahali papya, lakini kwa uwezo wake ameweza mpaka sasa naona jahazi la Chadema linakwenda vizuri.

MTANZANIA Jumapili: ACT-Wazalendo kuingia serikalini kunamaanisha nini?

Profesa Baregu: Hili jambo ni endelevu inawezekana Anna Mghwira akachukuliwa huko kwenye chama chake kama msaliti, lakini binafsi katika siasa za vyama vingi tunapaswa kuvumiliana.

Wengi waliamini ACT-Wazalendo imempoteza mtu muhimu. Kwamba amekwenda nje ya wigo wa upinzani. Kisiasa tunasema kajiunga na upande mwingine, hapo kuna wengine wanaona hilo ni jambo jema kuwa Rais Magufuli hana uchama na anasimamia maendeleo.

Binafsi hili suala la Mama Mghwira ninaweza nikasema limeamsha maswali mengi katika jamii, ni kiasi gani tumejitafakari wote na kujiuliza ni wangapi wako kwenye upinzani kwa ajili ya fursa?

Kwamba wako kwenye upinzani kunaweza kutokea viti maalumu kwenye uchaguzi ujao nikapata au inawezekana niko upinzani kwa sababu wanataka ubunge au wako upinzani kwa sababu wanataka udiwani, kwa ujumla watu wa aina hii wapo kwenye upinzani kutafuta fursa binafsi na si fursa ya kijamii.

Lakini kuna wengine tuko upinzani kwa fursa za kijamii kwa maana ya fursa kwa Watanzania kujibadilisha, kupiga hatua za kimaendeleo, kupata uhuru zaidi wa kisiasa, kuamua mambo yao na kuyasimamia au kidhibiti Serikali zao wanazozichagua.

Ukiwa kwenye upinzani kwa maana ya fursa ya kijamii ambayo ni pana huwezi kurubuniwa kwa vitu vidogo vidogo kama hizi nafasi za kuteuliwa.

Tofauti na hivyo labda iwe kwamba tunaelekea katika Serikali shirikishi.

Lakini kwetu sisi wanasiasa kwa mfumo tulionao wa vyama vingi vya siasa basi uwe ni mfumo wa mazungumzo baina ya vyama badala ya kurubuni mtu mmoja mmoja na kuchomoa watu.

Kama una nia njema na mfumo wa vyama vingi na una imani kuwa ni mfumo ambao unasaidia nchi kusonga mbele na hutaki kuupiga vita, basi zungumza na vyama vya wenzako, muelewane kama unahitajika mfumo wa aina hiyo kwamba mnataka kulifanikisha kikatiba, kisheria au liwe jambo la muda kwa maana ya kuongoza siasa za nchi.

Tofauti na hivyo basi wale ambao wanateuliwa nafasi hizo kama vile Profesa Kitila Mkumbo au Mama Mgwira wanaongozwa kwa fursa zao binafsi. Lakini kwa upande wa pili rais hana nia njema, si kwamba anawateua waende kupeleka maoni ya upinzani lakini wanakwenda kule kutumikia Ilani ya CCM.

Kwa hiyo nia ya Rais si tu anataka kudhohofisha upinzani bali ni kuua  upinzani kuanzia sera zake.

Sasa hayo ni huko ACT–Wazalendo lakini sijui akigeukia Chadema, maana anaweza akaona wazo lake ni zuri, kumbuka katika hili chama hasa kinacholengwa ambacho ni tishio ni Chadema.

Kwa hiyo napenda kuwaambia wana-Chadema wakae chonjo maana hata yeye rais alisema kwamba kule Chadema kuna watu wanamlilia kumuomba.

Sasa ukiipima kauli hii unabaini nia yake anataka kutuchonganisha sisi Chadema kwamba tuanze kujitazama kwa kuhoji ni nani amekwenda Ikulu kumuomba rais, ukurugenzi au ukuu wa mkoa.

MTANZANIA Jumapili: Kwa upande wako, ikitokea rais akakuteua kutumikia nafasi yoyote ndani ya Serikali yake, uko tayari?

Profesa Baregu: Hapana

MTANZANIA Jumapili: Kwanini?

Profesa Baregu: Kwa sababu mara ya mwisho nimetumikia Taifa hili wakati nilipoteuliwa na kupata heshima ya kuwekwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tukafanya kazi kubwa na nzuri lakini matokeo yake ya aibu mkayaona.

Kwahiyo binafsi nikisema kuwa sitakubali nafasi yoyote ya kuteuliwa, nitakuwa ni mwongo lakini ikitokea rais anaamua kurudi kwenye mchakato wa Katiba Mpya na akanihitaji kusaidia hili suala la Katiba kurudi kwenye maridhiano, nitakubali ili kuisaidia nchi hii kukamilisha zoezi ambalo lilianza vizuri tena kwa gharama kubwa alafu likaachwa kama pagale.

MTANZANIA Jumapili: Tofauti na kazi hiyo, ikitokea ukateuliwa kwa kazi nyingine utafanyaje?

Profesa Baregu: Hiyo nyingine nimeshastaafu, nimefikisha miaka 73 nadhani haiwezekani, la msingi ni hili la Katiba yaani hata kesho niko tayari kumsaidia rais. Lakini kazi nyingine ambazo ni za kisera kwa mfano binafsi huwezi ukanipa Ilani ya CCM halafu ukaniambia nifanye kazi kwa kuifuata nitaikataa.

Nimekuwa kwenye maoni tofauti tangu tunapigania Katiba mpya na ile Sheria ya vyama vingi ambayo ilikuja kupatikana mwaka 1992.

Mimi nilikuwa ni mmoja wa wajumbe wa mkutano ulioanzisha Kamati ya Kutaka Katiba Mpya Tanzania mwaka 1990, Sasa miaka 27 nimekuwa katika msimamo huo leo nikubali Ilani ya CCM, si hata wajukuu wangu watanishangaa na nitaonekana msaliti kuanzia ngazi ya familia.

MTANZANIA Jumapili: Unaizungumziaje Afya ya Ukawa pia hali ya kisiasa ndani ya CUF.

Profesa Baregu: (anashusha pumzi kidogo), Labda tuanze na hili la CUF. Kwa ujumla hali ya kisiasa ndani  CUF ni tete nadhani hilo sihitaji kueleza.

Ni kwa bahati mbaya Profesa Ibrahim Lipumba tunaheshimiana sana na tulichukua shahada za uzamivu pamoja nchini Marekani kwenye chuo kikuu chenye heshima sana cha Stanford.

Kile chuo huwa kinashindana na Chuo Kikuu cha Harvard kwamba kipi cha kwanza na kipi cha pili, kwa hiyo ni chuo kimoja chenye heshima sana duniani na kawaida vyuo hivi vinajenga mshikamano kati ya watu ambao mmepitia kimasomo ndani ya vyuo hivyo.

Kwenye vyuo hivyo, kuna mambo ambayo mnajifunza kwamba hayafanywi na mtu yeyote wa kusoma kwenye vyuo hivyo, hiyo ni katika kujenga maadili ya wahitimu wa vyuo hivyo kwamba ukifanya hiki hutaeleweka kama ulisomea chuo hicho.

Sasa mwenzangu Profesa Lipumba sijui. Binafsi nilimwita tuzungumze na tulikutana nyumbani kwake kama mwanachuo  mwenzangu, nikamuuliza kulikoni akanijibu ameamua kurejea kwenye uongozi wa CUF kwa sababu chama kilikuwa na kiashiria kuhatarisha muungano.

Nilimsikiliza  lakini sikuona sababu zenye mashiko, tukaongea mengine kisha tukaachana.

Tukirejea kwenye swali lako kuu ya afya ya Ukawa, ninaweza kusema  Ukawa inaendelea vizuri ingawa baadhi ya vyama washirika wana mivutano ya hapa na pale ambayo nayo wako ukingoni kuivuka, NCCR–Mageuzi mmeona baadhi wamejitoa kwenye chama na wengine kujiunga CCM, CUF ndio hali hiyo inayojulikana, lakini Chadema tuko imara na tunaendelea na mshikamano wa Ukawa kama kawaida.

MTANZANIA Jumapili: Unaizungumziaje nidhamu ya viongozi vijana ndani ya Chadema hususani wabunge ambao wamesimamishwa kutohudhuria mikutano ya Bunge kwa takribani mwaka mmoja?

Profesa Baregu: Tuseme tu ukweli kwamba maadili ndani ya Taifa yameporomoka, tusiwalenge vijana pekee, watu wazima nao wengi wao wamekosa maadili.

Kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba nimezunguka nchi nzima na sisi kama tume tumeliona hilo.

Nikirudi kwenye swali lako la msingi,  kwa hawa vijana wetu kule bungeni siwezi kusema tu kwamba ni suala la maadili pekee.

Kwanda kutoonyeshwa kwa Bunge mubashara kumechochea vituko ndani ya Bunge, kwa kuwa wabunge wenyewe wanatambua hawaonekani mubashara wamekuwa na mengi wanayoyafanya huko, pia kumbuka kwamba kumekuwa na mbinu nyingi za kuwavuruga wabunge wa upinzani.

Wakati mwingine inapoonekana wanavurugwa, kwa uchungu nao wanajikuta katika hali ya kukabiliana na mvurugano na matokeo yake ndio haya tunayoyaona kwa vijana wetu kufungiwa vikao vya bunge.

Ili kujiepusha na hali hii, uongozi wa Bunge unatakiwa kuwa na ngozi ngumu kuweka hali ya usawa pindi mvutano unapotokea.

Kuhusu hali ya nidhamu ndani ya Chadema, kwa kifupi ninaweza kusema jambo hilo tumeliona na tayari uongozi umeniteua kuwa mlezi wa vijana.

MTANZANIA Jumapili : Umekuwa katika siasa za mageuzi kwa muda mrefu, kwanza unastaafu lini siasa. Umefanikiwa nini na nini kimekushinda?

Profesa Baregu: Kwanza binadamu kaumbwa kisiasa kwa hiyo siwezi kustaafu siasa angali niko hai.

Pili, katika siasa nimefanikiwa mengi  na kubwa kuliko yote ni Taifa kuwa na mfumo wa vyama vingi. Nimekuwa nikipigania mfumo wa vyama vingi kwa miaka mingi na baada ya TANU kufa na kuzaliwa kwa CCM, mimi na wenzangu wachache tulisimama pamoja kuendesha vuguvugu la kudai mfumo wa vyama vingi mpaka hapo ulipopatikana mwaka 1992.

Kuhusu nini nimeshindwa, ninaweza kusema kwenye hili suala la kupata Katiba Mpya limekuwa gumu kidogo, lakini sijakata tamaa nitaendelea kupambana.

MTANZANIA Jumapili: Rais anachagua maprofesa wenzako kuitumikia Serikali yake, unalionaje suala hili, je kuna mapinduzi katika uongozi?

Profesa Baregu: Hapana hilo swali ni gumu kulijibu moja kwa moja (anacheka). Ni swali gumu kwa sababu usije ukanigombanisha na wenzangu ila niseme kwa kifupi tu kwamba kila mmoja ana dhamira yake, kuna baadhi ya hao ambao wameteuliwa walinipigia simu au mimi niliwapigia kuwapongeza na kuwapa pole.

Niliwapongeza kwa maana kuwa wamepewa dhamana kubwa ya kuwatumikia Watanzania, lakini kuwapa pole kwa kuteuliwa chini ya uongozi ambao hauonyeshi usikivu.

Inaelekea watu ambao wamesimama na kuongozwa na weledi wa ujuzi wao kidogo wanapata shida.

Kama profesa unateuliwa, kwanza anatakiwa asipokee upokezi wa kifursa kwamba anashukuru Mungu kuwa amepata fursa ya kumalizia nyumba yake. Profesa anatakiwa apokee uteuzi kama dhamana, tena ajiamini atachangia kwa hilo aliloteuliwa na kwamba atakuwa na uhuru wa kutosha wa kufanya mchango wake, lakini katika mazingira yaliyopo binafsi naona magumu kwa mfano mimi huwa nikiamini jambo lazima nilisimamie na hali hii imeniumiza sana huko nyuma kwenye kazi zangu  na ningeteuliwa leo ingekuwa mbaya zaidi.

Kuna dhana ya hapa kazi tu  na mimi nachagiza kidogo ‘hapa kazi tu fikra marufuku’.

Na kwa wakati mwingine ukimsikia anasema kwamba watamchelewesha. Sasa watu kama maprofesa  dhana yao kuu ni hapa fikra tu, kwamba kazi inakwenda baada ya fikra.

Kwa mfano rais alichukua uamuzi wa kununua ndege Bombardier kwa msingi wa kufufua ATCL. Hiyo ni kazi ya fikra ingefanywa kabla ya kununua ndege. Sasa Profesa hapo unafanya nini?

Hivi karibuni maprofesa waliteuliwa kuunda kamati ya kuchunguza makinikia, lakini wakasahau uchunguzi wa wao peke yao hauna maana.

Makontena yale ya mchanga ni mali ya Kampuni ya Acacia, sasa unakwendaje kukagua mali ya mtu wakati mwenyewe hayupo? Je ataaminije kwamba hukumbambikiza?

Hili swali iliwapasa maprofesa wangemshauri rais kwamba angalau ukaguzi ungefanyika na wenye mali na hata ingebidi wangetafuta mtu wa tatu ambaye atakuwa katikati kuwapatanisha pale panapotokea tafsiri tofauti kuhusu uchunguzi.

Kwa mtazamo wa jumla tu, rais aliwatuma maprofesa hawa wafanye kazi ya kisiasa ya kutangaza na kuibua uzalendo na sasa hivi ukipinga mambo ya makinikia, utaonekana si mzalendo kabisa, lakini tujiulize sheria  na mikataba ilizosababisha haya ni za nani?

Kwa hiyo walichokifanya hawa maprofesa ni jambo ambalo linaweza kugharimu uprofesa wao kwa ujumla kwa sababu wamefanya jambo ambalo linawaweka kwenye kundi wale wasiosoma. Najua hawataipenda lakini ni mtazamo wangu katika hili.

MTANZANIA Jumapili: Unaizungumziaje sera ya viwanda?

Profesa Baregu: Nadhani dhana ya viwanda bado haijaeleweka vizuri. Picha ya kwanza ya viwanda ni sawa na kutaka kufanya mabadiliko ya uchumi lakini ikiwa hauna teknolojia, hauna nyenzo unataka kubadilisha nini?

Kama unataka kuimarisha dhana hii, unaangalia asilimia 80 ya wakulima, kwa hiyo tija kubwa ya uzalishaji ndani ya nchi hii ipo kwenye kilimo, kwa mantiki hiyo kuna kipindi cha mpito ambacho viwanda vikue kutokana na uzalishaji wa watu wengi na kuongeza tija katika uzalishaji.

Mpaka sasa mpango wa viwanda na fikra yake bado zijaiona. Nadhani dhana ya viwanda kwao wanafikiria viwanda kimoja kipo Kibaha kinginge kipo Mkuranga. Msingi unatakiwa kuwa marejeo ya fikra kwamba pale kuna kiwanda cha aina hii na kitanufaisha wazalishaji kiasi kadhaa. Lakini kusema viwanda kwa kuhesabu kwamba vingapi vipo mkoa huu inaweza isiakisi uzalishaji wa wananchi.

Sikatai kwamba kuwa na wazo la viwanda ni vizuri lakini fikra za viwanda zinatakiwa kujengwa kwenye vichwa vya watu kama walivyofanya china.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Hongera Profesa Baregu! uwezo wakuona mbali ulionao umesababisha ujiepushe na mambo mengi yanayoweza kupandikizwa pasipo wewe kujua! Ni kweli Maprofesa waliokuwa kwenye kamati zote mbili “Usomi wao” umedhalilishwa na wanasiasa!

    HONGERA SANA PROFESA! MUNGU AKUPE MAISHA MAREFU!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles