VALENCIA, HISPANIA
KOCHA wa klabu ya Valencia, Cesare Prandelli, amejiuzulu kuifundisha klabu hiyo huku akiwa amepata ushindi wa mchezo mmoja tangu ajiunge na klabu hiyo Septemba, mwaka jana.
Kocha huyo ameondoka huku akiiacha klabu ikiwa katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Hispania, baada ya klabu hiyo kucheza michezo 15 na kufanikiwa kupata alama 12.
Inadaiwa kwamba, kocha huyo ameamua kuondoka ndani ya klabu hiyo kutokana na kuwa na migogoro na baadhi ya wachezaji nyota wa timu hiyo, kama vile Daniel Parejo.
Kocha huyo alitangaza kujiuzulu Desemba 30, ambapo alituma taarifa yake kwa bodi ya klabu hiyo pamoja na chama cha soka nchini Hispania, lakini klabu hiyo kwa sasa imepanga kutaka kuzungumza na kocha huyo kutokana na maamuzi ya kuvunja mkataba wake.
Inasemekana kwamba, kocha huyo alituma maombi kwa uongozi wa klabu hiyo kuwachukulia hatua wachezaji wake ambao wamekuwa wakionesha utovu wa nidhamu katika chumba cha kubadilishia nguo, lakini hadi anatangaza kujiuzulu hakuna hatua yoyote ambayo ilichukuliwa.
Prandelli, mwenye umri wa miaka 59, amekuwa kocha wa nne kwa mwaka wa 2016 kuifundisha klabu hiyo, baada ya kuondoka Gary Neville nafasi yake ilichukuliwa na Pako Ayestaran, kabla ya Salvador ‘Voro’ Gonzalez kuchukua nafasi ya Pako, na nafasi ya Pako kuchukuliwa na Prandelli.
Klabu hiyo ya Valencia inatarajia kushuka dimbani kesho kutwa dhidi ya Celta Vigo kwenye michuano ya Copa del Rey, huku Valencia wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani.
Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo umedai kuwa, hauna wasiwasi na timu yao kwa kuwa wanaamini wanaweza kupata kocha ambaye ataisaidia timu hiyo kuweza kufanya vizuri katika michuano mbalimbali msimu huu.
“Huu ni wakati mgumu kwa timu, hasa ikiwa inafanya vibaya halafu kocha anatangaza kujiuzulu, kuna uwezekano mkubwa tangu kujiunga kwa kocha huyo wachezaji tayari waliweza kufuata mifumo mipya, lakini ujio wa kocha mpya utawafanya wachezaji waanze kubadili mfumo”, Waliandika Valencia.