Polisi wakamata bunduki nne za kivita

0
889

Walter  Mguluchuma,Katavi.

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi,  limekamata bunduki nne maeneo tofauti tofauti  katika makazi ya wakimbizi  Katumba wilayani  Mpanda na Mlele.

Katika msako huo, watuhumiwa kadhaa wametiwa mbarano na wengine wanaendelea kutafutwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga alisema silaha hizo zilikamatwa wakati wa msako mkali kwa kushirikiana na wananchi ambao ni raia wema.

Alisema ukamataji ilifanyika Desemba 17, mwaka huu  saa 2 usiku, polisi wakiwa doria pori  la Nzaga, makazi ya wakimbizi  kambi ya Katumba wilayani,walikamata silaha moja ya kivita aina ya Ak-47 yenye namba 340736, ikiwa na magazine moja isiyokuwa na risasi iliyotupwa na mtu anayefahamika kwa majina ya Barotel Mjeshi mkazi wa Kijiji cha Ivungwe-B.

Alisema mtuhumiwa alipogundua anafuatiliwa,aliamua kutupa silaha hiyo na kutokomea kusikojulikana.

Alisema Novemba 26, mwaka huu ndani ya makazi hayo saa 3 usiku barabara ya tano ya Kijiji cha Ivungwe, walimkamata Leonidas Etien(36) mkazi wa Kijiji cha Kalunga akiwa na  silaha aina ya Ak-47 namba 6096282 na Mussa Chubwa(30) mkazi wa Kijiji cha Katumba, wakiwa silaha ya kivita aina ya Ak-47 namba 3314805, ikiwa na magazine moja isiyokuwa na risasi.

Alisema Novemba mosi, mwaka huu, saa 4 usiku Kijiji cha Kamalampaka polisi  kwa kushirikiana na vikosi vingine,walifanikiwa kukamata silaha moja ya kivita iliyokuwa na magazine moja, isiyokuwa na risasi ikiwa imetelekezwa porini.

Pia alisema jeshi hilo, limekamata silaha zingine nne za kienyeji aina ya gobole na msako unaendelea ili kubaini na kutokomeza mtandao  wa utumiaji na umiliki wa silaha za kivita.

Katika hatua nyingine jeshi hilo, limekamata dawa za binadamu na vifaa tiba katika kituo cha afya Inyonga  ambazo zinadaiwa Dk. Calvin Mnaso .

Mtuhumiwa alikamatwa baada ya polisi taarifa juu ya wizi huo na  walifika nyumbani kwake kufanya upekuzi na kukuta akiwa na boksi tano zilizokuwa na dawa mbalimbali za kutibu wanadamu ,vifaa vya kupima maradhi ya binadamu,vifaa vya upasuaji na tohara ,godoro moja,sindano ambazo zote ni mali ya Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here