Na ASHA BANI
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole, ametuma salumu nzito, huku akiahidi kuchomoa mwanachama mmoja baada ya mwingine kutoka vyama vya upinzani.
Polepole alisema hayo juzi, wakati wa ziara yake wilayani Bagamaoyo mkoani Pwani, huku akitumia muda mwingi kujibu tuhuma zilizoelekezwa CCM na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye aliyesema kuwa wapinzani wamekuwa wakinunuliwa ili wahamie CCM.
Polepole, alisema anashindwa kuwaelewa wapinzani kwamba wakifanya wao sawa, lakini wakifanya wenzao wa upande mwingine inakuwa ni kama vile usemi wa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu uchungu.
“Siwaelewi wale jamaa, siwaelewi siwaelewi, mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu, akitoka kwao kuja kwetu kahongwa… wale wawili au watatu wametoka kwetu kwenda kwao na watu tulikuwa tunawatafutia ‘angle’ waondoke tukafungua mlango wakaporochoka wakaenda sijui wamewahonga shilingi ngapi, sisi hatukusema lolote.
‘’Na sijui kama tangu waondoke hao wamepata mwingine 2016 au 2017 na wahakikishia hatoki mtu tena kutoka kwetu kwenda kwao kwa sababu wameanza utovu wa nidhamu, sasa tutakuwa tunatoa mmoja baada ya mwingine, mmoja baada ya mwingine kwa sababu orodha ni ndefu sana wakijipanga ni kama wanakwenda kulipia kodi za majengo,’’alisema.
Alisema wapo wenyeviti, madiwani, wabunge, ambao amewazuia kuwapokea kwa sababu ni kama kundi linalokwenda kusajili kodi ya majengo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Aliwaahidi wana CCM wa Mkoa wa Pwani, kuanzia wiki hii atahakikisha anaotoa mmoja tu kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na ni kwa sababu hakuna muda wa kupokea wengine.
“Tutapokea mtu huyu, mmoja mmoja kutoka Mkoa wa Dar es Salaam,na nyota mmoja tu… basi kwa sasa hatuna muda tunaanza na mmoja tu ,’’alisema Polepole.
Aliwataka kuachana na maneno kwa sababu hayana msingi mzuri.
‘’Ukiadhibu kwenye moyo ni hatari kubwa, hatari kubwa kabisa,sasa kama wanataka huko wasije leta maneno maana chama chetu kinafanya siasa safi na uongozi bora.
Juzi Waziri Mkuu mstaafu, Sumaye alisema hana shida na madiwani wa Chadema kujiuzulu, lakini anashangaa sababu zao kufanana .
Alisema hawezi kuwalaumu kuhama kwao kwa kuwa hata yeye alitoka ndani ya CCM, lakini alikuwa si kwa kulazimishwa na mtu, bali ilikuwa ni matakwa yake.
Hivi karibuni Mbunge wa Viti Maalumu ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisikika akisema katika baadhi ya mikutano yake ya ndani na wanawake wa Umoja wa Wanawake (UWT) kuwa watahakikisha majimbo yote Mkoa wa Dar es Salaam, yanarudi mikononi mwao.
Kairuki aliwataka akina mama kujipanga kikamilifu kuhakikisha wanayachukua majimbo muda utakapowadia kwa sababu awali walifanya makosa na kuachia wapinzani.