25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Polisi Ugiriki wakabiliana na wakimbizi wanaojaribu kuingia Ulaya

KASTANIES, UGIRIKI

POLISI nchini Ugiriki imetumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wakimbizi waliokusanyika kwenye mpaka kati ya nchi hiyo na taifa jirani la Uturuki.

Taarifa kutoka nchini humo zilieleza kuwa wakimbizi hao walifika kwenye mpaka huo baada ya Alhamisi wiki hii Uturuki kutangaza kuwa haitazuia tena wakimbizi walioko kwenye ardhi yake ambao wanataka kwenda barani Ulaya.

Picha za matukio kutoka nchini humo ziliwaonesha askari polisi wa kupambana na ghasia wa Ugiriki wakitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya makundi ya wahamiaji, yaliyokuwa yakiwakabili polisi mawe.

Msemaji wa Serikali ya Ugiriki, Stelios Petsas, alisema kuwa serikali yake itafanya kila njia inayowezekana ili kulinda mipaka yake dhidi ya wakimbizi.

Wimbi hilo jipya la wakimbizi wanaojaribu kuingia barani Ulaya kupitia Ugiriki wakikimbia vita vinavyoendelea katika jimbo la Idlib nchini Syria, ambapo hapo juzi kiasi cha wanajeshi 33 wa Uturuki waliuawa katika mapigano dhidi ya kundi la dola ya kiislamu ya IS.

Hata hivyo, Petsas alidai kuwa wimbi hilo jipya la wakimbizi halina uhusiano wowote na hali inayoendelea huko Idlib na kusisitiza kuwa nchi hiyo imewazuia wakimbizi wapatao 4,000 kuingia kwenye ardhi yake katika muda wa saa 24.

Ugiriki ambayo kwa muda mrefu imekuwa na mivutano na Uturuki, ilikuwa njia kuu iliyotumiwa na mamia ya maelfu ya wakimbizi walioingia barani Ulaya kati ya mwaka 2015 na 2016, mara hii inasisitiza kuwa haitaifungua mikono yake.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters zaidi ya watu 500 walikuwa wamepiga kambi katika eneo hilo na kwamba mamia wengine walikuwa wakisubiri upande wa mpaka wa Uturuki.

Taarifa zinaeleza kuwa wakimbizi wengine zaidi ya 3,000 walikuwa wakisubiri kuvuka mpaka kuingia Ulaya katika mji wa Kastanies mpakani upande wa Uturuki.

Aidha Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Edogan, alinukuliwa akisema kuwa wakimbizi wapatao 18,000 tayari wamekwishaondoka Uturuki na tayari wamefika upande wa Ulaya.

Inaelezwa kuwa waandishi wa habari wanaofuatilia mzozo huo wamezuiwa umbali wa kilomita moja kutoka katika mji wa Kastanies.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2015, zaidi ya wakimbizi milioni moja waliingia Ulaya wakitokea Uturuki, jambo lililosababisha mzozo mkubwa wa wahamiaji katika bara hilo.

Hata hivyo makubaliano yaliyosainiwa kati ya EU na Uturuki mwaka 2016 yamesababisha wakimbizi wengi kusalia nchini Uturuki.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles