Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
MSANII maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu, atapandishwa kizimbani baada ya kupekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na msokoto wa bangi na karatasi za kufungia dawa hizo za kulevya.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema Wema atapandishwa kizimbani pamoja na mwenzake Omar Michen aliyekutwa na kete tatu za dawa zizaniwazo kuwa za kulevya.
Mbali na hao, watuhumiwa wengine 10 wa dawa za kulevya pia watapelekwa mahakamani kupata kiapo cha hakimu ili wawe chini ya uangalizi wa mahakama na Jeshi la Polisi katika kipindi cha miaka miwili.
“Huyu Wema baada ya kuhoji wenzake ambao anatumia nao, walieleza vizuri na alipokwenda kupekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na msokoto wa bangi na baadhi ya karatasi ambazo anatumia kufunga bangi, hili halina ubishi kwamba ni mtumiaji wa dawa za kulevya… tuna evidence (ushahidi) wa kutosha.
“Tukimuhoji mtu hata kama akisema anayemuuzia yuko Musoma au Zanzibar, lazima tutakwenda. Wengine wanakwambia wanapenda heroin, cocaine au bangi na wanasema kabla hawajaingia kwenye ‘stage’ (jukwaani) huwa ni lazima wapate mzuka,” alisema.
Alisema wamekamata kete 299 za dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya ambazo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi na kukamata misokoto mikubwa 104 na midogo 107.
RC MAKONDA
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa siku 10 kwa wazazi wenye watoto wanaotumia dawa za kulevya kujisalimisha nao polisi.
Pia ametoa siku 10 kwa wenyeviti wa mitaa kutoa taarifa za watu wanaotumia au kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Baada ya siku 10 tukimkamata mtu mwenye dawa za kulevya katika mtaa wako na wewe hujajishughulisha, tutaamini na wewe ni sehemu ya wanaonufaika.
“Haya mapambano si ya mtu mmoja na kelele nyingine mnazozisikia zinatupa hamasa tuendelee kufanya kazi, tunachotafuta sisi ni majibu, tukifika mbinguni tumweleze Mungu kwamba dhamana uliyotupa tuliitendea haki,” alisema Makonda.
Tangu Makonda awataje baadhi ya wasanii na wafanyabiashara wanaodaiwa kuhusika na dawa za kulevya wiki iliyopita, idadi ya watuhumiwa hao imefikia watu 112.