26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

POLISI YAELEZA JINSI MTEKAJI MWANAFUNZI ALIVYOANGALIA FILAMU

Na BENJAMIN MASESE

-MWANZA

JESHI la Polisi mkoani Mwanza, limetoboa siri ya mtuhumiwa wa tukio la utekaji wa mwanafunzi wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Ilonganzila, Khailati Bashiri (8), Emmanuel Kirumbas (25) mkazi wa Malampaka mkoani Shinyanga.

Limesema mtekaji alifanya tukio hilo kama jaribio baada ya kutazama sinema mbalimbali za kuigiza kwenye runinga.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema baada ya mahojiano na mtuhumiwa huyo wa utekaji, wamebaini alitenda kosa hilo kama jaribio baada ya kuangalia picha mbalimbali za maigizo.

Msangi alisema bila mtuhumiwa kujua anatenda kosa kubwa, alimteka mwanafunzi huyo na kumpeleka kusikojulikana na kuamua kuwapigia simu wazazi wake akitaka watumiwe Sh milioni tatu ili aweze kumrejesha.

“Tumegundua mtuhumiwa wa utekaji alifanya kile kitendo kama jaribio baada ya kutazama picha za maigizo, hivyo aliona afanye kwa vitendo na alikwenda katika familia ambayo kwa namna moja au nyingine alikuwa anaijua, sasa matukio kama haya yamewahi kutokea katika mikoa kadhaa hapa nchini likiwamo Jiji la Arusha na Dar es Salaam.

“Sasa tutamchukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanaiga vitu vya namna hiyo, niwaombe wazazi wawe makini katika malezi ya watoto wake, huyu kijana wa utekaji ni ukosefu wa malezi  ndio maana anaanza kuwa na tabia ya namna hiyo kutaka fedha,” alisema Kamanda Msangi.

Agosti 21, mwaka huu, mtuhumiwa alimteka mwanafunzi huyo saa sita mchana baada ya kutoka shuleni na kutokomea kusikojulikana  ambapo wazazi na majirani  walimtafuta bila mafanikio na kuamua kutoa taarifa polisi.

Hata hivyo, wakati polisi wakiendelea na upelelezi nyumbani kwa mwanafunzi huyo na maeneo mengine ndani ya Mkoa wa Mwanza, mtekaji aliwapigia simu wazazi akiwataka  kumpatia Sh milioni tatu ili kumrejesha nyumbani.

Kabla ya mtekaji hajakamatwa, polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine watano ambao kwa namna moja au nyingine walishirikiana katika tukio hilo. Kamanda Msangi alisema tayari mwanafunzi huyo amekabidhiwa kwa wazazi wake na anaendelea na masomo yake kama  kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles