23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

POLAND WATAUKUMBUKA UZEMBE WAO KWA PODOLSKI

Na BADI MCHOMOLO


TASNIA ya michezo nchini Ujerumani inajivunia kuwa na mchezaji kama Lukas Podolski, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alitangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo ya Taifa.

Mchezaji huyo ametangaza kustaafu soka la timu ya Taifa baada ya kuitumikia Ujerumani kwa michezo 130 na kufanikiwa kufunga mabao 49.

Katika washambuliaji wenye kasi kubwa duniani ambao kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, amewahi kukutana nao ni Podolski, kocha huyo alisema hajawahi kumfundisha mchezaji mwenye kasi katika ufungaji mabao kama nyota huyo.

Mshambuliaji huyo alifanya makubwa akiwa amevaa uzi wa Arsenal pale kwenye Uwanja wa Emirates na alifanya makubwa akiwa na timu ya Taifa ya Ujerumani.

Podolski hakuzaliwa nchini Ujerumani, mchezaji huyo alizaliwa katika mji wa Gliwice ambao upo Kusini mwa Poland, mji ambao una wingi wa watu kufikia milioni 2.

Lakini familia ya mchezaji huyo iliamua kuhamia nchini Ujerumani, huku mchezaji huyo akiwa na umri wa miaka miwili.

Podolski ambaye alizaliwa Juni 4, 1985, alianza kuonesha dalili za kucheza soka huku akiwa na umri wa miaka sita, lakini alipofikisha miaka 11 alipata nafasi ya kucheza timu ya vijana ya FC 07 Bergheim nchini Ujerumani.

Wakati anatoka nchini Poland bado alikuwa hana pasi ya kusafiria (Passport), lakini alikuwa na cheti cha kuzaliwa, hivyo alilazimika kuwa na uraia wa nchi mbili ambayo ni Poland na Ujerumani ambako familia yake ilihamia.

Baadaye alipata nafasi ya kuitumikia timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, 18, 19 na 21, hapo ndipo Poland wakaanza kuguswa na uwezo wa mchezaji huyo na kumhitaji arudi kuitumikia timu ya Taifa.

Mchezaji huyo alikuwa tayari kufanya hivyo kwa kuwa bado alikuwa na mapenzi na taifa lake la Poland, lakini aliwaomba wamfanyie mpango wa Pasi ya kusafiria ili aweze kurudi nchini humo kulitumikia Taifa hilo kwenye michuano mbalimbali.

Lakini uzembe wa shirikisho la soka nchini humo ulimfanya mchezaji huyo aendelee kubaki nchini Ujerumani. Poland walishindwa kufanya mpango wa pasi hiyo ya kusafiria hivyo Podolski aliendelea kuitumikia Ujerumani hadi pale alipopata nafasi ya kuitwa ndani ya kikosi cha timu kubwa mwaka 2004.

Kama Poland wangeweza kufanya hivyo mapema kabla ya 2004, basi mchezaji huyo angeitumikia timu hiyo ya Taifa. Kwa sasa Poland wanajuta kwanini walishindwa kutatua tatizo hilo mapema? Kwa kuwa mchezaji huyo ameweka historia ya soka ndani ya klabu ya Arsenal, Bayern Munich, Galatasaray na timu ya Taifa ya Ujerumani.

Kwa kuwa Ujerumani walitambua thamani ya mchezaji huyo kutokana na uwezo wake, leo hii wamefurahia kumuaga kwa furaha kubwa mbele ya idadi kubwa ya mashabiki ambao walithamini mchango wake.

Anajivunia makubwa ambayo ameyafanya ndani ya timu ya Taifa ya Ujerumani ikiwa ni pamoja na kujiwekea rekodi mbalimbali.

2006 ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano ya Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani, katika michuano hiyo aliweka historia ya aina yake ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili kwenye mchezo mmoja ndani ya dakika 12, huku mara ya mwisho ilitokea 1962.

Hata hivyo, katika michuano hiyo Ujerumani ilimaliza nafasi ya tatu huku mchezaji huyo akishika nafasi ya pili kwa ufungaji bora baada ya kufunga mabao matatu sawa na Ronaldo, Thierry Henry, Fernando Torres, David Villa, Maxi Rodriquez, Hernan Crespo na Zinadene Zidane.

Hata hivyo, mchezaji huyo alijizolea sifa na kutajwa kuwa mchezaji bora kwa wachezaji wenye umri mdogo kwenye kombe hilo la dunia.

Mchezaji huyo alikuwa katika kikosi cha Ujerumani ambacho kilishiriki michuano ya Euro 2008, 2012, 2016 pamoja na Kombe la Dunia 2010.

Miongoni mwa kitu ambacho atakikumbuka mchezaji huyo ni pamoja na kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Dunia 2014.

Kipindi hicho chote Poland walikuwa wanamwangalia mchezaji huyo ambaye walishindwa kumfanyia mpango wa pasi ya kusafiria.

Wiki iliyopita itakuwa ya kumbukumbu kwa mchezaji huyo kwa kuwa alicheza mchezo wa mwisho katika kikosi cha Ujerumani na kufunga bao lake la mwisho huku Ujerumani ikishinda bao 1-0 dhidi ya England katika mchezo wa kirafiki.

Wajerumani walishindwa kuzuia hisia zao kwenye uwanja huo wa Dortmund ambapo Podolski alicheza mchezo wake wa mwisho, mashabiki waliimba wimbo kwa Kijerumani huku wakisema ‘Danke podolski, deutsch wird sich an sie erinnern‘ wakiwa na maana kwamba ‘Asante Podolski, Ujerumani itakukumbuka’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles