27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi yafukua kaburi la mtoto albino

Jumanne Muliro
Jumanne Muliro

Na SAM BAHARI-SHINYANGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limelazimika kufukua kaburi la mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Michael Juma (2), aliyefariki na kuzikwa Agosti 14, mwaka huu kutokana na kudaiwa kukatwa viungo kabla ya kuzikwa.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Jumanne Muliro, alisema uamuzi wa kufukuliwa kwa kaburi hilo umetokana na kuenea kwa taarifa zilizotolewa na baadhi ya watu ambao hawajafahamika wakieleza kuwa kabla ya kuzikwa alikatwa baadhi ya viungo vyake kwa ajili ya kuuzwa.

Alisema hata taarifa hizo zilipotolewa na baadhi ya mashirika ya kimataifa waliingia shaka ndipo walipoamua kuhakiki iwapo marehemu huyo alikatwa baadhi ya viungo vyake kabla ya kuzikwa.

“Kaburi la mtoto huyo lilifukuliwa Agosti 18, mwaka huu, saa 11 jioni katika Kijiji cha Bunambiyu Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kukuta mwili wake uko salama na hakuna kiungo chochote kilichopungua,” alisema.

Muliro alisema kabla ya kifo chake, baba yake mzazi, Juma Masoud, alisema mwanaye alikuwa akisumbuliwa na malaria kwa kipindi cha wiki moja mfululizo na kutibiwa katika Kituo cha Afya cha Bunambiyu na ilipofika Agosti 13, mwaka huu alizidiwa na saa tatu usiku alifariki dunia.

“Kutokana na kufariki, ndugu, jamaa na marafiki walikusanyika na taratibu zote zilifuatwa hivyo kuzikwa Agosti 14, mwaka huu nyumbani kwa Juma Masoud kwa mila na desturi za ukoo wake lakini yalipozuka maneno hayo tukalazimika kuufukua mwili wake,” alisema Muliro.

Naye Mganga wa Kituo cha Afya cha Bunambiyu, Dk. Hellena Kaunda, alisema baada ya kufukuliwa na kuufanyia uchunguzi mwili huo waliukuta uko salama na hakuna kiungo kilichopungua na ukazikwa upya huku akieleza kuwa uchunguzi umefanyika mbele ya wazazi wote wa marehemu na viongozi wa chama wa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Katibu wa watu wenye ualbino Mkoa wa Shinyanga, Lazaro Anael, alisema Agosti 14, mwaka huu yeye na baadhi ya wenzake walihudhuria mazishi ya mtoto huyo na walihakikisha amezikwa bila dosari yoyote lakini walishangazwa na taarifa hizo.

“Tulikuwa wengi katika mazishi hayo, wengine walikuwako wageni wa kitaifa na wote tulijiridhisha kuwa mazishi yamekwenda vizuri bila ya kuingia dosari na ndivyo ilivyokuwa,” alisema Anael.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles