31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

POLISI YAONYA WIZI MITANDAONI

ACP-Advera-Bulimba

Na EVANS MAGEGE

JESHI la Polisi limewataka wananchi kuwa makini na biashara zinazofanywa kwa njia ya mitandao kwa sababu kuna ongezeko kubwa la watu wanaoibiwa au kutapeliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Advera Bulimba, alisema taarifa za matukio ya uhalifu wa biashara za mtandao zimeongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni.

Kutokana na ongezeko la matukio hayo, alisema uchunguzi uliofanywa na polisi umebaini kuwa watu wengi waliojikuta katika kadhia ya kutapeliwa au kuibiwa kupitia aina hiyo ya biashara wanatokana na kuwa na tamaa za mafanikio ya haraka au kutokuwa na uelewa wa biashara hiyo.

“Jeshi la Polisi linawakumbusha wananchi kuwa makini pindi wanapofanya biashara kwa njia ya mitandao kwa sababu wananchi wengi wamekuwa wakiibiwa kwa kutokuchukua tahadhari za kutosha kabla ya kutuma fedha.

“Wengi wanajikuta wakitumbukia katika kadhia hiyo ya kutapeliwa kutokana na kuwa na tamaa za mafanikio ya haraka na wengine kutokuwa na uelewa wa biashara za kimtandao,” alisema Advera.

Mbali na uhalifu huo, pia alisema matukio ya wananchi kuvamiwa na majambazi na kuporwa fedha nyingi wakati wanapozisafirisha kutoka eneo moja kwenda jingine yametokana na wahusika kutokuwa na usiri.

Advera alisema uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo umebaini kuwa matukio hayo yamekuwa yakisababishwa na wafanyabiashara wenyewe au watendaji wa ofisi za uhasibu ambao wamekuwa na tabia ya kutoa taarifa kwa watu wanaowazunguka kwamba wanapeleka fedha benki.

“Katika siku za hivi karibuni kumetokea matukio mbalimbali ya wananchi hususani wafanyabiashara kuvamiwa na majambazi na kuibiwa kiasi kikubwa cha fedha wakati wanaposafirisha fedha hizo kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Unakuta mfanyabiashara au mhasibu anamtaarifu mwenzake au ofisi nzima inajua kwamba siku fulani fedha zinapelekwa benki na inakuwa hivyo. Kwa msingi huo taarifa lazima ziwafikie wahalifu ambao hujipanga mapema na kufanya uhalifu,” alisema.

Pia aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaomba ulinzi wa polisi au kampuni binafsi za ulinzi zinazoshughulikia usafirishaji wa fedha.

“Tunawataka wasafirishaji wa fedha kuwa na usiri katika michakato yote inayohusiana na usafirishaji wa fedha ili kuweza kupunguza matukio hayo, wafanyabiashara nao wanatakiwa kuepuka kubeba kiasi kikubwa cha fedha na badala yake watumie miamala ya kibenki ili kupunguza matukio hayo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles