25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi watoa onyo watakaojaribu kufanya fujo

CLARA MATIMO Na ASHA BANI, DAR ES SALAAM/ Mwanza

WAKATI wananchi wakirejea kwenye shughuli zao baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, polisi katika mikoa mbalimbali imeonya juu ya watu watakaojaribu kufanya fujo za aina yoyote kwa kisingizio cha uchaguzi huo.

Jijini Dar es Salaam, jeshi hilo limesema limebaini uwepo wa vikundi vya watu wanaofanya vikao vya siri ili kupanga njama za kuvuruga zoezi la kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazzaro Mambosasa, alisema wamebaini kuwepo wa vikundi vya watu wanaofanya vikao vya siri kupanga njama za kuvuruga kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo alisema wamejipangakila kona ya jiji hilo, kuhakikisha wanadhibiti vikundi hivyo ambavyo vimepanga kuingia barabarani kufanya maandamano.

Hayo aliyasema juzi wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikihitimisha  kutangaza matokeo ya kiti cha urais katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

“Kwa kufanya hivyo ni sawa na kuchezea demokrasia nchini ambayo kimsingi ni maamuzi ya wananchi, hivyo ni budi kwa wanasiasa mbalimbali kukubaliana na matokeo ya uchaguzi na kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka 2025,”alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa, jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha halitoi nafasi ya kufanyika kwa aina yoyote ya vurugu ama maandamano kufuatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu.

Aliongeza kwa kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, pindi watakapobaini uwepo wa vikundi vya namna hiyo ili vidhibitiwe mapema.

Alisema  wanaendelea kufuatilia taarifa hizo na uimarisha ulinzi na usalama katika kila pande za Jiji hilo kwani inaonekana kuwa vikundi hivyo vimeamua kufanya vurugu hizo jijini hapa.

Nako jijini Mwanza, jeshi la polisi limetoa onyo kwa watu wanaodaiwa kupanga njama za kufanya fujo au  vitendo vya kihalifu baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, alisema wamepata  taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna watu ambao wamepanga kufanya fujo katika maeneo mbalimbali  na hivi sasa  wanaendelea kufuatilia mienendo yao  watakapobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema jeshi hilo liliimarisha usalama kwa kiwango cha juu kwa vipindi vyote vya kampeni, kabla na baada ya kupiga kura  pamoja na kipindi hiki ambacho matokeo yanatangazwa hivyo hakuna matukio makubwa na ya ajabu yaliyotokea ya kuweza kuathiri mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28.

“Jeshi la polisi halitamvumilia mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kitakachojaribu kuandaa mipango au njama za kufanya vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani wenye nia hiyo nawatahadharisha mapema waachane na mpango huo kwa sababu hawatafanikiwa zaidi wataishia mikononi mwa vyombo vya dola.

“Tumejipanga kweli kweli kulinda amani ya wananchi wa Mkoa huu hivyo watambue kwamba hawatapata nafasi hata sekunde moja ya kufanya  vitendo vyovyote ambavyo ni kinyume na sheria za nchi yetu njama ovu zozote watakazozipanga zitatufikia nasi tutawathibiti mapema kabla hawajatekeleza uhalifu walioupanga.

“Natoa wito kwa wananchi wema waendelee kutuletea taarifa mbalimbali za wahalifu ili tuwakamate mapema kabla hawajatenda uhalifu pia tunawashauri  wananchi waendelee na shughuli zao za kawaida  wasiwe na hofu yoyote kuhusu usalama wao maana tumeimarisha ulinzi,”alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, watu wote waliojaribu  kupanga njama za fujo au kufanya vurugu kipindi cha uchaguzi mkuu  walikamatwa na kuhojiwa baadaye waliachiwa kwa dhamana, upelelezi unaendelea utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles