29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wagoma kuchangia mafuta kusafirisha mwili wa mwenzao

Na Ahmed Makongo, Bunda
POLISI wilayani Bunda, mkoani Mara, wanadaiwa kugoma kuchangia fedha za mafuta kwa ajili ya kusafirisha mwili wa askari mwenzao, Koplo Mahamudu Magasa, aliyefariki dunia baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria kwa muda mfupi.
Mafuta hayo yalikuwa yanatakiwa kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Koplo Mahamudu kwenda nyumbani kwako, Wilaya ya Mahenge, mkoani Morogoro.
MTANZANIA jana ilifika Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bunda na kukuta umati mkubwa wa askari polisi wakiwa kituoni hapo, wakipinga hatua ya kulazimishwa kuchangia mafuta kwa vile si jukumu lao.
Walisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha wazi kwamba Serikali haithamini utumishi wao, kwani watumishi wa idara nyingine wanapofariki dunia fedha hutolewa na Serikali kwa ajili ya kusafirisha miili yao.
“Leo (jana) kafariki dunia mwenzetu imekuwa hivi, je, kama angekuwa mke wake au mtoto ingekuwaje, si ndiyo aibu kabisa,” alisema askari mmoa ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Walisema siku zote wamekuwa wamejiwekea utaratibu endapo mwenzao anafariki dunia huchangia Sh 5,000 kila mmoja, ili ziweze kusaidia familia ya marehemu na si kuchangia mafuta ya kusafirisha.
Hata hivyo, wakati polisi hao wakiwa wamekusanyika nje ya kituo hicho wakipinga hatua hiyo, maofisa wa jeshi hilo wilayani hapa wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bunda (OCD) Gwisael, walikuwa kwenye kikao cha pamoja.
Gazeti hili lilipata nafasi ya kuzungumza na OCD Gwisael, ambaye alikanusha madai ya askari hao kuchangishwa fedha za mafuta.
Alisema askari hutoa mchango wa Sh 5,000 kwa hiari yao kama ilivyo kawaida na siyo za mafuta ya Sh 10,000 kama inavyodaiwa na baadhi ya askari.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philipo Kalangi, akizungumzia tukio hilo alisema ofisi yake imetoa gari na lita 220 za mafuta kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Koplo Magasa.
Alisema ni marufuku kwa askari yeyote kuchangishwa mchango wa mafuta.
“Tayari nimeshatoa gari na mafuta lita 220 kwa ajili ya kusafirisha mwili wa askari wangu… pia tunatoa na posho ya kujikimu kwa askari watakaosafirisha mwili wa marehemu, nani kawaambia wachangie tena…sisi tuna utaratibu wetu wa Serikali, siyo kuchangisha askari fedha za mafuta,” alisema Kamanda Kalangi
Gazeti hili jana saa 7:52 mchana lilishuhudia gari la polisi lililotumwa na Kamanda Kalangi kutoka mjini Musoma, lenye namba za usajili DFP 1822, likiwa Kituo cha Polisi Bunda kwa ajili ya kuanza safari ya kwenda Mahenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles