POLISI: LISSU HATOKI

1
769

AGATHA CHARLES Na YASSIN ISSAH

KUNA kila dalili zinazoonyesha kuwa Jeshi la Polisi limeamua kushughulika na mwenendo wa kauli za mwanasiasa machachari, Tundu Lissu.

Hilo linaweza kuthibitishwa na kauli iliyotolewa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lucas Mkondya, kuwa Jeshi hilo halitamwachia huru Lissu hadi pale upelelezi utakapokamilika na kisha kumfikisha mahakamani.

Si hilo tu, hatua ya Jeshi hilo kuwazuia mawakili wa Lissu, Peter Kibatala na Fatma Karume kuonana naye inaweza kuwa na tafsiri hiyo hiyo.

Watu ambao wamekuwa wakifuatilia matukio ya Lissu kukamatwa na Jeshi la Polisi wanasema wanashangaa hatua ya sasa kutokana na huko nyuma Lissu kuruhusiwa kuonana na wanasheria wake na kupata dhamana kwa wakati.

Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, anashikiliwa tangu juzi na jeshi hilo kwa tuhuma za uchochezi.

Alikamatwa juzi saa 12 jioni katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akiwa anaelekea Kigali, nchini Rwanda, kuhudhuria mkutano wa Wanasheria wa Afrika Mashariki ulioanza jana.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Mkondya, ambaye alikiri kuendelea kumshikilia Lissu, alisisitiza kwamba hawawezi kumwachia hadi upelelezi utakapokamilika, kwa kile alichodai kuwa amekuwa akitumia kichaka cha ubunge kuchochea uhalifu.

“Bado tunaendelea kumhoji, hatumwachii, anatumia kichaka cha ubunge kuchochea uhalifu, tunaye na tukikamilisha upelelezi ni mahakamani,” alisema Mkondya.

Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata jana jioni na kuthibitishwa na wakili wake, Kibatala, zilieleza kuwa Lissu amekataa kutoa maelezo yoyote hadi atakapofikishwa mahakamani na zaidi amekataa kuchukuliwa vipimo vya mkojo baada ya kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Pamoja na hilo, inaelezwa kuwa, Polisi pia walifika nyumbani kwa Lissu na kisha kufanya upekuzi.

Taarifa hizo za Lissu kupekuliwa na kisha kufikishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali zilithibitishwa pia na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema.

“Ni kweli wamempeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kutaka kumpima mkojo, lakini alivyofika Lissu alikataa akawaambia mashtaka waliyomfungulia hayahusiani na yeye kupimwa mkojo.

“Baada ya hapo walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi na walianzia maktaba yake, mpaka sasa (12:41 jioni) wanaendelea na huo ukaguzi wao na hatujui ni nini wanatafuta hasa,” alisema Mrema.

Awali akizungumza na waandishi wa habari nje ya Kituo Kikuu cha Polisi, baada ya kukataliwa kumuona Lissu, Wakili wake, Fatma Karume, alisema mwanasiasa huyo anashikiliwa kwa kosa la uchochezi.

“Alipokamatwa jana (juzi) alinipigia simu, akaniomba nimwakilishe, na nilimwambia niko tayari, nimekuja jana usiku (juzi) na polisi walimhoji akasema hana masuala yoyote ya kujibu, lakini usiku wa jana wamemcharge (wamemshitaki) kwenye saa 1:30 hivi kwa kosa la uchochezi,” alisema Fatma.

Fatma alisema suala la uchochezi ni la kisheria zaidi na kwamba inapaswa ionekane nani kachochewa na kwa kufanya jambo gani la uhalifu.

Alisema Lissu alimpigia simu akimwomba kumwakilisha kwa kuwa pia ni rafiki yake na kwamba jana alifika kituoni hapo saa 4:45 za asubuhi, lakini alizuiwa getini kuingia kwa madai kuwa ni amri kutoka juu.

“Jana (juzi) tulivyouliza hawajasema kamchochea nani, na kamchochea kufanya jambo gani, kwa hivyo wametumia tu lile kosa la kuchochea kama kisingizio tu,” alisema Fatma.

Alisema baada ya dakika 45 za yeye kukaa nje, Wakili Peter Kibatala alionana na Ofisa mmoja wa Polisi ambaye alizungumza naye na baadaye waliruhusiwa kuingia ndani.

“Baada ya kama dakika 45 hivi, wakili mwenzangu Kibatala alizungumza na Ofisa mmoja wa Polisi, nafikiri jina lake Kingai, akatoa ruhusa tuingie. “Nilimuuliza Kingai, Lissu mtampeleka mahakamani lini, jana (juzi) msham-charge (mshitaki) kimebaki kumpeleka mahakamani, akaniambia hawajui watampeleka lini, na bado wanaendelea na upelelezi,” alisema Fatma.

Fatma alisema anavyofahamu ni kwamba upelelezi unafanyika na kupata ushahidi ndipo mhusika anakamatwa na kupelekwa mahakamani.

“Hivyo Polisi kama wanadhani wanaweza kumkamata mtu bila ya upelelezi kukamilika ili waendelee kumweka mahabusu, hiyo haiwezekani,” alisema Fatma.

Alisema kutokana na hilo, waliamua kulishtaki Jeshi la Polisi Mahakama Kuu wakiomba Lissu afikishwe mahakamani.

“Leo ndio tumepeleka nyaraka za kuiomba mahakama ili Lissu kama ana kesi waikabidhi mahakama na si kumweka selo ya polisi mpaka wao watakapotimiza uchunguzi wao,” alisema Fatma.

Alisema kutokana na jana kuzuiwa kuonana na mteja wake, alimwomba Ofisa huyo wa Polisi amruhusu afike kituoni hapo leo, lakini alimjibu kuwa hajui.

Hali nje ya Kituo

MTANZANIA Jumamosi ambalo lilifika kituoni hapo saa nne asubuhi, lilizuiwa kuingia ndani kwa madai kuwa hakukuwa na taarifa za mkutano wa waandishi na kwamba kama kuna lolote lisubiri pembeni litajulishwa.

Licha ya waandishi kuruhusiwa kukaa pembeni, saa 5: 58 alifika Ofisa mmoja wa Polisi na kuwataka kuondoka eneo hilo.

“Mna appointment? Hapa sio sehemu ya mkusanyiko. Nendeni mkatafute habari huko sehemu maalum au mpigieni Inspekta,” alisema Ofisa huyo.

Hata hivyo, waandishi ambao muda huo walikuwa wamejibanza katika eneo la stesheni karibu kabisa na kituo hicho waligoma kuondoka na kuwataka polisi kuwaacha kwani nao wako kazini.

Baada ya mabishano hayo ya muda, polisi hao waliondoka kurudi kituoni hapo.

Mbali na waandishi, pia walikuwapo baadhi ya wafuasi wa Chadema, ambao nao waliondolewa eneo hilo, huku wengine wakizuiwa kuingia ndani.

Nje ya geti la kituo hicho, kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi ambao walionekana kuzunguka wakiwa na silaha.

Wakati hayo yakitokea Kituo Kikuu cha Polisi, maofisa wa jeshi hilo walikuwa wakihaha  kukamilisha upelelezi dhidi ya Lissu.

Katika kukamilisha upelelezi huo, kwa nyakati tofauti jana, maofisa hao waliwahoji waandishi wawili wa habari walioripoti mkutano wa Lissu uliofanyika Jumatatu ya wiki hii.

Waandishi waliohojiwa ni pamoja na mwandishi wa gazeti hili, Aziza Masoud na Ibrahim Yamola wa gazeti la Tanzania Daima.

Maofisa hao wawili wanaume na mmoja mwanamke, wakijitambulisha kutoka Kituo Kikuu cha Polisi, walifika kuwahoji waandishi hao kila mmoja katika kituo chake cha kazi.

Taarifa ilizonazo gazeti hili, Yamola alihojiwa saa 3:00 asubuhi, wakati Aziza akihojiwa saa 5:30 asubuhi katika ofisi za gazeti hili, zilizopo Sinza Kijiweni.

Mahojiano kati ya maofisa hao na Aziza yalichukua takribani saa moja.

Akizungumza na gazeti hili, Yamola alisema: “Mimi walinipigia simu, awali walitaka niende Central (Kituo Kikuu cha Polisi), lakini niliwaambia sitaweza, ndipo walipoahidi kunifuata leo (jana) kwa  kunihoji”.

Alisema katika mahojiano yake, ambayo yalichukua takribani dakika 55, walikuwa wakiuliza kuhusu habari aliyoiandika na alipata fursa ya kutolea ufafanuzi kile nilichokiandika tu.

“Kuna muda walikuwa wanataka kutoka nje ya kitu nilichoandika, lakini nilisimamia kilichomo kwenye gazeti kulingana na misingi ya uandishi, ilifika muda nililazimika kushika gazeti ili niwasomee kilichomo,” alisema Yamola.

Wakati huo huo, Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kimelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata na kuendelea kumshikilia Rais wa chama hicho, Lissu, kwa makosa ya uchochezi.

Taarifa iliyotolewa jana na Makamu Rais wa TLS, Godwin Ngwilimi, ilieleza mawakili walipojaribu kuhoji Lissu aliwachochea akina nani, na alifanya kosa hilo wapi, wakajibiwa kuwa uchunguzi bado unaendelea.

“Kwa maoni na mtazamo wetu, Lissu anashikiliwa kwa kitendo cha kutoa maoni yake binafsi, basi kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria za nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa katika vipindi tofauti, hususan Ibara ya 18 ya Katiba hiyo, kwani inatoa na kulinda uhuru wa kutoa maoni kwa watu wote bila kujali kabila, rangi na imani.

“Haki hii ya msingi pia inatamkwa bayana katika mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imetia saini na kuiridhia, kama vile Tamko la Kimataifa la Haki za Kijamii na Kisiasa la mwaka 1966 (International Covenant on Civil and Political Rights) na Tamko la Afrika la Haki za Binadamu la mwaka 1986 (The African Charter on Human and Peoples’ Rights),” alisema Ngwilimi.

Alisema TLS inalaani na kupinga vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata watu wanapotoa maoni yao binafsi kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yao, kwamba ni vema nchi ikaendeleza utamaduni wa kuvumilia maoni tofauti na kukosoana bila kupigana.

Lissu alikamatwa ikiwa ni siku moja baada ya Jumatano  kung’ang’ania ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, ili kukwepa kukamatwa na polisi.

Lissu anadaiwa kukamatwa kutokana na kauli alizozitoa katika mkutano na waandishi wa habari alioufanya hivi karibuni, ambapo alizungumza mambo mbalimbali kuhusu serikali na viongozi wake.

 

 

Kubenea na Polisi

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limesema linamtafuta Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, kutokana na malalamiko aliyoyatoa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba.

“Tunamtafuta popote alipo Tanzania hii na ajitokeze yeye mwenyewe, hii Tanzania ni ndogo, aje atupe ushirikiano tumalizane na hili,” alisema Mkondya.

Hivi karibuni, Kubenea alifanya mkutano na vyombo vya habari kama Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wa CUF iliyo chini ya uongozi wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif na kutangaza operesheni ya kumwondoa Profesa Lipumba katika ofisi za chama hicho, zilizopo Buguruni.
Baada ya Kubenea kutangaza operesheni hiyo, siku mbili baadaye, Profesa Lipumba alikwenda kutoa malalamiko polisi.

Mbali na hilo la Kubenea, taarifa nyingine zinadai kuwa, Mwenyekiti wa Taasisi ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, jana alihojiwa kwa mara nyingine na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, taarifa hizi zilishindwa kuthibitishwa na Kaimu Kamanda Mkondya, huku simu ya Sheikh Khalifa ikiita pasipo majibu.

Bado haijajulikana iwapo Sheikh Khalifa alikuwa bado mikononi mwa polisi au aliachiwa.

Hivi karibuni Sheikh Khalifa alizungumza na kuunga mkono hotuba ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, juu ya masheikh wa uamsho pamoja na matamshi mengine aliyotoa juu ya Waislamu nchini.

1 COMMENT

  1. Mazingira ya uhuru ktk nchi hii yapo shakani, majibu ya jeshi la Polisi hayaridhishi kabisa, kuna kila dalili siasa ndiyo sababu ya yote haya, wanajaribu kukwepa hili lkn wanashindwa kulitolea maelezo, sisi kwa Mtazamo wetu Jeshi letu linatumika kisiasa kwa maslahi ya chama cha mapinduzi, polisi hawataki kulikataa hili pengine kwa sababu ya mfumo wetu wa kisiasa ulivyo, kwa hali hii tunahitaji katiba mpya

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here