Na Amina Omari na Oscar Assenga, TANGA
KAIMU Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, amesema watu waliopambana na askari polisi na wale wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ni kikundi cha wahuni.
Harakati za mapambano baina ya polisi na wahalifu hao zilidumu kwa takribani saa 48, huku Mkuu wa Mkoa huo, Said Magalula akikiri kwamba wameshindwa kuwakamata watu hao.
Jana Ndaki aliwaambia waandishi wa habari kuwa, jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa kutokana na tukio la majambazi kushambiliana na askari polisi usiku wa kuamkia Jumamosi.
“Kuna watu kadhaa tumewakamata kuhusika na tukio hilo na upelelezi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wote waliohusika.
“Niwatoe hofu wananchi, tukio zima lilihusisha kikundi kidogo cha wahuni ambacho walikuwa wanajificha katika Mapango ya Kijiji cha Mleni kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuhalifu “alisema Ndaki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, alisema hali katika Mji wa Amboni ni salama na kuwa, waliookuwa wanapambana na polisi ni majambazi na si magaidi.
Magalula aliwaeleza waandishi wa habari jana, mapambano hayo yalilenga kuwapata wahalifu ambao walipora silaha za polisi mwishoni mwa wa Januari.
“Januari 26 askari wetu waliokuwa katika doria wawili waliporwa silaha hivyo harakati zilizokuwepo ili kuwa ni kuzipata silaha zilizoibwa”alisema Magalula.
Aliongeza kuwa mapambano yaliyofanyika ilikuwa ni pamoja na kuwakamata wahalifu waliohusika na uporaji huo.
Katika hatua nyingine, Magalula amethibitisha kifo cha askari polisi mmoja, Sajenti Said Kajembe, ambaye alijeruhiwa kutokana na tukio hilo.
“Askari wengine watano waliojeruhiwa wanaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali ya Bombo”alisema mkuu huyo wa mkoa.
Hata hivyo Magalula alikana vikosi vya jeshi kuendelea na kutupa mabomu kwenye maeneo waliyoyashuku kuwa na wahalifu.
“Licha ya mapambano hayo hatukuweza kuwakamata wahalifu wa silaha zilizoibwa, lakini msako bado unaendelea katika maeneo yote” alisema Magalula.
Jana hali ilionekana ya kawaida, tofauti na siku bili zilizopita kutokana na ulinzi kuimarishwa zaidi huku maeneo yanayozunguka vijiji hivyo yakiwa kama vile watu ambao wamefiwa kutokana na kuwa kimya.
MTANZANIA imebaini kuwa, pango hilo walilotumia wahalifu hao, lilikuwa na njia ya kuingilia na ya kutokea.
Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya njia zilizosababisha watu hao kutoroka kwa urahisi.
Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia maeneo mbalimbali ya mapango hayo, yakiwa na alama zilizodaiwa kuwa ni za risasi walizokuwa wakirusha askari waliokuwa wakiwashambulia watu hao.