POLISI WAKAMATA WAHALIFU 760 DAWA ZA KULEVYA, UWINDAJI HARAMU

0
733

Na Ashura Kazinja- Morogoro

WAHALIFU zaidi ya 760 wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro katika msako wa kipindi cha mwezi mmoja, wakiwamo 25 wanaojihusisha na dawa ya kulevya na uwindaji haramu, ambapo pembe za ndovu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 zimekamatwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema kati ya wahalifu hao, 25 wanajihusisha na uwindaji haramu, dawa ya kulevya na 22 ambao walisalimisha silaha zao aina ya gobore zinazotumia baruti na marisao (gololi).

Kamanda Matei alisema jumla ya silaha 26 zikiwamo pisto 1, gobore 25, risasi za shortgun 4 pamoja na vipande 5 vya pembe za ndovu na pembe  za ndovu mbili nzima zenye thamani  zaidi ya shilingi milioni 100 zimekamatwa.

Alisema Oktoba 12 saa saba mchana katika maeneo ya Mtakuja Kata ya Dakawa wilayani Mvomero, walikamatwa watuhumiwa 5 wote wanaume wakiwa na pistol moja aina ya revolver 32 S&W long yenye namba R.374973 .

Aidha, alisema silaha nyingine aina ya gobore 1 inayoweza kutumia risasi 2 za shortgun, iliyokuwa imehifadhiwa katika mfuko wa salfeti iliokotwa na askari polisi waliokuwa doria Oktoba 19 mwaka huu saa 8 mchana katika Kijiji cha Madato wilayani Kilosa.

Pia alisema wananchi wa Kijiji cha Mlunga Wilaya ya kipolisi Ruhembe na wa Kitongoji cha Ibanda Kata ya Uleling’ombe Tarafa ya Mikumi, walisalimisha jumla ya magobore 22 kufuatia agizo la Kamanda wa Polisi

Mkoa wa Morogoro la kusalimisha silaha zote zinazomilikiwa na wananchi kinyume cha sheria.

Matei alisema watuhumiwa wengine watatu walikamatwa mmoja akiwa na magobore 2 yenye namba 9916 na 539 na wengine wawili waliokuwa na risasi 2 za silaha aina ya shortgun bila kibali.

Alisema mtu mmoja aitwaye Nehemia Nashoni, alikamatwa Novemba 8 katika maeneo ya Nanenane Hoteli ya B-Z na baada ya kupekuliwa alikutwa na pembe za ndovu vipande vitano na pembe za ndovu nzima 2 alivyokuwa amevihifadhi kwenye begi jeusi vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 100 na hatua za kumfikisha mahakamani zinaendelea.

Hata hivyo, Kamanda Matei, amewapongeza wananchi kwa kushirikiana vyema na Jeshi la Polisi katika kuwafichua wahalifu na kuzitaka halmashauri kuacha kutoa vibali vya umiliki wa silaha kiholela.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here