24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi yabariki maandamano kumpongeza JPM

ABRAHAM GWANDU –SIMANJIRO

JESHI la Polisi Mkoa wa Manyara, limesema maandamano ya wadau wa madini yanayotarajiwa kufanyika leo kwa nia ya kumpongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa sababu zozote zile yanaruhusiwa mradi tu wahusika wamepata kibali.

Maandamano hayo yanafanyika ikiwa ni takribani miaka mitatu sasa tangu Serikali ilipopiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano na hasa ile inayohusisha vyama vya siasa kwa lengo la kutoa fursa kwa wananchi kujielekeza katika kufanya kazi za maendeleo.

Wadau wa madini hususan wachimbaji wa tanzanite mkoani Manyara, wameandaa maandamano ya amani kumpongeza Rais Magufuli baada ya kukubali kutia sahihi muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha jambo ambalo litasaidia kufuta kodi zilizokuwa kero kiasi cha kulalamikiwa kwa muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Agustino Senga, alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuzuia maandamano kama hayo kufanyika mradi wahusika wapate kibali kutoka kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).

“Mtakumbuka hivi karibuni yalifanyika maandamano kama hayo ya wafugaji na wakulima kwa lengo linalofanana na hili la hawa wadau wa madini. Nayo ni kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwatetea hivyo hata hayo tunayaruhusu,” alisema.

Kwa mujibu wa waratibu ambao ni Chama cha Wachimbaji (Marema),  maandamano hayo ya kilomita tatu yataanzia lango la Magufuli mbele ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya tanzanite hadi kwenye viunga vya Mji mdogo wa Mirerani katika  Uwanja wa Barafu unaomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, taarifa ya Marema iliyotolewa na Shwaibu Mushi, ilieleza kuwa maandalizi ya maandamano hayo yatakayopokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, yamekamilika.

Alisema maandamano hayo yatahusisha wachimbaji wote wa madini katika Mkoa huo hususan kutoka wilaya zote za Simanjiro, Kiteto, Babati, Hanang’ na Mbulu.

“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kukubali ombi letu kiasi kwamba Serikali anayoiongoza ikapeleka muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha na bahati nzuri wabunge wakapitisha muswada huo na sasa yeye Rais atausaini.

“Ni jambo la kupongeza kwa sababu  sheria hiyo imerekebishwa siku chache baada ya mkutano wa kisekta wa Mheshimiwa Rais na wadau wa madini uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.”

Alisema kauli mbiu ya maandamano hayo ni ‘Rais wetu, madini yetu, uchumi wetu’ ambapo wadau mbalimbali wa madini wakiwemo wachimbaji, wamiliki wa migodi na wazamiaji (WanaApolo) watashiriki.

Wengine watakaoshiriki ni wanaonufaika na madini wakiwemo wafanyabiashara, madalali na wanunuzi wa madini mbalimbali.

Alisema wao kama wadau wa madini hawana cha kumpa Rais Magufuli hivyo wanatumia maandamano hayo kwa lengo la kumuunga mkono na kuonyesha kuwa wapo pamoja naye katika uongozi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles