JENGO la Kituo cha Polisi Wilaya ya Longido mkoani Arusha halijaanza kutumika kutokana na ukosefu wa mabati, misumari na mbao za kumalizia ujenzi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, wakati akizindua Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Pori, Tengeru kilichogharimu Sh milioni 117.6.
Alisema kuchelewa kwa ujenzi huo kumemlazimu Mkuu wa Polisi wa Longido, Mkuu wa Upelelezi na Mkuu wa Kituo kufanya kazi katika chumba kimoja.
“Kukosekana kwa jengo la kutosha kumeendelea kuathiri ufanisi wa kazi. Licha ya ujenzi wa jengo la kituo hicho kukwama lakini uko mbioni kukamilika.
“Mabati, misumari na mbao imekwamisha kukamilika ili kituo kianze kutumika, tunakuomba mkuu wa mkoa kusaidia juhudi za kukamilisha ujenzi huo,” alisema Sabas aliyehamishiwa Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.
Alisema katika maeneo mengi ya mkoa huo yameendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama kutokana na kutokuwapo kwa vituo vya polisi vinavyotosheleza mahitaji.
Akielezea kuhusu Wilaya ya Karatu, alisema polisi wilayani humo inakabiliwa na tatizo la jengo la wilaya huku Arumeru na maeneo mengine mkoani humo yakiwa na upungufu wa vituo vya polisi.
Alisema katika miji midogo inayoendelea kupanuka kila mwaka nako kumeendelea kuwa na changamoto kwa vituo vilivyopo vinavyohitaji kupanuliwa ili viendane na mahitaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, alisema kwa kushirikiana na wadau itaendeleza juhudi za kuboresha vituo hivyo katika maeneo mbalimbali.
“Tayari nimekutana na wamiliki wa mashamba makubwa wilayani Karatu, wamekubali kuchangia ujenzi wa kituo cha polisi wilayani humo ambao majengo yake yamechakaa.
“Pia tutaendelea kuhamasisha wadau wengine wilayani Longido ili tuweze
kukamilisha kituo cha polisi,” alisema Ntibenda.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliwataka polisi kuacha kuwabambikizia wananchi kesi badala yake watumike katika kutoa huduma bora.