25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi jamii wafanikiwa kupunguza uhalifu mtaa wa Amani

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Vitendo vya uhalifu katika Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Liwiti vimepungua baada ya kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi shirikishi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti, Ignas Maembe na Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata, Mrakibu wa Polisi, Colle Senkondo, wakikata utepe wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Polisi Jamii Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Liwiti, Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Polisi Jamii Mtaa wa Amani, mgeni rasmi ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti, Ignas Maembe, amekipongeza kikundi hicho na kuwataka wananchi kukitumia vizuri ili kukomesha vitendo vya uhalifu kwenye maeneo yao.

“Tunaunga mkono jitihada za Mkuu wa Jeshi la Polisi hasa katika jukumu la ulinzi, sisi tunatekeleza maelekezo yake na tuna imani ulinzi utaimarika zaidi,” amesema Maembe.

Naye Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata Mrakibu wa Polisi, Colle Senkondo, amesema kupitia kituo hicho wahalifu watapatikana kwa urahisi na suala zima la uhalifu litapungua kama si kuisha kabisa.

“Uzinduzi wa kituo hiki ni faraja kwetu kwa sababu sisi kama polisi hatutoshi bila kushirikiana na wananchi. Kupitia kituo hiki watatusaidia kwa kuwa hawa wako karibu na wananchi na huko ndiko ambako wahalifu wanapatikana,” amesema Senkondo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Grace Mwingira, amewataka wananchi kulipa ada za ulinzi shirikishi kwa wakati ili kuwatia moyo vijana hao. Amesema kila kaya huchangia Sh 3,000 kwa mwezi.

“Wakati naomba kura kwa wananchi nilisema mtaa huu unasumbua kuhusu vibaka lakini nitahakikisha unakuwa na amani kama jina lake lilivyo, sasa hivi tunalala bila matatizo yoyote,” amesema Mwingira.

Kamanda wa Ulinzi Shirikishi Mtaa wa Amani, Erick Massawe, amesema uhalifu umepungua hasa eneo la Ladwa na kwamba wameshirikiana na polisi kuondoa vijiwe vyote vya bangi, dawa za kulevya na gongo.

Hata hivyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile kutokuwa na vifaa vya kutosha yaani pingu, tochi, filimbi, virungu, sare na usafiri wa kupeleka wahalifu kituoni.

Kikundi hicho chenye vijana 31 kina miaka miwili tangu kianzishwe huku wakimshukuru mama Joseph Shola na familia yake kwa kukubali kutoa jengo lake kuwa ofisi ya polisi jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles