Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, amesema vitendo vya mauaji ya albino vimeanza kushamiri tena katika baadhi ya maeneo nchini.
Amesema kutokana na hali hiyo, jeshi la polisi limewaomba wananchi, asasi za raia, viongozi wa dini na wanasiasa kushirikiana nao waweze kukamata mtandao wa watu wanaojihusisha na shughuli hizo na kuwachukulia hatua.
Alisema kuwa vitendo hivyo vinahusishwa moja kwa moja na imani za ushirikina hali inayosababisha baadhi ya albino kuuawa na wengine kukatwa viungo vya mwili wao.
“Vitendo hivi vimeanza kurudi tena nchini baada ya kudhibitiwa kipindi kilichopita. Hii inatokana na baadhi ya wananchi kuweka mbele imani za ushirikina na kuamua kuingia kwenye mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi,”alisema Mngulu.
Alisema jeshi la polisi linaendelea na operesheni ya kuwakamata watu wanaohusika na vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua za sheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Alisema kutokana na hali hiyo watu saba wamekamatwa katika tukio lililotokea Mei 12 mwaka huu mkoani Simiyu na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.
Alisema tukio la pili lilitokea Agosti 5 mwaka huu katika Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ambako mtu mmoja alikatwa mkono na hadi sasa watu watatu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Tukio la mwisho lilitokea Agosti 16 mwaka huu wilayani Igunga ambako mtu mmoja alikatwa mkono na watu wasiojulikana na mpaka sasa tunawashikilia watu watatu,”alisema Mngulu.
Kamanda amewaomba wananchi kupiga simu namba 0755,785,557 za makao makuu ya polisi kwa ushirikiano zaidi.