NA ASIFIWE GEORGE,
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemtaka mwigizaji wa vichekesho wa kundi la Orijino Komedi, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ ajisalimishe Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano kabla hawajamharibia ‘honeymoon’ yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Hezron Gyimbi, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba jeshi lake linajua alipo Masanja kwa ajili ya mapumziko yake, hivyo ni vyema ajisalimishe bila shuruti kabla hawajamkamata.
“Tunamtangazia leo ajisalimishe mwenyewe kituo kikuu kwa mahojiano, lakini akikiuka na kwa kuwa tunafahamu alipo tutakwenda kumkamata huko huko bila kujali ‘honeymoon’ yake,’’ alieleza Kamanda Gyimbi.
Gyimbi aliongeza kwamba miongoni mwa mambo wanayotaka kujua kutoka kwa Masanja ni kwamba yeye ndiye aliyewakodishia ama kuwashonea sare hizo waigizaji wenzake wakazitumia siku ya harusi yake ama la.
“Unapovaa sare za Jeshi la Polisi huwezi kufanya mambo kinyume cha maadili ya jeshi hilo, mfano askari hawezi kucheza kama walivyokuwa wanafanya Joti na wenzake wakiwa wamevaa mavazi hayo, kuvaa na kuyatumia vile ni kinyume cha sheria,” alisisitiza Gyimbi.
Juhudi za kumpata Masanja Mkandamizaji ili azungumzie mwito huo wa Polisi hazikufanikiwa, kwa kuwa simu yake haikupatikana.