NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM
SERIKALI imepiga marufuku uingizaji na usambazji wa mifuko ya plastiki huku wanaotengeza kileo maarufu kwa jina la ‘viroba’ nao wakikumbwa na zahama hiyo.
Imesema kwa sasa inaendelea na mchakato wa kutafuta vifungashio mbadala badala ya kutumia mifuko hiyo ambayo imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira nchini.
Wamiliki wa viwanda wanaotengeneza kileo aina ya viroba kwa kutumia paketi ya plastiki kama vifungashio wametakiwa kutafuta vifungashio mbadala kuliko wanavyotumia sasa kwenye kileo hicho.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba (Muungano na Mazingira), alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema kuanzia Januari mwaka 2017, hakutakuwa na uingizaji, usambazaji na utengenezaji wa mifuko ya plastiki nchini.
Waziri Makamba alisema hatua hiyo haitawahusu watengenezaji wa mifuko hiyo wanaosafirisha nje ya nchi bali na watengenezaji na wasambaji wa ndani pekee ndiyo watawagusa.
Alisema mifuko ya plastiki imekuwa ni changamoto kubwa ya mazingira kutokana na kutolewa bure hali inayosababisha kuzagaa ovyo mitaani.
“Nia ya Serikali ni kuweka zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki ndani ya sheria, na hii pia inahusu matumizi ya mifuko ya plastiki kufungashia pombe, maarufu kwa jina la viroba.
“Natoa wito kwa watengenezaji, wasambaji na waagizaji wa mifuko ya plastiki waanze kujiandaa sasa kwa zuio hili,” alisema Makamba
Alisema asilimia kubwa uchafu kwenye vyanzo vya maji hasa mito, maziwa na fukwe za bahari inatokana na mifuko ya plastiki.
Makamba alisema ofisi yake inakamilisha majadiliano na baadaye itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku moja kwa moja matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
“Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko ya plastiki kujiandaa kuacha shughuli hizo na itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikaji wa vifungio mbadala,” alisema Makamba.
Alisema kwa sasa wizara yake imetuma ujumbe wa watu watano kwenda Rwanda ikiwa ni moja kati ya nchi zilizoendelea duniani kwa kutotumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kulitekeleza.
Akizungumzia hatari ya nchi kugeuka jangwa, alisema hivi sasa imebainika asilimia 61 ipo hatarini kwa mwelekeo mbaya wa mazingira kwa miaka 15 ijayo.
Makamba alisema kila mwaka nchi inapoteza ekari milioni moja za misitu kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira hali inayosababisha kuvamiwa kwa vyanzo vingi vya maji na kuharibiwa.
Alisema uharibifu mkubwa wa mazingira umesababisha kuongezeka ukame kwenye maeneo mengi, rutuba ya ardhi kupungua, maporomoko ya ardhi kwenye maeneo ya milima na mafuriko yanayosomba miundombinu na kuharibu mali na maisha ya watu.
Alisema kila mvua inapopungua kwa asilimia 10 pato la taifa linalotokana na kilimo hupungua kwa asilimia mbili, kila joto linapoongezeka kwa nyuzi mbili za sentigredi mavuno ya mahindi hupungua kwa asilimia 13 na mavuno ya mpunga hupungua kwa asilimia17.
“Uharibifu wa mazingira unaathiri sekta zote nyeti za uchumi na maisha ya watanzania sekta ambazo zimeathiri zaidi kilimo, ufugaji , uvuvi, utalii, nishati, huduma ya maji na sekta ya afya,” alisema Makamba.