24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi Mwanza watumia mabomu kutawanya wafuasi Chadema

3NA JOHN MADUHU, MWANZA

JESHI la Polisi mkoani Mwanza, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafuasi zaidi ya 500 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokuwa wamefurika katika Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya kushuhudia mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita marehemu Alfonce Mawazo ambaye alifariki dunia kwa kukatwa mapanga.

Mawazo alifariki juzi katika mazingira ya kutatanisha huku kifo chake kikihusishwa na masuala ya kisiasa.

Wafuasi hao wa Chadema kutoka katika mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa,  walifika hospitalini hapo wakiwa katika msafara wa magari zaidi ya 50.

Mwili wa marehemu Mawazo ulihamishiwa hospitalini hapo kutoka mkaoni Geita, huku ukisindikizwa na wafuasi wa Chadema ambao waliungana na wenzao wa Mkoa wa Mwanza.

Msafara huo wa kusindikiza mwili huo uliwasili Hospitali ya Bugando saa 10 jioni lakini msafara huo ulijikuta ukikwama baada ya walinzi wa hospitali hiyo kuzuia magari mengine, huku wakitoa maelekezo ya kuruhusu magari mawili tu kwa ajili ya kuhifadhi maiti.

Kutokana na maelekezo hayo ya mofisa usalama wa hospitali wafuasi hao wa Chadema waligoma na kutaka magari yote yaruhusiwe kuingia katika eneo la hospitali hali iliyowafanya walinzi hao kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Baada ya dakika chache Polisi walifika katika eneo hilo na kuwataka wafuasi hao kuondoka katika eneo hilo kwani wanaleta usumbufu kwa wagonjwa kutokana na kelele walizokuwa wakipiga, ambapo wengine walikuwa wakiimba nyimbo za Chadema.

Pamoja na jitihada za Polisi kuwataka wafuasi hao wa Chadema kuondoka katika eneo hilo, juhudi zao ziligonga mwamba na kuwalazimu kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatanya wafuasi hao waliokuwa wamejaa katika eneo hilo la hospitali.

Kutokana na vurugu hizo MTANZANIA ilimtafuta kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo,  lakini hakuweza kupatikana huku simu yake ya mkononi ikiita muda mrefu bila majibu.

Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustine Senga, alisema Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafuasi hao wa Chadema, kutokana na vurugu zilizokuwapo.

“Tumefanikiwa kudhibiti vurugu hizo ni suala la kutokuelewa tu, taratibu za hospitali ya rufaa ya Bugando ziko wazi, walitaka kulazimisha vitu ambavyo haviwezekani, tumewakamata baadhi yao tunaendelea na mahojiano,” alisema RCO Senga.

Marehemu Mawazo alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifariki dunia baada ya kushambuliwa kwa mapanga na shoka katika eneo la Katoro wilayani Geita na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.

Mawazo alikutwa na mauti saa tisa alasiri juzi akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita baada ya kushambuliwa alipokwenda kwa ajili mkutano wa kampeni ya udiwani wa Kata ya Ludete.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjoli, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini hakutaka kutoa maelezo zaidi kwa madai kuwa alikuwa akielekea eneo la tukio, lakini kwa mujibu wa mashuhuda, Mawazo alishambuliwa saa tano asubuhi.

Ilidaiwa kuwa kabla ya kwenda katika mkutano wa kampeni, Mawazo alikuwa kikaoni Mjini Katoro na baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichokuwa cha ndani aliondoka kuelekea Ludete, lakini akiwa njiani ndipo alipovamiwa na kundi la vijana hao na kuanza kushambulia msafara wake na yeye kujeruhiwa vibaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles