24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi waokota bastola ya Brazil mtaani

 ELIUD NGONDO -MBEYA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limeokota silaha aina ya bastola ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana nje ya ofisi za Serikali ya Mtaa wa Maendeleo katika Kata ya Iyela jijini Mbeya hali ambayo imeibua hofu ya usalama.

Akizungumza na wandishi wa habari ofsini kwake juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alisema katika tukio la kwanza maofisa wa Jeshi hilo waliiokota bastola hiyo aina ya Taurus ambayo imetengenezwa nchini Brazil.

Alisema bastola hiyo ina namba za usajili TGT.10582/PT 809 ambayo mmliliki wake hajafahamika na kwamba Jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini mmiliki wa slaha hiyo.

“Bastola hii iliokotwa Julai 25 mwaka huu, sasa unapokuta silaha kama hii katika mji huu ujuwe hata wahalifu wapo, hivyo tunaomba mtu yeyote ambaye anamfahamu mmiliki wa silaha hii atoe taarifa ili tuwakomeshe wahalifu hawa,” alisema Kamanda Matei.

Aidha Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia mzee mmoja aliyetajwa kwa jina la Amani Mpendule (68) mkazi wa Kata ya Lualaje wilayani Chunya kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya gobore iliyotengenezwa kienyeji bila kuwa na kibali.

Katika hilo Kamanda Matei alisema Mzee Mpendule alikamatwa na gobore hilo ambalo analimiliki bila kuwa na kibali akiwa anaendelea kulitumia kwenye uwindaji haramu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Alisema mzee huyo alikamatwa wakati wa msako wa pamoja kati ya maofisa wa Jeshi la Polisi na maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chunya.

Alisema mbali na mtuhumiwa huyo kukamatwa na bunduki hiyo pia alikutwa akiwa na vipande vya nondo na baruti ambavyo alikuwa anavitumia kuua wanyama kwenye hifadhi hiyo.

“Tunaendelea kumhoji mtuhumiwa na ushahidi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, hivyo natoa tahadhari kwa watu wote wanaomiliki silaha bila kuwa na vibali kuzisalimisha haraka Jeshi la Polisi,” alisema Kamanda Matei.

Alisisitiza kuwa Jeshi hilo litafanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha watu wote wanaomiliki silaha bila kuwa na vibali wanakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles