21.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 5, 2022

Polisi yaeleza sababu za kumwita Mbowe

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe jana aliitwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na kisha kuachiwa.

Hatua ya kuitwa kwa Mbowe ilikuja saa chache kabla ya kufanya mkutano mubashara kupitia mitandao ya kijamii ya Chadema kuwasilisha ujumbe kwa Watanzania.

Taarifa kutoka ndani ya Chadema ilieleza kwamba Mbowe akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam, alifuatwa na maofisa wa Jeshi la Polisi, lakini wasaidizi wake waligoma kufungua mlango.

Hata hivyo, saa chache kabla ya kuanza kwa mkutano wake, alipokea wito wa polisi na kutakiwa kwenda kuripoti ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni katika Kituo cha Oysterbay.

Mbowe aliitikia wito huo na kwenda polisi huku akiwa na jopo la wanasheria wake.

KAULI YA POLISI

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mussa Taibu, alisema kuwa alimwita Mbowe ili kufahamiana.

 “Ni kweli nilimwita tufahamiane kwa sababu yeye ofisi yake ya Chadema iko maeneo haya haya ya Kinondoni, hivyo baada ya kufahamiana yeye ameendelea na ratiba zake,” alisema Kamanda Taibu.

Jana, muda mfupi baada ya Mbowe kutaka kufanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alitoa taarifa kupitia mitandao ya kijamii akisema mkutano huo hautafanyika tena.

“Mkutano wa Mwenyekiti Mbowe uliokuwa ufanyike mubashara kuzungumza na umma, hautafanyika kama ilivyopangwa baada ya Jeshi la Polisi kumhitaji akaripoti ofisi ya RCO Kinondoni, Kituo cha Oysterbay,” ilisema taarifa hiyo ya Makene.

Awali gazeti hili lilipomtafuta Makene kutaka kujua kuhusu kuitwa kwa Mbowe, alisema polisi hawakusema sababu ya kumwita mwenyekiti huyo.

“Kweli alikwenda polisi kitambo, tangu muda ule wa saa tano na polisi hawakusema sababu, nadhani mkiwauliza kwa sasa wanao wajibu wa kusema hilo,” alisema Makene.

MAAMUZI YA CHADEMA

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa wiki za hivi karibuni aliendesha kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kwa njia ya mtandao ambacho kiliazimia kuwavua uanachama wabunge wake wanne.

Wabunge waliofutwa uanachama ni pamoja na Joseph Selasini (Rombo), Antony Komu (Moshi Vijijini) ambao wote kwa nyakati tofauti walitangaza kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi mara baada ya Bunge kumaliza muda wake.

Wengine ni Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) na David Silinde (Momba).

Mbali na wabunge hao, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya chama na kutakiwa kujieleza kwanini asichukuliwe hatua.

Uamuzi huo umefikiwa kutokana na wabunge hao kukiuka maelekezo ya chama ya kuwataka wabunge wote wa chama hicho

wasishiriki vikao vya Bunge vinavyoendelea Dodoma na kukaa karantini kwa siku 14.

Wabunge wengine ambao wanaendelea kuhudhuria vikao vya Bunge na kutakiwa kujieleza kwa kukiuka makubaliano hayo ni Suzan Masele, Joyce Sokombi, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Sware Semesi, Jafari Michael, Peter Lijualikali, Willy Kambalo, Rose Kamili, Sabrina Sungura na Anne Gideria.

Siku 14 za wabunge hao kujiweka karantini zilikamilika juzi.

SPIKA AWAZUIA

Hata hivyo juzi Spika Bunge, Job Ndugai aliwazuia wabunge 15 wa Chadema kuhudhuria bungeni, iwapo hawatakamilisha masharti mawili muhimu.

Wabunge hao watatakiwa kutimiza masharti hayo kwa kuwa hawajulikani waliko na wamekuwa wakihesabiwa kama watoro tangu walipoacha kuingia bungeni Mei 1.

 “Ofisi ya Bunge inatoa taarifa kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekuwa watoro kwa kutohudhuria vikao vya Bunge bila ruhusa ya Spika kwa muda wa wiki mbili kinyume na masharti ya Kanuni ya 146 inayosisitiza wajibu wa kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Aidha, tunapenda ifahamike kwamba wabunge hao walisusia vikao vya Bunge huku wakiwa wamelipwa posho ya kujikimu ya kuanzia Mei 1-17, 2020.

“Kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 5 ya Kanuni za Bunge, Spika alitoa masharti mawili kwa wabunge hao,” ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa sharti la kwanza ni kuwataka wabunge hao kurejea bungeni au kurudisha fedha walizolipwa mara moja na sharti la pili ni kwa kuwa haijulikani wabunge hao walipo, watalazimika kuwasilisha ushahidi kwamba wamepimwa na hawana maambukizi ya virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kuingia bungeni

Iliwataja wabunge hao kuwa ni Freeman Mbowe, Ester Bulaya, Halima Mdee, John Heche, Joseph Mbilinyi, Peter Msigwa, Rhoda Kunchela, Pascal Haonga, Catherine Rage, Devotha Minja, Joyce Mukya, Aida Khenan, Upendo Peneza, Grace Kiwelu na Joseph Haule.

“Hivyo basi, kwa taarifa hii, na kwa mujibu we Kanuni ya 144 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayohusu usalama katika maeneo ya Bunge, Spika ameagiza Kitengo cha Usalama cha Bunge kutowaruhusu wabunge waliotajwa hapo juu kuingia katika maeneo ya Bunge kuanzia leo (juzi) Jumatano Mei 13, 2020 mpaka watakapotimiza masharti tajwa hapo juu,” ilieleza taarifa hiyo ya Bunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,680FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles