26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI YAIPIGA MKWARA MZITO TFF

Na JESSCA NANGAWE-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi limetoa onyo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhakikisha halizidishi idadi ya mashabiki watakaoingia kwenye mchezo kati ya Azam FC dhidi ya timu ya Simba, utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya Polisi imetokana na TFF kupeleka mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Azam FC dhidi ya Simba katika uwanja huo, uliopo Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, uliojengwa mwaka 2010 na unachukua watazamaji 5,000.

Azam na Simba zitakutana katika uwanja huo kutokana na TFF kusisitiza kuwa, michezo yote ya Simba na Yanga zitakapokuta na Azam zitachezwa katika uwanja huo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, alisema wao kama sehemu ya kuimarisha ulinzi watafanya kazi yao ipasavyo na wamejiandaa kuhakikisha ulinzi unaimarishwa ndani na nje ya uwanja, ili mchezo uwe wa amani na furaha.

Alisema kuwa, Polisi watafika mapema katika mchezo huo, ila ameionya TFF wahakikishe wanauza tiketi zinazoendana na uwezo wa uwanja huo na si kuzidisha idadi ya watazamaji.

“Sisi tutatimiza majukumu yetu katika kuhakikisha amani inakuwapo, suala la udogo wa uwanja si kazi yetu, kikubwa TFF na wahusika wote wahakikishe wanatoa tiketi ambazo hazizidi uwezo wa idadi ya mashabiki wanaotakiwa kwenye uwanja huo,” alisema Mwakalukwa.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, amesema wameamua kupeleka mchezo huo katika uwanja huo ili kuwapa heshima, kutokana na uwekezaji walioufanya pamoja na kutoa motisha kwa klabu nyingine kuboresha viwanja vyao.

“Kila siku tukisema uwanja ni mdogo tutaendelea kuwa na mawazo mgando, hii pia itakuwa fursa kwa Azam na tunaamini msimu ujao wataboresha uwanja wao na kuongeza ukubwa zaidi ya huu wa sasa,” alisema Lucas.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, alisema wamejipanga kuhakikisha mchezo huo unachezwa katika mazingira ya amani na watahakikisha wanasimamia suala zima la uuzaji wa tiketi na kudhibiti idadi ya mashabiki wanaotakiwa kwenye uwanja huo.

 

Lakini jambo hili la kutumia Uwanja wa Azam Complex si jambo geni katika soka, kwani hata kwenye Ligi Kuu ya England, Uwanja wa Vitality unaomilikiwa na Bournemouth, ndio uwanja mdogo kuliko vyote kwa timu zote za ligi hiyo, ukiwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 11,464, lakini timu zote zinakwenda kucheza mechi zao za ugenini dhidi ya wenyeji hao.

Hata Manchester United, yenye uwanja mkubwa wa Old Trafford, unaochukua watazamaji 75,653, nayo hulazimika kuifuata Bournemouth na kucheza katika uwanja huo mdogo, hii yote ni kufuata sheria zilizowekwa kiuweledi na FA, ili kuipa haki timu hiyo pamoja na mashabiki wake kuipa sapoti timu yao.

VIWANJA VYA LIGI KUU BARA

Uwanja wa Taifa

Ndio uwanja mkubwa kuliko vyote nchini, upo Dar es Salaam, una uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000.

Uwanja huu unamilikiwa na Serikali ya Tanzania, ulijengwa kwa ushirikiano na Serikali ya China mwaka 2007.

Uwanja wa Kirumba

Uwanja huu upo jijini Mwanza, unamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ulijengwa mwaka 1980 na una uwezo wa kuchukua watazamaji 45,000.
Kirumba ni uwanja wa pili kwa ukubwa Tanzania Bara.

 

Uwanja wa Uhuru

Uwanja wa Uhuru upo la Dar es Salaam, unamilikiwa na serikali, ulijengwa mwaka 1961 kwa madhumuni ya sherehe za uhuru wa Tanganyika na unachukua watazamaji 10,000 na ulipofanyiwa ukarabati wa kwanza uliongeza idadi ya watu na kufikia 15,000 na sasa una uwezo wa kuchukua watazamaji zaidi ya 30,000.

Uwanja wa Jamhuri 

Uwanja wa Jamhuri, Morogoro unamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM),  ulijengwa mwaka 1978, una uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000.

Uwanja wa Sokoine

Uwanja wa Sokoine, Mbeya, ulijengwa mwaka 1977, una uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000 na unamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uwanja wa Majimaji

Uwanja wa Majimaji upo Songea, Mkoa wa Ruvuma, unamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), una uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000 na ulijengwa mwaka 1979.

Uwanja wa Kambarage

Uwanja wa Kambarage upo Shinyanga, unamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ulijengwa mwaka 1983, una uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000.

Uwanja wa Kaitaba

Uwanja wa Kaitaba upo katika Mkoa wa Kagera, ni mali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ulijengwa mwaka 1976 na unachukua watazamaji 25,000.

Uwanja wa Azam

Uwanja wa Azam unamilikiwa na klabu ya Azam ya Dar es Salaam, upo Chamazi, nje kidogo ya jiji. Uwanja huu ulijengwa mwaka 2010, unachukua watazamaji 5,000.

Uwanja wa Nangwanda Sijaona

Uwanja wa Nangwanda Sijaona upo Mkoa wa Mtwara, ulijengwa mwaka 1992 na Halmashari ya Mji wa Mtwara, unachukua watazamaji 10,000.

Uwanja wa Manungu

Uwanja wa Manungu upo Turiani, Morogoro, ulijengwa mwaka 1999 na kampuni ya Mtibwa Sugar, unachukua watazamaji 10,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles