Amon Mtega -Songea
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, amewataka wakazi wa mkoa huo kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo viovu kwenye jamii ili kuvikomesha.
Wito huo aliutoa jana wakati akionyesha baadhi ya vitu vilivyoibwa kwa wananchi, zikiwemo televisheni, mafuta ya kula, pombe na spika za redio vilivyokamatwa kwenye msako unaoendelea mkoani hapa.
Kamanda Maigwa alisema ili kukomesha vitendo hivyo, wananchi wanatakiwa kuimarisha ulinzi na kuendelea kutoa taarifa za watu wanaovifanya.
Alisema kufuatia uhalifu huo watu wanne wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa kuwabaini wengine unaendelea ili kuuvunja mtandao wa wahalifu.
Kamanda Maigwa alisema wahalifu hao wamekuwa wakivunja majumba ya watu na maduka kisha kuiba mali zikiwemo televisheni.
Alisema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria ili wajibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda Maigwa aliwataka wakazi wa mkoa huo ambao waliibiwa vitu vyao, kwenda kuvitambua vitu Kituo Kikuu cha Polisi.