24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wamsaka mwanamke aliyepanga njama za ugaidi

Baadhi ya wafanyakazi wa Hoteli ya Dusit ya jijini Nairobi nchini Kenya ambao wamefariki katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa mwanzoni mwa wiki hii.

NAIROBI, KENYA

POLISI kitengo cha kupambana dhidi ya ugaidi nchini Kenya, wamethibitisha kuanza msako dhidi ya mtuhumiwa namba moja wa tukio la kigaidi lililofanyika Januari 15, mwaka huu katika Hoteli ya DusitD2 jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini humo, jana vimeripoti kuwa polisi wanamtafuta mwanamke ambaye anaaminika kupanga njama za kutekeleza shambulizi la kigaidi nchini humo, anayefahamika kwa jina la Violet Kemunto Omwonyo.

Msako huo umetokana na mwanamke huyo kuwa mke wa mtuhumiwa wa tukio hilo, Ali Salim Gichunge, ambaye anatajwa kulisaidia kwa kiasi kikubwa jeshi hilo kuwanasa watuhumiwa wengine 9 walioshiriki kutekeleza jinai hiyo.

Hadi sasa maswali yanayoulizwa ni mahali alipo, Violet Kemunto na kama kweli alihusika kupanga njama na kutekeleza shambulizi la kigaidi katika hoteli tajwa. Je, ni kweli yeye ndiye aliyeandaa mpango mzima wa shambulio hilo? Je, ni yeye aliyetoa fedha za kutekeleza tukio hilo? Je, ni kweli alifanikiwa kumshawishi mume wake, Ali Gichunge, kutekeleza shambulio hilo lililoua watu 21? Kwa namna gani mwanamke ambaye alionekana duni jijini Nairobi na ambaye kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vikieleza alikuwa rafiki mzuri na mpole akawa mtuhumiwa wa ugaidi?

WAPELELEZI

Maswali hayo ni miongoni mwa yanayotafutiwa majibu na maofisa usalama nchini Kenya ambao wanaendelea kumsaka mwanamke huyo. Juzi kikosi cha wapelelezi kilivamia nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke huyo na mumewe, Gichunge, kupata majibu ya maswali yao.

Ripoti zilizoibuliwa mwanzoni mwa wiki hii zilidai kuwa Jeshi la Polisi lilielekeza kumkamata mwanamke huyo, ambapo hakuwa miongoni mwa watuhumiwa watano waliofikishwa mahakamani wakihusishwa na kushiriki shambulizi la kigaidi.

Tangu Jumanne, Violet Kemunto, amekuwa mwanamke anayesakwa zaidi duniani pamoja na uchunguzi wa sakata hilo kufanyika kila sehemu ambazo alikuwa akitembelea, marafiki na ndugu zake wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Kenya, Marekani, Uturuki, Uganda na Somalia ambako anatajwa kuishi baada ya kutoweka kati ya mwaka 2016 na 2018.

Juzi, gazeti la Nation liliripoti kushuhudia askari takribani 30 wakiwa wamepiga kambi katika nyumba namba E7 iliyopo eneo la Guango katika Kaunti ya Kiambu, ambako Violet aliwahi kuishi hapo na mumewe.  

Idadi ya maofisa wa polisi na vifaa walivyobeba ambavyo ni mahususi kwa uchunguzi, walikuwa tayari kwa mapambano yoyote ambayo yangetokea.

Wakuu wa polisi katika kaunti mbalimbali wamepewa maagizo ya kuendesha msako mkali dhidi ya Violet.

VIOLET NI NANI?

Violet Kemunto, ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya uandishi wa habari na mahusiano ya umma katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST), mwaka 2015.

Violet aliwahi kufanya kazi kwenye kampuni ya simu jijini Nairobi. Kisha akapata mwanamume mwingine.

Rekodi katika taasisi hiyo zinaonyesha Violet amejikita kwenye uofisa habari. Kwa marafiki zake walitambua kuwa ameingia kwenye soko la ajira kutafuta kazi kwenye kampuni kubwa za habari.

Lakini kwake ilikuwa kazi ya muda mfupi tu. Alikuwa na mipango mingine na mipango hiyo ndiyo ilitimia Jumanne ya Januari 15 kwenye tukio la kigaidi la Kenya. Jeshi la Polisi linaamini kuwa mwanamke huyo alivuka mpaka kuelekea Somalia saa chache kabla ya shambulizi hilo kutekelezwa.

Mashushushu wamechunguza maisha yake na kubaini kuwa ni mfanyabiashara ya ugaidi. Rafiki yake Kemunto anasema binti huyo alikuwa mkimya na rafiki mzuri, ambaye wakati wote akiwa darasani au kokote alikuwa anajitanda nguo mwilini huku kichwani akivalia Hijab ambayo huvaliwa na wanawake wenye imani ya dini ya Kiislamu.

“Hakukuwa na kitu cha kutilia shaka kwake, isipokuwa unaweza kuhisi ni Mkristu kwa jina lake. Mara nyingi alikuwa mkimya sana na rafiki wa kila mtu aliyekuwa karibu yake. Aliongea pale tu zinapokuwa kazi za kwenye makundi ya majadiliano chuoni. Wala hakuwa mnywaji wa pombe au kuvuta sigara,” anasema rafiki yake, Masinde Muliro.

Katika Chuo cha MMUST, ushindani mkubwa wa kupata chumba kwenye hosteli umechochea watu kujenga nyumba kandokando ya chuo hicho na kujipatia fedha kutoka kwa wanafunzi. Violet, alipanga chumba kwenye hosteli binafsi kwa kipindi chote alichokuwa akiishi chuoni. Alifahamika kwa jina la Hadija, ambalo lilifupishwa kwa kuitwa “Didge” kwa wanafunzi wenzake.

Alikuwa na marafiki watatu wa karibu na wa nne alikuwa mwandani wake ambaye wanafunzi wenzao waliwaita “Gang of Four”, wakiwafananisha na kundi la wanasiasa machachari wa China, Jiang Qing, Zhang Chunqiao, Yao Wenyuan na Wang Hongwen, waliopambana na utawala wa Mao Zedong.

Mmoja wa marafiki zake wenye mawasiliano na ndugu zake Violet, walipopigiwa simu hawakuwa tayari kuzungumza lolote. Baadaye walizima kabisa simu zao.

Vile vile alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi mwenzake wa kiume ambaye alikuwa akisoma naye fani moja na walidumu hadi alipohitimu. Mara baada ya kuhitimu, Violet alivunja uhusiano huo.

Walikuwa karibu sana na walipanga kuoana, lakini mambo hayakwenda vizuri kama walivyopanga.

Violet alisoma sekondari ya wasichana ya Kiislamu kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu mwaka 2010. Mara baada ya kuhitimu mwaka 2015 alihamia Nairobi na kupanga chumba katika Kitongoji cha Ngumba, kilichoko barabara ya Thika Road. Alifanya kazi katika duka la simu kabla ya kuanza biashara ya kuingiza vifaa vya umeme, vito na simu nchini Kenya ambapo vingi vilitoka  Marekani.

MITANDAO YA KIJAMII

Taarifa zinazoonekana katika mtandao wa kijamii wa Facebook, Violet, amewahi kutembelea maeneo ya Kisii. Chochote kinachoendelea sasa ndugu na marafiki wanahitaji majibu.

Juni mwaka 2016, Violet, alisafiri hadi Kisii kumtembelea ndugu yake. Katika safari hiyo alikutana na marafiki na ndugu zake ambapo walipiga picha za pamoja na kuzirusha katika mtandao wa Facebook. Akiwa Kisii hakuwahi kuvaa baibui kama mwanamke wa imani ya Kiislamu. Katika kipindi hicho Violet alikuwa akitumia jina la Violet Omwoyo kwenye mtandao wa Facebook.

Oktoba mwaka 2016, alibadilisha jina lake na kutumia jingine la Didgesupuu Omwoyo. Marafiki zake wanasema jina la ‘Didge’ ni kifu cha jina lake la Kiislamu la Khadija, wakati ‘Supuu’ lina maana ya ‘mzuri’.

Baada ya hapo, Violet, alitoweka katika uso wa marafiki na ndugu zake. “Hatujui alikokwenda. Alitoweka na hakuwasiliana na yeyote,” alisema mmoja wa dada zake.

Kutoweka kwake kulianza kwa kubadilisha jina lake kwenye mtandao wa Facebook kutoka Didgesupuu Omwoyo hadi jina la Didgesupuu Faruq. Kisha akatoweka.

Mwaka 2018, alirejea na kutangaza kuoana na Ali Salim Gichunge, mtu ambaye majirani zake wanasema ni mmoja wa magaidi walionaswa kwenye kamera za hoteli ya Dusit siku ya shambulizi la kigaidi.

Kabla ya shambulio hilo, rafiki yake wa utotoni, Issa Mussa, aliliambia gazeti la Nation kuwa Violet aliishi na mumewe kwa mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa rafiki zake, aliwahi kutoa taarifa kupitia Facebook kuwa anauza samani zake zote za Muchatha kwa kuwa alikuwa anahamia makazi mapya huko Ruai.

Violet alizaliwa Ruai katika familia ya watoto sita, wanawake wakiwa wanne na wanaume wawili. Baba yake mwenye asili ya kabila la Kalenjin alifariki dunia miaka 14 iliyopita, wakati mama yake alikuwa mwenyeji wa Gusii. Kaka zake wanaishi Marekani.

Baada ya kifo cha baba yake, mama yao ambaye anamiliki duka hapo Ruai aliolewa na mwanamume mwingine.

SOMALIA

Mkuu wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Magharibi nchini Somalia, Rashid Yakub, amesema wanafanya uchunguzi dhidi ya madai hayo na shughuli nzima za mwanamke huyo, bila kutoa ufafanuzi wa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles