23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Polisi watano, mwanajeshi kizimbani kwa wizi wa mafuta

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

JAMHURI imewafikisha mahakamani askari polisi watano na mwanajeshi mmoja wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu, likiwamo la wizi wa mafuta ya ndege yenye thamani zaidi ya Sh milioni nne na kutakatisha fedha hizo.

Washtakiwa walifikishwa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomwa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Mwaikambo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Koplo Shwahiba (38), MT. 74164 SGT Ally Chibwana (47) wa JWTZ, PC Elidaima Paranjo (38), PC Simon (28), PC Dickson na PC Hamza.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali, Faraji Nguka akisaidiana na Saada Mohammed alidai washtakiwa wote hao wakiwa ni watumishi wa umma walikiuka maadili ya kazi zao kwa kupanga genge la uhalifu na kuiba lita 2,180 za mafuta ya ndege (Jet A-1/Ik) yenye thamani ya Sh  4,647,760.

Katika shtaka la pili, inadaiwa Julai 30, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, watuhumiwa hao waliiba lita 2,180 za mafuta ya ndege (Jet A-1/Ik) yenye thamani ya Sh 4,647,760 mali ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Katika shtaka la tatu imedaiwa siku na mahali hapo washtakiwa hao wote walifanya wizi wa mafuta hayo na kutakatisha kiasi hicho cha Sh milioni 4.6 wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi kinyume na sheria.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo husikilizwa Mahakama Kuu au pale DPP atakapotoa kibali cha mahakama hiyo kusikiliza.

Washtakiwa hao ambao wanatetewa na Wakili Hasaan Kiangio, wamerudishwa rumande hadi Septemba 24 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Wakili Kiangio aliomba tarehe ijayo awasilishe hoja kwamba shtaka la kutakatisha liliwekwa kwa lengo la kuwanyima dhamana washtakiwa, lakini mahakama ilikataa kusikiliza hoja hizo kwa sababu haina mamlaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles