25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Polisi sita watuhumiwa kuomba rushwa kwa mzee wa miaka 95

Na Abdallah Amiri -Igunga

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, inawachunguza askari polisi sita wa Kituo cha Igunga kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 8.

Polisi hao wanadaiwa kuomba kiasi hicho kutoka kwa mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa, Ngaka Mataluma (95) ili wasimpeleke kituoni.

Inadaiwa kuwa Juni 12, mwaka huu, askari hao walikwenda kwa Mataluma na kuomba Sh milioni 20, lakini wakajadiliana hadi Sh milioni 8.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley, alikiri kuwapo tukio hilo na kusisitiza kuwa wenye nafasi ya kulizungumzia vizuri ni Takukuru ambao ndio wanahusika zaidi na masuala ya rushwa.

“Suala hili nimelisikia, wenzetu wa Takukuru ndio wanaohusika zaidi na masuala ya rushwa, watafuteni, sisi tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwao, tutachukua hatua,” alisema Kamanda Nley.

Alipotafutwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Chaulo Mussa, alisema wako hatua za mwisho za kukamilisha upelelezi wa suala hilo.

“Ni kweli tukio hili lipo, tupo hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi wetu, baada ya hapo tutatoa majibu,” alisema.

Diwani wa Kata ya Isakamaliwa, Dotto Kwilasa (CCM) alisema baada kutokea tukio hilo, aliamua kuitisha mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na wananchi zaidi ya 680.

Alisema katika mkutano huo, wananchi walitoa malalamiko dhidi ya askari hao sita na viongozi wa Serikali wawili.

Askari hao ni  Inspekta Frank Matiku, PC Raphael Maloji, D.1 Koplo Paul Bushishi, PC Lome Laizer, DC Lucas Nyoni na Koplo Charles ambao wote wanafanya kazi Kituo cha Polisi Igunga.

Viongozi wa Serikali ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isakamaliwa, Edward Kitenya na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zahanati, Maulid Hamisi.

OC-CID

Ofisa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Igunga, Meshack Sumuni, alipoulizwa na wananchi wakati wa mkutano huo wa hadhara, alisema askari hao hawakutumwa na mamlaka yoyote kwenda Isakamaliwa, bali siku hiyo walitumwa kwenda Kata ya Itumba ambako kulikuwa kunafanyika uchaguzi wa diwani.

“Suala hili tunalishughulikia, siku hiyo hawa askari hawakutumwa Isakamaliwa kama ambavyo wanadai,” alisema.

DED

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Igunga, Revocatus Kuuli, alithibitisha kupokea barua na muhtasari wa mahudhurio ya wananchi waliomkataa Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Kitenya na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zahanati, Hamisi.

Alisema viongozi hao, wakimaliza kuhojiwa na Takukuru atawaita ofisini kwake ili wajieleze kutokana na tuhuma hizo.

DC IGUNGA 

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Igunga, John Mwaipopo, alisema suala hilo amelipata, lakini hajapewa majibu ya uhakika kutoka kwa Mkuu wa Polisi, Wilaya ya Igunga, Ally Mkalipa.

“Sijapata majibu ya msingi kuhusu tukio hili, nitalitolea majibu ya uhakika Jumatatu (leo),” alisema Mwaipopo.

SIMULIZI YA TUKIO

Juni 17, mwaka huu, Diwani wa Kata ya Isakamaliwa, Kwilasa aliitisha mkutano wa hadhara kusikiliza kilio cha wananchi, baada ya kusikia polisi wamefanya tukio hilo.

Katika mkutano huo, mtoto wa Mataluma, Nkende Ngaka alisimulia tukio zima na kusema Juni 12, mwaka huu saa 2 asubuhi, askari sita wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1825, wakiwa na silaha za moto walifika Isakamaliwa, kisha wakaenda kwa baba yake.

“Walifika nyumbani, waliposhuka kwenye gari yao walinihoji kwanini sipokei wageni, baadae waliniuliza kama mimi ni mganga wa kienyeji.

“Niliwajibu mimi sijihusishi na suala la uganga wa kienyeji, baada ya kutoa kauli hii waliniambia wao wamepotea njia,” alisema Nkende.

Alisema baada ya kuhojiwa hapo, askari hao waliamua kuondoka, lakini muda mfupi wakarudi tena na kumwamuru awapeleke kwa baba yake, Mataluma.

“Tulipofika kwa baba, walimuomba atoe leseni ya uganga, aliwaambia hana na wala shughuli za uganga hajawahi kufanya.

“Majibu haya hawakuridhika nayo, waliingia ndani na kuanza kupekua nyumba nzima, huku wakiwa hawana hati ya upekuzi, walipata rasta, kipande cha mifupa, kipisi cha msokoto wa bangi, ngozi ya kenge na kinyesi cha chatu na bunduki aina ya gobole.

“Baada ya kukamilisha upekuzi, waliomba wapewe kiasi kikubwa cha fedha (tumekihifadhi) ili wasimbebe baba yangu kwenda naye kituo cha polisi Igunga,” alisema.

Alisema baada ya kuambiwa watoe kiasi hicho, walihoji kosa walilofanya kwa kuwa vitu walivyodai wamekuta ndani vilikuwa vingine havipo.

“Pamoja na kupinga kutoa fedha hizo, polisi walimbeba baba yangu hadi ofisi ya mtendaji wa kijiji.

“Wakiwa ofisini kwa mtendaji, askari hawa, mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji walitaka tutoe Sh milioni 15 au 12 ili wamwachie, huku wakitutisha kwa maneno mengi. 

“Baada ya kugoma, wakashusha mpaka Sh milioni 10, tukagoma tena, kutokana na vitisho vikali tuliamua kuwapa Sh milioni 6, lakini wakaendelea kusisitiza kuwa wanataka Sh milioni 8,” alisema.

Alidai kuwa baada ya kuambiwa hakuna hela wanayotaka, wakamlazimisha baba yake awapigie wafanyabiashara waje kununua ng’ombe.

Naye Mataluma, alidai baada ya kuona hali tete na kuhofia usalama wake, aliamua kuwapigia wafanyabiashara na wakaja kununua ng’ombe 13 kwa Sh milioni 8 ambazo askari hao walizichukua.

Alidai kiuwa baada ya askari kupata fedha hizo, waliondoka na bunduki yake aina ya gobole ambayo anaimiliki kihalali.

“Walichukua bunduki yangu ambayo naimiliki kihalali siku zote, wameondoka nayo. Katika maisha yangu yote sijawahi kufanya vitendo vya uhalifu,” alidai.

WANANCHI

Mkazi wa kijiji hicho, Jilumba Hamko (81) ambaye ni mfugaji wa ng’ombe, alidai kuwa Juni  12, mwaka huu, baada ya askari kutoka kwa Mataluma walifika nyumbani kwake na kumpekua wakimwambia anajihusisha na upigaji ramli chonganishi tuhuma ambazo alikataa katakata.

Alidai kuwa baada ya kukataa, walimbeba hadi ofisi ya mtendaji wa kijiji ambako walimwamuru atoe Sh milioni 4 ili wamwachie.

Hamko alisema kuwa aligoma kutoa kiasi hicho cha fedha, lakini ghafla akajikuta akianguka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia.

“Wale askari baada ya kuona nimeanguka, waliniambia nitoe Sh 500,000. Sasa sikuwa na kitu, mwanangu  mmoja aliamua kutoa Sh 450,000  ndiyo wakaondoka,” alidai.

MWENYEKITI WA KIJIJI

Mwenyekiti wa Kijiji cha Isakamaliwa, Simon Makolo na Mwenyekiti wa CCM, Tawi la Isakamaliwa, Nkwabi Galishi, walisema baada ya kupata taarifa hiyo ya kusikitisha walitoa taarifa kwa Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Igunga,Francis Zuakuu na kuweka mitego kwenye minada yote.

Viongozi hao, walisema Juni 15, mwaka huu taasisi hiyo, ilifanikiwa kukamata ng’ombe 11 kati ya 13 katika mnada wa Igunga, wakiwa wanauzwa, huku wafanyabiashara walionunua ng’ombe hao walipowahojiwa walikiri kununua kwa Sh milioni 8 kutoka kwa Mataluma.

“Tulipigiwa simu tukiambiwa kuna ng’ombe wanauzwa, tulipofika tulikuta askari sita na tulitoa Sh milioni 8 tukampa Mataluma,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

MTENDAJI

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Isakamaliwa, Getruda Stanslaus, alisema ng’ombe 11 waliokamatwa na taasisi hiyo, wamerudishwa nyumbani kwa Mataluma kama ushahidi dhidi ya watuhumiwa ambao wapo chini ya uangalizi.

“Kitendo hiki walichomfanyia mzee Mataluma ni cha kinyama kabisa, ni aibu kwa askari waliopewa dhamana ya kulinda wananchi na mali zao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles