24.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Polepole atoa onyo wabunge wa CCM

Na MWANDISHI WETU

-MTWARA

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, ameonya wabunge wa chama hicho aliosema wamekuwa na matatizo na Serikali pale inapojitahidi kutatua kero za wananchi.

Polepole alisema hayo jana katika mahafali ya wahitimu wa vyuo vikuu tawi la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Mtwara.

Alisema wabunge hao wajipange kwa 2020 kwa sababu chama hicho kipo pamoja kuanzia Sekretarieti hadi Kamati Kuu.

Alisema lazima wafahamu kwamba katika michakato yote na yeye yumo kama sehemu ya wakataji majina na msemaji wa chama.

 “Kama wewe ni mbunge wa CCM na unashiriki kuendeleza nongwa kwa jambo hili, jipange mapema kwa sababu mimi na wenzangu kuanzia Sekretarieti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu tupo kitu kimoja,” alisema.

Polepole alisema wamelinda utu na heshima ya mkulima kwa kununua korosho na kuhoji wale ambao wanabeza hatua hiyo.

Alisema katika kufanya hivyo, kwanza waliamua kumsaidia mkulima kwa kununua korosho zao ndipo masuala mengine yaendelee.

“’So’ unasema tunanunua halafu itakuwaje, nunua kwanza heshima ya watu isimame, ndoa za watu ziimarike, hapa watu wasingekuwa wamenunuliwa korosho zao, tungekuwa tumeharibu uchumi mzima wa eneo hili,” alisema Polepole.

Alisema kwa sasa korosho ambazo zimenunuliwa na Serikali na kuwekwa kwenye maghala zinatafutiwa utaratibu mwingine.

Polepole pia alionya Bodi ya Mazao Mchanganyiko akitaka itoe pembejeo za kilimo kwa wakati na wakichelewa ataielekeza Serikali kushughulikia watu kwenye bodi hiyo na Wizara ya Kilimo.

Karipio hilo kwa Bodi na Wizara ya Kilimo linakuja ikiwa ni siku chache tangu Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally kusema anaona ndoto mbaya juu ya wizara hiyo na kuwataka kubadilika.

 Jana Polepole alisema; “zile korosho tunaendelea kutafuta utaratibu utawekwa sawa, na watu wawe wabunifu kwenye Wizara ya Kilimo kuliweka sawa jambo hili, mchango mkubwa wa Serikali ni mfano tosha Serikali ya kijamaa inaweza ikasimama na kutetea watu wake.

“Mbona Ulaya wanafanya hivyo kila siku, hapa tunaambiwa tunaishi kwa dola moja kwa siku, Ulaya ng’ombe ndio anaishi kwa Euro mbili kwa siku, na pesa hiyo inatolewa bure na Serikali, sasa kwanini sisi tusitoe pesa hiyo kwa mkulima ambaye ndiye msingi wa uchumi wetu,” alisema Polepole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles