25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi kumulika Chadema

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

NA ELIZABETH MJATTA

JESHI la Polisi limetangaza kuanzisha uchunguzi wa kina dhidi ya viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliotajwa na kada wa zamani wa chama hicho, Habibu Mchange, kujihusisha kupanga na kutekeleza njama zenye mwelekeo wa ugaidi.

Limesema tuhuma zilizotolewa na Mchange zimelishtua, hivyo zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa hali ya juu, unaohusisha mwenendo wa uchunguzi wenye tahadhari wa makosa ya jinai, unaopaswa kuendeshwa na makachero waliobobea kwenye kazi ya upelelezi.

Tamko la kuanzishwa kwa uchunguzi huo limetolewa jana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, katika mahojiano na MTANZANIA Jumapili kupitia simu ya kiganjani alipotakiwa kutoa tathmini iliyofanywa na polisi dhidi ya makundi mawili yenye uhasama wa kisiasa yaliyoshutumiana hadharani kupanga na kutekeleza mauaji.

Mngulu alisema ungamo la Mchange kuwa alishiriki kwa namna moja au nyingine kupanga mipango ya mauaji, kuvuruga amani ya nchi na kulihusisha Jeshi la Polisi na matukio ya mauaji aliyodai kutekelezwa na viongozi wa Chadema, linaangaliwa kwa mitazamo miwili.

Alisema mtazamo wa kwanza unaweza kuwa upotoshwaji unaofanywa makusudi ili kuwahadaa polisi wasiendelee na uchunguzi wanaoufanya kuhusu matukio hayo na kuanzisha mwingine mpya kulingana na tuhuma za Mchenge, na wa pili madai hayo yanaweza kuwa na ukweli ambao utawaongoza makachero kuwakamata wahusika halisi.

“Nilikuwa sina taarifa, lakini sasa baada ya kuzipata ninafuatilia ukweli wa kilichosemwa, lakini kumbuka wakati mwingine baadhi ya taarifa zinazotolewa ni mbinu ya kukutoa kwenye mstari sahihi. Tuseme labda wewe umeshamkamata Isaya anayetuhumiwa halafu mtu mwingine akajitokeza akakuambia aliyefanya tukio ni John wakati kumbe lengo lake ni kukuondoa kwenye mstari sahihi.

“Lazima tuwe na tahadhari kwamba mtu huyu alikuwa wapi toka mwanzoni, kama yeye alikuwa mtu mwema kwanini hakujitokeza mapema wakati tukio lilipotokea. Niseme tu kwamba nikipata hiyo taarifa rasmi ya Mchange itanirahisishia sana kazi,” alisema DCI Mngulu.

Alipotafutwa jana na MTANZANIA Jumapili kupitia simu yake ya kiganjani ili aeleze kama yupo tayari kulisaidia Jeshi la Polisi kuthibitisha tuhuma zake kwa viongozi wa Chadema, Mchange alisema tayari amekwishatoa ushahidi usiokuwa na shaka, unaowapa polisi mahali pa kuanzia upelelezi wao.

Mbali na ushahidi huo, alisema yuko tayari kushirikiana na jeshi hilo kueleza na kutoa ushahidi wa kile anachokijua kuhusu madai aliyoyatoa, na kuwataka polisi wamuite wakati wowote watakapohitaji msaada wake.

“Siyo tu kutoa ushahidi, nishautoa na niko tayari kuwaongezea taarifa na ushahidi mwingine nilionao wa kile nilichokieleza.

“Taarifa yangu yenyewe ni ushahidi tosha, lakini wakati wowote niko tayari kuwaongezea ushahidi na taarifa wanazozihitaji juu mauaji, niseme wazi Mbowe (Freeman) ni muuaji mkubwa,” alisema Mchange.

TUHUMA ZA MCHANGE

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Tamali Hotel, Dar es Salaam, Agosti 14 mwaka huu kwa lengo la kujibu tuhuma alizoelekezewa na uongozi wa Chadema kuwa alishiriki kupanga njama za kulipua helikopta iliyopangwa kuwabeba Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema ni madai ya kipuuzi yaliyoratibiwa na Tundu Lissu.

“Haingii akilini hata kidogo kwamba mimi nimepanga na CCM kuilipua helikopta ambayo ingewabeba Dk. Slaa na Mnyika. Upuuzi huu ulioratibiwa na Tundu Lissu, ni uthibitisho wa kushindwa na kuporomoka kisiasa kwa kasi ya ajabu kunakoikabili Chadema kwa sasa,” alisema Mchange.

Katika tuhuma nyingine, aliwataja Dk. Slaa, Lissu, Mbowe, Mnyika na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa ndio mabingwa wa matukio ya kigaidi na mauaji ya watu wanaotofautiana nao kimsimamo na mtazamo.

Mchange aliyataja matukio aliyodai viongozi hao kushiriki kuyapanga na kuyatekeleza kuwa ni pamoja na mauaji ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Chacha Wangwe,

Tuhuma nyingine ni kushiriki kikamilifu kupanga na kutekeleza mauaji yaliyotokea mkoani Arusha pamoja na kumtumia kijana aliyemuelezea wajihi wake kuwa ni mweupe, mwenye mazoea ya kufuga nywele nyingi, aliyechanganya uraia wa Tanzania na Ujerumani kutekeleza matukio ya kigaidi.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Habari hizi ni za kushtua sana. Lakini mtoa habari hizi anapaswa kuhojiwa kwa undani. Mbona alikalia habari hizi bila kuzitoa iwapo kweli zilitokea? Mbona basi amejitokeza mara baada ya yeye kushitumiwa kuwa alihusika na mipango ya
    ulipuaji wa ndege iliyombeba Dr. Slaa? Wakati wote huu habari hizi alizikalia bila kusema chochote. Kuna nini nyuma yake? Nchi yetu ni ya amani na itaendelea kuwa hivyo maana huo ndio mpango wa Mungu kwetu. Asitokee mtu kutuingiza katika chuki wenyewe kwa wenyewe kwa faida zake mwenyewe au kwa kutofautiana kiitikadi. Polisi wawe macho na masuala ya jinsi hii.

    • hili linashtua sana inaonekana huyu mtoa taarisa sio mkweli kabisaaa!!! kwa akili ya kawaida unaona je alikuwa wapi wakati wote huo? inaonekana kunakitu katoswa sasa anatafuta huruma ya kisiasa kwa jamii, waandishi wa habari naona pia muwe makini katika kuandika mambo kama haya kwakuwa hayana usaidizi wowote kwa jamii alikuwa wapi wakati wote huyu anaonekana anakitu fulani anataka kukipotosha anataka kupoteza ukweli aitwe na makachero na ahojiwe vizuri.

      naungana moja kwa moja na Kachero mkuu Isaya Mungulu huyu anaonekana kuna kitu anataka kukificha anapoteza malengo kwa polisi, huwezi kusema fulani ni muuaji wakati ulikuwa inajua na hukutoa taarifa anatakiwa kushughulikiwa huyu! kwanza kwa kutoa taarifa za kichonganishi.Kama ameshindwa kisiasa akae pembeni, nilipomuona sio mkweli anajichanganya ni pale alipoanza kusema tukio la iringa wakati polisi wakwisha maliza upelelezi wao na mtu aliyefanya mauaji hayo anatambuliwa anasubiri masuala ya kisheria. pia ningependa kumshauri kuwa watanzania sio wa kuwadanganya hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles