25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

POLEPOLE: KUNA WATU WANAIHUJUMU CCM

*Amwonya Zitto Kabwe, amtaka asikurupuke

 

ELIZABETH HOMBO Na ASHA BANI

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole amefichua siri akisema kuna watu wanakihujumu chama hicho kwa makusudi.

Amesema mfano mzuri ambao unadhihirisha kuwa chama hicho kinahujumiwa ni pale sukari ilipoadimika, ambapo baadhi ya wafanyabiashara walificha bidhaa hiyo kwa lengo la kuuza kwa gharama kubwa.

Polepole alitoa kauli hiyo jana alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Limited inayochapisha magazeti ya MTANZANIA, RAI, BINGWA na DIMBA.

“Tunahujumiwa. Rais alipoanza kazi, lilikuja jambo la sukari hii ilikuwa hujuma kabisa lakini hakuna mtu anasema, sasa naomba ninyi (New Habari) muwe wa kwanza kusema,” alisema.

Ingawa Polepole hakusema wahujumu hao wapo ndani ya chama au nje, lakini alisisitiza uamuzi wa kujitenga na marafiki wezi wasiokuwa na nia njema na chama hicho.

“Ifike mahali tuweze kujitenga wakati mwingine na rafiki mwizi. Ubinadamu ni kuamua kuwa na rafiki mwizi au kuishi kama binadamu mwema au ukajitenga na mwizi ambaye ni rafiki yako.

“Rais alipokuja alisema Tanzania ya viwanda na msingi wake ulikuwa ni kuprotect (kulinda) viwanda vya ndani ambavyo vinaajiri watu kwa sababu teknolojia  yetu iko chini.

“Tunaajiri watu wengi, hivyo  fedha inayopatikana kwenye sukari inalipa watu wengi kwenye hiyo chain (mnyororo) mpaka inapatikana sukari.

“Sasa wapo wafanyabishara wakaona ni bora kuagiza sukari nje ambayo imetengenezwa kwa mfumo mbaya kwa hiyo inakuwa cheaper na sukari ya nje ikiingia ya ndani haipati soko.

“Baadaye  kiwanda kinaendeshwa kwa hasara na watu watashindwa kulipwa fedha zao na baadaye anayenyonywa ni mkulima anayelima miwa na mkulima akinyonywa kura za CCM zimepungua.

“Binafsi nimeliona hili kwa macho yangu kwa makusudi kabisa  wameficha sukari na imeshaleta taharuki lakini tukahangaika sana likapoa,” alisema.

Polepole alisema baada ya suala la sukari kushughulikiwa likazuka jingine. “Hilo lilipotulia likaja jingine hela hamna, hela hamna!

“Tulimtaka Rais ambaye ataimarisha nidhamu ya utumishi wa umma, matumizi ya Serikali kwa sababu watu walikuwa hawalipi kodi tukaona matumizi hayo yatumike kihalali kwa sababu kuna watu walikuwa hawalipi kodi na kuna ambao walikuwa wananufaika na hela hii ya rushwa. Hivyo lengo la Rais ilikuwa ni kukata mianya ya wakwepa kodi.

“Sasa nilidhani upinzani wangekuwa mstari wa mbele kulieleza hili kwa kuleta nidhamu kwa sababu tukishaimarisha nidhamu sasa tunaachilia hela kwa watu…sasa mtu anaanza kuvumisha hela hakuna uchumi wa ovyo sasa unaleta taharuki kwa watu.

“Kwa sasa hakuna matumizi mabaya ya fedha za umma na kama kuna mikutano ndani ya  taasisi za Serikali basi inafanyikia katika kumbi za ofisi za Serikali, nashangaa watu kusema ohoo kwa sasa hoteli zinafungwa, mara hakuna wateja sasa je utaamuaje kujenga hoteli huku hujui wateja wako ni akina nani?,’’ alihoji.

Polepole ambaye alipata kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma na baadaye Ubungo, alisema chama chake hivi sasa kinafanya siasa za maendeleo na si siasa za madaraka.

“Niko hapa kujenga demokrasia ya kweli na sipo kwa ajili ya kujibu watu. CCM ikiamua kugeuka ni fursa kubwa kwa Watanzania… Huko nyuma tumejifunza kutokana na namna ambayo inaumiza lakini sasa naiona nidhamu ndani ya CCM,” alisema.

Alisema wananchi wamekaa wakisubiria ile ahadi ya Sh milioni 50 kila kijiji na kwamba fedha hizo zinapatikana kutokana na makusanyo mbalimbali.

Alitolea mfano katika Halmashauri ya Ubungo ambapo wanakusanya Sh bilioni 24 hadi 25 kwa mwaka fedha ambazo zikitengwa zinatosha kutenga fungu la vijana na wanawake.

Katika hatua nyingine Polepole alimwonya Mbunge Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) kutokana na kauli yake kwamba ataweka ubunge wake rehani endapo Serikali itamwonesha tani milioni 1.5 za mahindi.

“Zitto asirudie tena ole wake, tutachukua ubunge wa wake katika nchi kuna namna nyingi za kuhifadhi chakula siyo hadi aaone yeye (Zitto), anang’ang’ania hifadhi moja ya NFRA sisi hatuna matatizo ya chakula wenye matatizo ni Kenya, mwambieni asirudie tena vijana wa mjini wanasema tutakula kichwa,” alisema.

Polepole ambaye alipata kuwa mjumbe Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema suala la Katiba ni jambo zito ambalo wananchi walitaka kuwepo kwa utatuzi wa kero ya Muungano.

“Bila kujali iwe ni serikali moja mbili au …nini lakini kero ya muungano ni lazima ziondolewe kama wananchi walivyokuwa wakidai na Rais anatakiwa kufanya kazi hiyo,’’alisema.

Kwa upande wake Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006), Absalom Kibanda akimkaribisha Polepole ofisini hapo, alimshukuru Rais Magufuli kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari.

“Tunakushukuru kwa kututembelea, sisi ni chombo cha habari cha kwanza kututembelea tangu upate nafasi hiyo, karibu sana New Habari.

“Tutaendelea kutoa ushirikiano kwako wewe mwenyewe na chama chako kwa ujumla, pia tunakuomba umfikishie salam mwenyekiti wa chama ambaye pia ni Rais (Dk. Magufuli) kwamba sisi kama chombo cha habari tupo nae bega kwa bega katika kile anachokifanya iwe katika Serikali au katika chama,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles