24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

POLEPOLE, MNYETI WAMJIBU NASSARI

JANETH MUSHI, ARUSHA Na MANENO SELANYIKA- DAR



SIKU chache baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) kudai kuwa madiwani wa chama chake waliohamia CCM wamepewa rushwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, wamemtaka mbunge huyo kutoa ushahidi huo hadharani.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Polepole alimtaka Nassari kumtaja wazi aliyetoa na kupokea rushwa ili wahusika wachukuliwe hatua stahiki na kwamba CCM hawana maneno bali vitendo tu.

“Hii hoja ya kuhama inaonekana ni haramu kwa wanasiasa wanaotoka upinzani kuja CCM, lakini ni halali kwa wale wanaohamia upinzani wakitoka CCM au vyama vingine.

“Nashauri waache ‘kudololisha’ kama wana ushahidi wa rushwa waseme wasisubiri kuitwa Ikulu kwa Rais ndio wazungumze watakuwa wanapoteza muda wao.
“Zungumza wazi, fulani katoa fedha kiasi hiki amempa huyu, kwani ushahidi wa rushwa haudololishwi,” alisema Polepole.

Alisema kuna baadhi ya wapizani wameitwa na viongozi wa dini wakashikishwa Bibilia na Qurani ili wasihamie CCM.
Kutokana na hilo, Polepole alisema huo ni upumbavu na siasa mbaya, aliwataka wawe na akiba ya maneno kwani watu wanayo haki na uhuru wa kwenda chama watakacho kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema mtu yeyote akihamia chama fulani aachwe, kwani wapo viongozi waliokuwa katika nafasi za juu kama mawaziri wamehamia upinzani.

Mnyeti
Kwa upande wake, Mnyeti alimtaka Nassari kuacha woga na kuwataja baadhi ya wateule wa Rais aliodai wamekuwa wakiwanunua madiwani wa Chadema waliojiuzulu na kuhamia CCM.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mnyeti alidai katika mkoa huo wateule wa Rais ni wengi hivyo kwa kuwa mbunge huyo alisema ana ushahidi, angewataja wateule hao waliohusika kuwanunua madiwani hao.
“Kuhusu rushwa anazungumzia rushwa ipi, yeye rushwa anayofanya hapa wilayani ni mamilioni ya rushwa au anazungumzia rushwa aliyochukua na Mwenyekiti wa Halmashauri?,”alihoji.

“Akijibu hayo maswali alete na ushahidi wake tutamjibu zaidi,” aliongeza Mnyeti.
Akizungumza na waandishi wa habari jumapili ya wiki hii, Nassari alidai kuwa anao ushahidi usiokuwa na shaka kuhusu madiwani wa Chadema waliojiunga CCM kuwa wamepewa rushwa.

Nassari alisema kuwa yuko tayari kukutana na Rais,Mkurugenzi wa Takukuru,Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai(DCI), Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa,kuwaonyesha ushahidi usiotia shaka na kuwa baada ya siku 14 asipoitwa kuonyesha ushahidi huo atauweka hadharani.

Hadi sasa madiwani tisa wa Chadema wamehama na kuhamia CCM ambapo kati ya hao, watano wanatoka Jimbo la Arumeru Mashariki, Arusha Mjini wawili, Monduli mmoja na Longido mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles