Francis Godwin – Iringa
JESHI la polisi Mkoa wa Iringa limesema limemkamata Mhariri wa Uzalishaji Maudhui na Msimamizi Msaidizi wa Watetezi TV, Joseph Gandye, ili awaonyeshe askari waliohusika kusimamia watuhumiwa wa wizi kulawitiana wakati wakiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Mafinga.
Akizungumza na mwandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, alisema mwanahabari huyo alikamatwa jana jijini Dar es Salaam na kuwekwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Iringa.
“Tumemkamaa huyu mwandishi Joseph Gandye badala ya kujibizana kwenye mitandao tunataka aje huku Iringa ili akatuonyeshe na kuthibitisha habari alizoziandika na kuzisambaza mitandaoni kuwa kuna watuhumiwa walilazimishwa kuingiliana kinyume na maumbile wakiwa kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi.
“Hatuzuii taratibu nyingine za kwao ama ndugu kwa ajili ya dhamana na kuja na wakili wake kumsikiliza ila sisi tupo kwenye uchunguzi wetu kwa kumkamaa mwandishi aliyeandika ili ikibainika ukweli sheria ichukue hatua zake, “alisema Bwire.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa Agosti 14, Kamanda Bwire alisema mtuhumiwa Ambrose Malya (35) alidai kulazimishwa kuingiliana kinyume na maumbile akiwa mahabusu, suala alilolifikisha ofisini kwake na polisi ilianza uchunguzi .
“Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kudhalilishwa kwa watuhumiwa kwenye kituo cha Polisi cha Mafinga wilaya ya Mufindi.
“Malalamiko hayo yanatokana na kesi ya msingi iliyoripotiwa kituo cha polisi Mei 5 kwa jalada namba MFG/RB/1302/2019 kosa la wizi wa mafuta ya Dieseli, mota na mashine ya kuchoma vyuma kwenye kiwanda cha Hongwei International Company Ltd cha Mafinga na kupelekea watuhumiwa sita kukamatwa na kuhojiwa na polisi”ilisema ya Bwire.
Ilisema Malya ni miongoni mwa watuhumiwa sita waliokamatwa kwa hizo za wizi .
“Mara baada ya kupata taarifa hizo kama kamanda wa Polisi nilimuagiza Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai Issa J . Sulleiman – ACP kufungua jalada na kuanza upelelezi wa haraka sana ambapo alitekeleza maagizo hayo na kufungua jarada namba IRR/CID/PE/31/2019” ilisema.
Taarifa ilisema upelelezi ulibaini madai hayo si ya kweli.