Na Mwandishi Wetu-Igunga
JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, linawashikilia askari wake 6 kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya Sh milioni 8.
Habari kutoka vyanzo vya uhakika ndani ya jeshi hilo, viliiambia MTANZANIA jana kuwa askari hao wanashikiliwa kwa siku ya nne kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa, Ngaka Mataluma (95).
“Kila askari anahojiwa kuhusiana na tuhuma hizi, ni jambo zito ambalo limelichafua jeshi letu, haiwezekani askari aliyekula kiapo ndiye anakuwa mshawishi wa kupokea fedha haramu,” alisema mtoa taarifa wetu.
Askari wanaoshikiliwa ni Inspekta Frank Matiku, PC Raphael Maloji, D. Koplo Paul Bushishi, PC Lome Laizer, PC Lucas Nyoni na Koplo Charles.
Akithibitisha kushikiliwa kwa askari hao, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, alisema hadi jana jioni walikuwa wakiendelea kuhojiwa kwa tuhuma zinazowakabili.
“Polisi hawa wanaendelea kushikiliwa na Takukuru kwa mahojiano… nipo Nzega na mkuu wa mkoa wangu tuna kikao cha kazi, nikitoka tu nitakupa taarifa kamili.
“Nategemea nikimaliza kikao nikimbie Igunga, najua ni karibu mwendo wa saa nzima, itabidi uvumilie. Hawa askari wanashikiliwa siku ya nne leo (jana),” alisema Mwaipopo.
Alisema kutwa nzima jana, Takukuru walikuwa wanalifanyia kazi suala hilo pamoja na watumishi wengine wawili wa Serikali wanaotuhumiwa kwenye sakata hilo.
Viongozi hao wa Serikali ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isakamaliwa, Edward Kitenya na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zahanati, Maulid Hamisi.
Juzi Mwaipopo alikiri kuwapo tukio hilo na kusisitiza angelitolea ufafanuzi jana, lakini kutokana na kuwa na kikao na mkuu wa mkoa hakufanya hivyo.
Katika hali ya kushangaza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley alipoulizwa aliruka kimanga kuwa hana taarifa za tukio hilo.
“Sina taarifa za tukio hilo, umezipata wapi, hazina ukweli wowote, wanashikiliwa kwa nini? Wamekosa nini? Waulize Takukuru, sihusiki na masuala ya rushwa,” alisema.
Lakini baada ya Kamanda Nley kugoma kuzungumzia suala hilo, DC Mwaipopo ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, alikiri kushikiliwa kwa askari hao.
Juni 12, mwaka huu, askari hao wanadaiwa walikwenda kwa Mataluma na kuomba Sh milioni 20, lakini wakajadiliana hadi Sh milioni 8.
Juni 17, mwaka huu, Diwani wa Kata ya Isakamaliwa, Dotto Kwilasa aliitisha mkutano wa hadhara kusikiliza kilio cha wananchi, baada ya kusikia polisi wamefanya tukio hilo.
Katika mkutano huo, mtoto wa mzee huyo, Nkende Ngaka alisimulia tukio zima na kusema Juni 12, mwaka huu saa 2 asubuhi, askari sita wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1825, wakiwa na silaha za moto walifika Isakamaliwa, kisha wakaenda kwa baba yake.
“Walifika nyumbani, waliposhuka kwenye gari yao walinihoji kwanini sipokei wageni, baadae waliniuliza mimi ni mganga wa kienyeji.
“Niliwajibu mimi sijihusishi na suala la uganga wa kienyeji, baada ya kutoa kauli hii waliniambia wao wamepotea njia,” alisema Nkende.
Alisema baada ya kuhojiwa hapo, askari hao waliamua kuondoka, lakini muda mfupi wakarudi tena na kumwamuru awapeleke kwa baba yake.
“Tulipofika kwa baba, walimwomba atoe leseni ya uganga, aliwaambia hana wala shughuli za uganga hajawahi kufanya.
“Majibu haya hawakuridhika nayo, waliingia ndani na kuanza kupekua nyumba nzima, huku wakiwa hawana hati ya upekuzi, walipata rasta, kipande cha mifupa, kipisi cha msokoto wa bangi, ngozi ya kenge na kinyesi cha chatu na bunduki aina ya gobole.
“Baada ya kukamilisha upekuzi, waliomba wapewe kiasi kikubwa cha fedha ili wasimbebe baba yangu kwenda naye kituo cha polisi Igunga,” alieleza.
Alisema baada ya kuambiwa watoe fedha, walihoji kosa walilofanya kwa kuwa vitu walivyodai wamekuta ndani vilikuwa vingine havipo.
“Pamoja na kupinga kutoa fedha hizo, polisi walimbeba baba yangu hadi ofisi ya mtendaji kijiji.
“Wakiwa ofisini kwa mtendaji, askari hawa, mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji walitaka tutoe Sh milioni 15 au 12 ili wamwachie, huku wakitutisha kwa maneno mengi. Baada ya kugoma, wakashusha mpaka Sh milioni 10, tukagoma tena, kutokana na vitisho vikali tuliamua kuwapa Sh milioni 6, lakini wakaendelea kusisitiza kuwa wanataka Sh milioni 8.
Alidai kuwa baada ya kuambiwa hakuna hela wanayotaka, wakamlazimisha baba yake awapigie wafanyabiashara waje kununua ng’ombe.
Naye Mataluma, alidai baada ya kuona hali tete na kuhofia usalama wake, aliamua kuwapigia wafanyabiashara na wakaja kununua ng’ombe 13 kwa Sh milioni 8 ambazo askari hao walizichukua.
Alidai kuwa baada ya askari kupata fedha hizo, waliondoka na bunduki yake aina ya gobole ambayo anaimiliki kihalali.
“Walichukua bunduki yangu ambayo naimiliki kihalali siku zote, wameondoka nayo. Katika maisha yangu yote sijawahi kufanya vitendo vya uhalifu,” alidai.