28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi kuendelea uchunguzi kifo cha aliyekuwa mgombea Serikali za Mitaa

JANETH MUSHI-ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limesema linaendelea na uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa mgombea ujumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mnara wa Voda, Kata ya Unga Ltd jijini hapa, Sirilli Homary, ambaye alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake.

Homary alikuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema, kabla ya chama hicho kujitoa katika uchaguzi huo uliofanyika juzi Jumapili, ambapo alikutwa amefariki dunia akidaiwa kuchinjwa.

Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shanna, alisema bado wanaendelea na upelelezi kuhusu tukio hilo na kuwa kwa sasa hakuna anayeshikiliwa.

“Bado tunaendelea na uchuguzi wa tukio hilo na tutakapokamilisha tutatoa taarifa zaidi,” alisema,

Juzi Kamanda Shanna alisema kuwa mwili wa Homary ulikutwa nyumbani kwake eneo la Mnara wa Voda, na inadaiwa tukio hilo lilitokea siku tatu zilizopita, huku ufunguo ukiwa ndani, hivyo inawezekana alijidhuru mwenyewe kutokana kile alichodai kuwa msongo wa mawazo.

Hata hivyo Kamanda Shanna alikemea tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaohusisha tukio hilo na masuala ya siasa kabla uchunguzi wake haujakamilika na kuwa watakaoendelea kufanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kuomba suala hilo liachwe kwa vyombo husika kwa uchunguzi.

Taarifa zaidi zinadai kuwa marehemu aliagwa na kusafirishwa jana kuelekea kwao eneo la Katesh wilayani Hanan’g mkoani Manyara kwa mazishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles