23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Polisi wazungumzia anayedaiwa kuuawa kwa kunyweshwa sumu

Na ELIUD NGONDO

-MBEYA

 JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kumtafuta mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya Osward Malambo, mkazi wa Kijiji cha Ifumbo, Wilaya ya Chunya mkoani hapa, anayedaiwa kuuawa kwa kunyweshwa sumu na ndugu zake kisha kuporwa Sh milioni 55.

 Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Sebastian Mbuta, alisema hadi sasa jeshi hilo linaendelea kumtafuta mjomba wa marehemu, Peter Mpamba ambaye ni mmoja wa washiriki wa tukio hilo.

Alisema sambamba na kuendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo, jeshi hilo bado linaendelea kufuatilia majibu ya vipimo kutoka katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya kujua chanzo hasa cha kifo cha Malambo.

“Majibu hayo ya vipimo ni ya kitsalamu, kwa hiyo hayawezi kuwekwa hadharani tu, yatatusaidia katika upelelezi wetu wakati tukiendelea kuchunguza tukio hilo,” alisema Mbuta.

 Alisema mtuhumiwa huyo akikamatwa ataunganishwa na wenzake wawili waliokwishakamatwa ambao ni Raphael Walolile na Goliat Walolile.

Tukio hilo lilitokea Juni 2 ambapo inadaiwa Malambo kabla hajafariki dunia alitoa taarifa kwamba alinyweshwa sumu na watuhumiwa.

 MTANZANIA lilizungumza na ndugu wa marehemu baada ya mazishi, ambao waliliomba Jeshi la Polisi kuwasaidia kwa kuwa wanapata vitisho kutoka kwa marafiki wa watuhumiwa.

 Kaka wa marehemu, Selemani Malambo, alisema kitendo cha kuondokewa na ndugu yao kimekuwa ni pigo.

 Alisema kwa sasa wanalitegemea Jeshi la Polisi kuweza kuwasaka watuhumiwa wa tukio hilo la kinyama dhidi ya ndugu yao ili sheria iweze kufuatwa.

 “Hapa sisi tunalitazama Jeshi la Polisi juu ya tukio hili kwani limekuwa ni pigo kubwa ndani ya ukoo wetu na familia yetu, hasa ilipotokea ndugu zetu kuamua kutufanyia unyama huo ambao sio mzuri.

 “Watuhumiwa wawili waliokamatwa ni shemeji zetu na mmoja ambaye ametoroka ni mjomba yetu, ambao walikuwa na kesi mahakamani ambayo inaendelea mpaka sasa, ila ajabu ni kwamba wameamua kuua ndugu yao,” alisema.

 Naye mdogo wa marehemu, Erenest Malambo alisema familia yao inazidi kupata vitisho vya ujumbe wa maneno kwenye simu zao kutoka kwa marafiki wa watuhumiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles