FRANCIS GODWIN -IRINGA
KUTOKANA na Jeshi la Polisi mkoani Iringa kumshikilia mwalimu wa masomo ya ziada, Anord Mlay kwa tuhuma za kulawiti watoto zaidi ya 24, jeshi hilo limewataka wazazi na walezi kuanza kuwakagua sehemu zao za siri watoto pasipo kuwaonea aibu ili kujua kama wamefanyiwa vitendo vibaya.
Limesema watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa ulawiti na ubakaji hukaa kimya bila kutoa taarifa kwa wazazi wao.
Akizungumza wakati wa mdahalo wa amani, uzalendo na ushirikishwaji wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika masuala mbalimbali ya maendeleo jana, ulioandaliwa na Mwamvuli wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Iringa (ICISO) kwa kushirikiana na Ushirika Tanzania, Ofisa wa Polisi Ushirikishwaji Jamii, Vicent Msami alisema tukio la mwalimu kulawiti watoto zaidi ya 24, ni la kutisha na linawapa somo wazazi kuanza ukaguzi wa watoto wao.
Msami alisema mtuhumiwa anaonyesha alianza kufanya vitendo hivyo kati ya mwaka 2015 na 2019.
Alisema idadi hii ni kubwa na kuna uwezekano ikaongezeka endapo wazazi watajitokeza.
“Mtuhumiwa alikuwa anatumia mbinu ya kuwawekea watoto picha za ngono zinazofundisha namna ya watu kufanya mapenzi, baada ya watoto kuangalia anawalazimisha kufanya nao mapenzi mmoja baada ya mwingine,” alisema Msami.
Alisema kumchunguza mtoto kama yupo vizuri kiafya ni jukumu muhimu na kuendelea kumwonea aibu ni mwanzo wa kumwathiri mtoto.
Alitaka jamii kujenga utamaduni wa kuongea na watoto wao mara kwa mara ili kujua kama wameanza kuchezewa na watu wabaya.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ameunda kamati ya watu 10 kufuatilia na kubaini watoto ambao wamefanyiwa ukatili.
Baadhi ya wazazi wa watoto, wanadai mwalimu huyo pia alikuwa anatumia mbinu ya kuchezesha michezo ya watoto kupitia kompyuta (game) kuwarubuni wengi zaidi kufika eneo hilo.