23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Prof.Asad azungumzia sakata la kuondolewa kwenye nafasi ya CAG, umuhimu wa katiba mpya

Na Clara Matimo, Dodoma

Aliyekuwa Mdhibiti  na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Asad, amezungumzia sakata la kuondolewa kwenye nafasi hiyo mwaka 2019 na kubainisha kwamba liligubikwa na maswali mengi kutoka kwa watu wa kada tofauti tofauti kwa kuwa anaamini aliondolewa kwa kutofuata katiba.

Profesa Mussa Juma Asad (katikati) akizungumza  jijini Dodoma kwenye mdahalo  uliolenga kujadili kitabu cha Rai ya Jenerali na Uukuu wa Katiba Tanzania ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).Picha na Clara Matimo.

Profesa Asad amebainisha hayo Oktoba 6, jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye mdahalo uliolenga kujadili kitabu cha mwandishi nguli wa habari, Jenerali Ulimwengu mada zikiwa ni miaka 25 ya Rai ya Jenerali, demokrasia na masuala yanayohusiana na katiba nchini ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambao uliwakutanisha wanazuoni kutoka vyuo mbalimbali, wabunge, viongozi wa Chama Cha wanasheria Tanganyika (TLS), Tume ya Haki za Bindamu na Utawala Bora ( THBUB) na waadishi wa habari.

Amesema anakerwa kuitwa CAG Mstaafu kwa sababu kuondolewa kwake kwenye  nafasi hiyo kulienda kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 144  ambayo inaweka  wazi sababu zitakazosababisha kiongozi huyo aondolewe madarakani.

“Sababu hizo ni kama CAG atatimiza miaka 65 sasa mimi leo Octoba  sita mwaka huu 2021 ndiyo nimetimiza miaka 60, atashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na ugonjwa au sababu nyingine, utovu wa nidhamu na kwenda kinyume na maadili, yote hayo mimi sikuyafanya naitwaje CAG mstaafu huwa nakerwa sana na kauli hii,” amesema na kuongeza.

“Kuna umuhimu mkubwa sana wa kupata katiba mpya lakini pia hata hii tuliyonayo ya mwaka 1977 bado baadhi ya watawala hawaifuati kwa sababu wanaona wananchi hatuisimamii vizuri kutokana na kutishwa, Jenerali Ulimwengu ni hazina ya taifa nampongeza sana kupitia makala zake alizoziandika tangu mwaka 1996  kama kuna jambo la kukosoa anakosoa anasimamia anachoamini.

“Wapo baadhi ya watu wamesoma lakini ni mazuzu hawatumii taaluma walizonazo  wanalinda maslah yao binafsi kwa kuwa wanatumia V8 na nyumba ya serikali anaogopa akitumia taaluma yake kusimamia ukweli akifukuzwa kazi atakosa  hivyo vitu wakati anayetoa riziki ni Mungu mimi nilisimamia ukweli na taaluma yangu ingawa sipo kwenye nafasi hiyo lakini bado napata riziki, ukweli ni kwamba mtu ambaye hana msimamo ni zuzu,” amesema Profesa Asad.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga,  ambaye aliwakilishwa na Mratibu wake William Mtwazi, amesema ili kujenga Tanzania ambayo kila mwananchi anaihitaji lazima kuwe na mifumo iliyoimara na thabiti  ya kiutawala inayowajibika kwa wananchi wenyewe.

“Huwezi kuzungumzia mfumo imara wa kiutawala bila kuzungumzia katiba ya nchi, ukisoma ibara ya nane ya katiba yetu utakubaliana na mimi kwamba  wananchi ndiyo wenye mamlaka dhidi ya serikali lakini wakati mwingine inaonekana ndivyo sivyo, wananchi tunamamlaka yaliyoandikwa kwenye katiba lakini inapokuja kwenye utekelezaji tunakuwa mashahidi kwenye sheria ambazo zimetungwa miaka michache iliyopita ambazo pamoja na mambo mengine zimelenga kupokonya uhuru wa wananchi katika kuamua au kutekeleza majukumu yao yanayolenga kujenga nchi au kuwajibisha mamlaka,”amesema.

Amefafanua kwamba  mdahalo huo  ambao umewakutanisha washiriki kutoka mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Iringa na Morogoro  ni muhimu kwa sababu unatoa fursa ya kujadiliana,  kushauriana na kuibua hoja ambazo zikijadiliwa zitasaidia kufikia maamuzi  yenye tija kwa taifa.

Naye Jenerali Ulimwengu, amesema kuna uhitaji  wa katiba mpya itakayoendana na falsafaya taifa” Tanzania ni nchi pekee duniani ninayoijua ambayo imesema itakuwa na utawala wa kidemokrasia na itakuwa na wabunge wanaochaguliwa na wananchi lakini  unaambiwa ukitaka kugombea nafasi yoyote lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa.

“Kama si mwanachama wa chama cha siasa inamaana wewe ni nusu raia au robo raia huna uraia kamili mpaka ujibanze kwenye chama cha siasa  suala hili tumelizungumza tangu mwaka 1992 hadi leo, hii inatoa tafsiri kwamba nguvu ya uhafidhina  yaani nguvu ya kuturudisha nyuma ni kubwa zaidi kuliko nguvu ya kutupeleka mbele  inayotambua umuhimu wa wananchi mmoja mmoja au katika makundi yao ambayo sio lazima yawe ya chama cha siasa  inaweza kuwa jamii,” amesema Ulimwengu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles